SoC02 Mama yangu ni mwanamke jasiri...

SoC02 Mama yangu ni mwanamke jasiri...

Stories of Change - 2022 Competition

Dr NGWAKWA

New Member
Joined
Jul 27, 2022
Posts
2
Reaction score
3
MAMA YANGU NI MWANAMKE JASIRI

Naitwa Moza Nilizaliwa Migato iliyokuwa wilaya ya Bariadi Mkoa wa Shinyanga, Ambayo Hivi Sasa Ipo wilaya ya Itilima Mkoa wa simiyu. Mimi Ni mtoto wa sita (6) Kati ya watoto (12) aliobahatika kupata mama yangu, Ambapo Kati ya hao wanane (8) ndio wako hai huku wanne (4) wakiwa wameshatangulia mbele za haki. Kati ya hai wanane walio hai sita Ni wa kiume na wawili Ni wa kike.

Mama yangu anaitwa Kulwa alizaliwa Malampaka iliyokuwa wilaya ya Maswa mkoa wa shinyanga, Ambayo kwa Sasa ipo mkoa wa Simiyu. Katika familia Yao walizaliwa wayoto watano wote wakiwa wa kike, mama akiwa mtoto wa pili Kati yao Na wote wakiwa hai mpaka Sasa.

Mama amezaliwa na kukulia katika familia ya wakulima wa pamba na mpunga. Baba na mama yao waliwafundisha watoto wao kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu kazi. Mafunzo hayo yalimjengea mama msingi bora wa kuheshimu kazi, kufanya kazi kwa bidii na kujituma pasipo kukata tamaa. Mnamo mwaka 1971 mama alianza darasa la kwanza katika shule ya msingi Malampaka, huku yeye na dada yake wakiendelea kumsaidia baba Yao katika kilimo chake cha mpunga na pamba.

Kutokana na Msingi Bora aliojengewa kutoka nyumbani wa kufanya kazi kwa bidii na kujituma, walimu wake walimpenda sana, kwani alikuwa kifanya vizuri Sana darasani na Hivyo kufanikiwa kushika nafasi ya Kwanza tangu darasa la Kwanza Hadi la Saba.

Mwaka 1977 alihitimu Elimu yake ya Msingi kwa matarajio makubwa ya kufaulu vizuri na kujiunga na Elimu ya Sekondari. Furaha iliyoje, baada ya matokeo kutoka alikuwa amefaulu vizuri kujiunga na Elimu ya Sekondari. Lakini Jambo la kusikitisha na la kukatisha tamaa Zaidi Ni kwamba baada ya matokeo hayo kutoka Baba yake hakumruhusu kuendelea na masomo yake kwa madai kwamba mwanamke Hana haki ya kuendelea na masomo Zaidi ya hapo, kwamba ataishia kuwa muhuni na kushindwa kuolewa.

Alilia Sana kwa muda wa siku tatu pasipo hata kula chakula lakini wazazi wake hawakubadilisha mtazamo wao. Hivyo ilimlazimu kubaki nyumbani kwa Uchungu mkubwa huku akiwasaidia wazazi wake katika shughuli za kilimo huku akisubiri kuolewa. Mara kadhaa huwa akitusimulia Historia yake analia, anasema "Moza mwanangu Soma kwa bidii, Mimi mama yenu sikupota Fursa hii ya kusoma siyo kwa sababu sikuwa na akili darasani, Bali kwa sababu tu ya ubinafsi aliokuwa nao baba yangu".

Mama alikaa nyumbani baada ya kumaliza shule miaka mitano Hadi ilipofika Mwaka 1982, Ambapo alikutana na baba yangu ambaye alienda kijijini kwao Kama Mtendaji wa Kijiji (VEO). Waliishi hapo kijijini kwa miaka miwili Kisha Baba aliachishwa kazi kwa makosa ya Ubadhilifu wa fedha na walihamia katika Kijiji cha Lugulu wilaya ya Bariadi kwa wakati huo ambako ndiko aliko kuwa akiishi Baba kabla ya Kwenda Malampaka Kama Mtendaji wa Kijiji (VEO).

