Dar es Salaam.
Wakati mama na dada wa marehemu Hamza Mohammed wakiachiliwa baada ya mahojiano, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema bado wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo.
Hamza aliuawa na polisi Agosti 25, mwaka huu baada ya kuwaua kwa risasi askari wanne, watatu kati yao wa polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi, jirani na ulipo Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi liliwakamata ndugu kadhaa wa Hamza waliokuwa jijini na Dar es Salaam na wengine Chunya mkoani Mbeya.
Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu watu waliokamatwa kutokana na tukio hilo jana, Kamanda Muliro alisema; “Jamani nyie hamtaki tupeleleze? Ni sahihi tuseme hadi wapo mahabusu namba ngapi? Ametoka au hajatoka? Ndugu yangu Mwananchi!”
Wakati Muliro akisema hayo, Msemaji wa familia ya Hamza, Abdul-rahman Hassan aliliambia Mwananchi kuwa watu takribani saba wakiwamo mama na dada wa Hamza wameachiwa na wengine watano wanaendelea kushikiliwa na polisi.