Wakuu kuna hoja huwa nakutana nayo mtandaoni kuwa kunyonyesha humsaidia mama kujikinga dhidi ya saratani ya matiti.
Je, vipi kwa ambaye tayari amebainika kuwa na Saratani ya matiti kunyonyesha ni salama na kunaweza kusaidia kuondoa saratani?
Je, vipi kwa ambaye tayari amebainika kuwa na Saratani ya matiti kunyonyesha ni salama na kunaweza kusaidia kuondoa saratani?
- Tunachokijua
- Kansa ya matiti ni aina ya kansa ambayo huanza kadri ya ukuaji wa seli katika tishu za matiti. Kansa hii mara nyingi imekuwa ikiwakumba wanawake zaidi ukilinganisha na wanaume japo yeyote anaweza akapatwa na ugonjwa huu.
Zipo sababu kadhaa ambazo zinaweza kusababisha ugonjwa huu ikiwemo, kuwa na familia yenye historia ya kuwa na ugonjwa huu, kuwa na historia binafsi ya kuwahi kukumbwa na ugonjwa huu mfano mtu aliyewahi kupata kansa ya titi la upande mmoja ipo hatari pia ya kupatwa katika titi la upande wa pili, kuanza kwa hedhi katika umri mdogo mfano chini ya miaka 12, utumiaji wa vilevi, kupata mtoto katika umri mkubwa na kadhalika.
Tafiti zinaeleza kuwa unyonyeshaji unaozalisha maziwa (mama wenye watoto) husaidia kupunguza hatari ya kukumbwa na ugonjwa huo. Hivyo wanawake wanashauriwa kunyonyesha watoto wao kwa muda mrefu ili kusaidi kupunguza hatari ya kupatwa na saratani ya matiti.
Tovuti ya Mayo clinic inaeleza kuwa endapo mwanamke akiwa ana mtoto mdogo, kunyonyesha kunaweza kusaidia katika kuzuia saratani ya matiti. Kadri unavyonyonyesha kwa muda mrefu, ndivyo ambavyo uwezakano wa kujikinga unaweza kuongezeka.
Kuhusu mama aliyebainika kuwa na Saratani ya matiti, Je, ni salama kunyonyesha na kunaweza kusaidia kuondoa saratani?
Wataalamu wanasema kuwa kwa kawaida unyonyeshaji wa mtoto unapaswa kusitishwa mara tu matibabu ya saratani yanapoanza. Dawa nyingi zinazotumika kutibu saratani, ikiwemo kemotherapi, tiba za homoni na tiba lengwa (targeted therapy), zinaweza kupita kwenye maziwa ya mama na kumdhuru mtoto.
“Dawa za kemotherapi zinaweza pia kuathiri seli nzuri mwilini, zikiwemo zinazozalisha maziwa ya mama,” anasema Dkt. Sudha Sinha, Mkurugenzi wa Kliniki ya Saratani katika Hospitali za Yashoda, Hyderabad, kutoka nchini India akizungumza na India Today.
Inaelezwa kuwa kunyonyesha kwa kawaida hakushauriwi ikiwa mama anapokea matibabu ya saratani yanayoathiri mwili mzima au ikiwa kuna uwezekano wa maziwa kuchafuliwa na dawa.
Kwa upande wa mionzi (radiotherapy), ikiwa inalenga sehemu nyingine za mwili tofauti na matiti, uwezekano wa kuathiri unyonyeshaji huwa mdogo, ingawa hutegemea kiwango cha mionzi na eneo linalotibiwa.
Dkt. Sinha anashauri kuwa kupunguza taratibu vipindi vya kunyonyesha kunaweza kurahisisha mpito huo kwa mama na mtoto. Mama pia anaweza kupata msaada kutoka kwa wataalamu wa unyonyeshaji, wanasaikolojia au washauri wa afya.
Inaelezwa mama anaweza au asiweze kunyonyesha kutegemea aina ya matibabu anayopokea. Katika baadhi ya hali, wanawake wanaopokea tiba ya mionzi wanaweza kuendelea kunyonyesha, lakini usalama wake hutegemea aina ya matibabu, hivyo ni muhimu kushauriana na daktari kabla ya kufanya uamuzi.
Ingawa saratani haiwezi kuambukizwa kwa mtoto kupitia maziwa ya mama, baadhi ya matibabu kama kemotherapi, tiba za homoni na tiba lengwa yanaweza kupita kwenye maziwa na kumdhuru mtoto, hivyo kunyonyesha hushauriwa kusitishwa.