Inasikitisha sana.
Shetani anapotamalaki juu ya nchi, haki hupotea, majuto na huzuni huenea, uonevu huwa furaha ya watawala, ibilisi hufurahia uwezo wa kutwaa uhuru wa watu, machozi ya wenye haki hudondokea mavumbini, Bwana wa mbingu huruhusu ubaya udhihirike ili shetani apate kuonekana kwa uwazi. Mioyo ya wenye hekima hutiwa upofu na woga. Ibilisi hujisifia kwa mateso ya wana wa Mungu.
Naam, lakini nyakati zaja, ibilisi atakapokanyagwa na nguvu ya Mungu. Ndipo watu wote, walio wa Mungu na mawakala wa shetani, watauchukia uovu na yule bwana wa uovu, yaani shetani. Watazilaani nafsi zao maana hawakutenda lolote lililowapasa kutenda kwaajili ya utukufu wa Mungu wa kweli. Waliwaabudu wanadamu, na walijisogeza kwa ibilisi ili wajipatie mvinyo wenye ladha nzuri bila ya kujali kama mvinyo ule ulikuwa na matone ya damu na machozi ya waliodhulumiwa haki.
Pole sana wafiwa, pole sana Kabendera. Kabendera na wafiwa wote, mkumbuke kuwa katika maisha yetu wanadamu, kila litokealo, limeandikwa katika akaunti zetu za safari yetu ya maisha. Shukuruni katika kila jambo maana Mungu wetu hakuwahi kupungukiwa hekima wala ukuu wake, wala maombi ya wenye haki hayakuwahi kulikosa sikio la Mungu.