Mama alishangaa Sana baada ya kufika huko na kukuta kumbe baba alikuwa ameoa Tena na watoto wengine wanne, alijuta Sana kwa kuolewa Bila kufanya uchunguzi wa kutosha, Aliamua kurudi nyumbani kwao Tena kwa kutembea kwa mguu na mtoto mgongoni, kuoka Lugulu mpaka Malampaka Ni Umbali wa takribani kilomita hamsini (50) mpaka sitini (60) hivi, lakini alimkuta baba yake akiwa mkali Kama mbogo na alimlazimisha arudi Haraka kwa mme wake, Hivyo ilimlazimu urudi kwa mme wake, mme wake ambaye alikuwa akikaa kwa mama yake. Na Hapa ndipo mateso yalipoanzia.

Kwanza, Mke mwenzake alimnyanyasa Sana kwa sababu katika maeneo ya vijijini kilimo ndiyo njia pekee ya kujipatia chakula, Hivyo kwa vile walirudi katika msimu wa kiangazi kipindi ambacho Hakuna kulima kwa hiyo hakuwa na chakula chake. Kwa sababu walikuwa anapika kwa pamoja Mara kadhaa mke mwenzake alimzuia kupika chakula na unapofika wakati wa kula Kama baba hayupo alipenda kumwambia mama na Hata watoto kuwa "Mnakula Sana utafikiri mlikuwepo wakati wa kulima". Maneno hayo yalikuwa Kama mwiba katika moyo wa mama.

Pili, Mama mkwe wake alimsimanga Sana kwamba hawezi kufanya kazi, Yaani mvivu mvivu. Maneno haya yalimfanya atamani Sana kipindi Cha masika kifike mapema ili amuoneshe kwamba yeye siyo mvivu.
Tatu, Baba alikuwa mlevi kupindukia, Pombe ilimfanya baba kuwa mkorofi na asiyejali kabisa familia yake.

Ilikuwa akirudi nyumbani amelewa anampiga mama na kumlazimisha amchinjie kuku, Siku moja alirudi nyumbani amelewa Sana alimpiga mama na kumfukuza Nyumbani na ilikuwa wakati wa Usiku, Alienda kulala kwa majirani na kulipopambazuka alirudi Nyumbani Lakini alimkuta Baba amefura kwa hasira akiuliza wapi alipolala pasipo kujua kuwa yeye ndiye alimfukuza Usiku uliopita alipokuwa amelewa.

PAMOJA na mambo mengi ya kuumiza aliyokuwa anayapitia kwa wakati huo mama hakukata tamaa kabisa, aliamini kwamba hayo Ni ya muda tu ipo siku yatakwisha.

Baada ya kuona manyanyaso yamezidi kutoka kwa mama mkwe wake, mke mwenzake na mme wake pindi alipokuwa amelewa, aliamua kutafuta sehemu akajenga nyumba ya matope na paa la Nyasi Huko migato walaya ya Bariadi kwa wakati huo na kuanza maisha yake. Na huko ndiko nilikozaliwa Mimi, Alinipa jina la MOZA, Akimaanisha kuwa naanza moja, Baada ya changamoto na kifo Cha mtoto wake Kutokana na utapiamlo.

Baba hakuwa mtu mbaya wakati Alipokuwa ajanywa Pombe, Hivyo alimuunga mkono katika uamzi huo japokuwa ilikuwa Ni Kama kishingo upande moyoni akijisemea "Ngoja nione Kama atafanikiwa". Msimu wa kilimo ulipofika mama alilima kwa bidii zote, Wakati mwingine lalitafuta vibarua vya kupalilia mashamba ili angalau apate chakula kwa ajili ya kulisha watoto wake.

Wakati huo alikuwa akinyonyesha mtoto wake wake wa tatu, Kutokana na kushinda shambani muda mwingi na kukosa lishe Bora afya yake ilidhorota Sana Jambo lilipolekea kukosa maziwa na matokeo yake mtoto alipata utapiamlo. Alipambana kadri iwezekanavyo Kuhakikisha anaokoa afya yake na ya mtoto Lakini bahati haikuwa upande wake mtoto wake alifariki dunia Kutokana na kukosa huduma Bora za kiafya kwa sababu ya maisha duni. Kwa kweli kilikuwa Ni kipindi kigumu Cha kuvunja moyo Sana kwa mama, Lakini alipiga moyo konde na kusimama imara Tena.

Mungu hamtupi mja wake bwaba! Msimu wa mavuno ulipofika mama alipata mavuno ya kutosha kabisa, chakula kilikuwa Cha kutosha kabisa, kingine aliuza akanunua Ng'ombe kwa ajili ya kumsaidia katika kilimo si unajua maisha ya kijijini.

Hapo maisha yalianza kuwa na ahueni kidogo. Mke mwenzake alianza kumchukia Tena Kutokana na mafanikio aliyokuwa ameanza kuyapata, mara Nyingi alikuwa akimsingizia mambo mengi ya uongo na kumchongea kwa baba ili amchukie, Lakini bahati nzuri baba alikuwa ashaanza kuona ndoto njema inaanza kuwaka upande wa mama kwa hiyo hakujali maneno hayo.

Mwaka mmoja baadaye mama alipata mtoto mwingine ambaye bahati mbaya alikuwa na shida kwenye moyo, aliishi kwa takribani Mwaka mmoja na nusu na Kisha alifariki dunia. Hili likawa pigo lingine kwa mama, Maneno akawa mengi Sana, wengine wakasema Ni laana na kadharika. Lakini hakujali aliendelea kuwa imara na kusonga mbele. Mungu alimbariki kupata mtoto mwingine wa kiume ambaye ndiyo Mimi ninayekusimulia Habari hizi. Na baada yangu wengine wawili walizaliwa.

Mnamo Mwaka 1999 kulikuwa na njaa katika sehemu Nyingi za Tanzania Kutokana na mvua kunyesha kupita kiasi (Elnino), wengi watakumbuka hii. Njaa hii iliondoka na Ng'ombe ambazo mama alikuwa amezinunua, kwa hiyo maisha yakawa magumu Tena, kipindi hicho ulikuwa Unaweza kuuza Ng'ombe mmoja na kurudi na gunia moja la mahindi! Unaweza usiiamini hii Lakini ndivyo ilivyokuwa.

Mvua ilipoanza kupungua tuliingia Tena shambani kwa nguvu Kama kawaida tukiongozwa na mama yetu. Mungu alibariki kazi ya mikono yetu, mazao yalistawi Sana, Lakini Hata kabla mahindi hayajakomaa vizuri tulianza kuvuna kuchemsha ili angalau kujipatia mlo wa siku, kwani ilikuwa si ajabu kula mchicha na kulala baadhi ya siku, kwa hiyo hiyo ilikuwa Ni ahueni.

Nakumbuka siku moja tulipura mahindi kabla hayajakauka vizuri Kisha tukayaanika ili yakauke tusage tupate unga, Bahati mbaya jua halikuwaka kwa siku kadhaa Hivyo mahindi yakashindwa kukauka, Ilitulazimu kuyakausha kwa kutumia Moto ndani ya kalai huku tukiyachunga yasiungue na kuwa kama yamekaangwa. Wakati tunafanya hayo mama alikuwa akituambia "Najua ipo siku mtakuwa na maisha mazuri na hamtayakumbuka haya Tena" Mama hakuwahi kukata tamaa na siku zote alikuwa akitutia moyo kutokata tamaa na kufanya kazi kwa bidii.

Tulisoma kwa bidii na Mungu alikuwa upande wetu, Kaka yangu na Mimi pia mara kadhaa tulishika bafasi ya Kwanza Darasani na ikitokea hatujashika nafasi ya Kwanza Basi hatuwezi vuka nafasi ya tatu. Wakati huo baba yetu alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya shule na alijivunia Sana sisi tulipokuwa tunafanya vizuri, tulifaulu kwenda Sekondari tukafanya vizuri pia.

Mwaka 2007 mambo mengi ya kusikitisha Sana yalitokea Ambayo yalimuumiza sana mama, Kwanza, mama yake mzazi alifariki na Muda si mrefu mtoto wake pekee wa kike kwa wakati huo alifariki pia kwa Ugonjwa ambao Kila hospital walipienda haukuonekana.

Hali hiyo haikumuathiri yeye tu Bali Hata Mimi ili niathiri vibaya Sana. Nilikaa siku kadhaa kwa upweke pasipo kuongea na mtu yeyote. Siku moja aliniita na kuniuliza "kwa Nini upo katika Hali hiyo?" Nilimjibu Niko salama, Sina shida yoyote. Nafikiri yeye Kama mzazi alitambua Hali yangu kuliko Mimi mwenyewe ilivyokuwa ninajitambua. Alinikalisha na kuongea na Mimi mambo mengi ya kutia moyo, pia alinisomea mstari kutoka katika biblia 2Wathesalonike 4:13, ambao ulinitia moyo Sana na sikukata tamaa Tena na huzuni yote niliyokuwa nayo ikapotea.

Haikutosha Mwaka mmoja baadaye mama alipata mtoto mwingine ambaye likuwa wa kike Kama ambaye alitangulia mbele za haki, Alifurahi Sana aliamini kuwa pengo Sasa limezibwa. Lakini mtoto huyu mzuri baada ya siku 5 alilala moja kwa moja asiweze Kuamka Tena. Huzuni iliyoje, huyo aliyekuja kufuta machozi naye kaondoka Tena. Kama familia Tulibaki na huzuni isiyokuwa na majibu kwa Muda mrefu, Lakini hatimae tulitiana moyo kusonga mbele Tena, maana Kazi ya Mungu haina makosa.

Licha ya kututia moyo sisi kuendelea kupambana kumbe yeye alikuwa akiumia Zaidi sema hakutaka tutambue Hilo, Kwani muda si mrefu tokea hapo pressure yake ilia za kuwa juu, miguu ikawa inavimba na Tumbo likawa kinavimba pia, Alipelekwa hospital na kufanyiwa vipimo mbalimbali na majibu yalivyotoaka tuliambiwa kuwa moyo umekuwa Mpana. Kwa wakati huo sisi tulikuwa shuleni na hakutaka tufahamu tusije tukawa na mawazo na kushindwa kusoma vizuri. Ugonjwa huo ameendelea nao Hadi Sasa.

Pamoja na hayo habari za kutia moyo Ni kwamba Kila mtoto wake aliyepata Fursa ya kwenda shule na kusoma alisoma, Wote wanaishi maisha ya amani na furaha Hata Kama siyo ya kitajiri sana Lakini ya amani na Furaha. Na mpaka Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo chuoni akiendelea na masomo licha ya changamoto hizo zote. Na mama yetu anajivunia kwa kile alichokipigania Zaidi ya miaka 30 iliyopita. Akiyaona matunda ya taabu zake huwa anafurahi na kusahau shida alizozipitia.

Niseme tu kwamba upendo wake ujasiri wake, na bidii zake ndizo zimetufikisha hapa.Neno moja kwa wazazi wote, Hatima ya maisha ya watoto wenu ipo mikononi mwenu, watie moyo Kila wakati Hata Kama wewe mwenyewe unaumia, wanenee mema na kuwaombea siku zote, Kisha wapiganie na wasaidie waweze kufikia ndoto zao, huku ukiwafundisha kufanya kazi kwa bidii na kupigania kile wanachokiamini Hata Kama mbeleni kunaonekana kuwa giza nene.

Mungu wabariki wazazi wote wanaopambana kwa ajili ya Hatima za watoto wao.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom