Aliko Musa
JF-Expert Member
- Aug 25, 2018
- 209
- 315
Njia mojawapo ya kuongeza thamani ya nyumba yako ya uwekezaji ni kuifanyia ukarabati. Ongezeko la thamani ya nyumba kutokana na ukarabati wa nyumba hutegemea sana maarifa sahihi aliyonayo mwekezaji husika.
Hivyo, ili uweze kufanya ukarabati wenye tija zaidi unahitaji kuwa na maarifa sahihi na taarifa sahihi. Pia, wanatimu (mafundi ujenzi, fundi seremala, fundi aluminiamu, mshauri mbobezi, n.k) watakusaidia sana kufanya ukarabati wenye tija.
Kuna chanagamoto mbili (2) za kuuza nyumba ndani ya miaka (2). Chanagamoto hizo ni kama ifuatavyo;-
✓ Kufahamu muda wa kukamilisha ukarabati.
✓ Kufahamu idadi ya miezi ya kumiliki nyumba unayonunua.
Changamoto hizi mbili (2) ni muhimu sana kuandaa suluhu zake ili uweze kuwekeza kwa mafanikio makubwa.
Kwenye sehemu hii ya kwanza ninachambua mwongozo wa kukuwezesha kufahamu muda na kufupisha muda wa ukarabati wa nyumba.
Mwongozo Wa Kutambua Na Kufupisha Muda Wa Ukarabati.
Moja.
Ongeza muda zaidi ya ukarabati baada ya kuambiwa na mafundi.
Makisio mengi ya muda wa kukamilisha ukarabati hufanyika kwa uzoefu na maarifa ya mafundi husika. Mafundi hao wanakuwa hawawezi kufikiria kuhusu dharura na changamoto nyingine.
Hivyo ili kuepuka migongano, unatakiwa kuongeza siku zaidi za ukarabati juu ya muda ulioambiwa na mafundi wako.
Mbili.
Fanya karabati nyingi kwa wakati mmoja.
Wakati nyumba inaendelea kupakwa rangi, endelea kupanda bustani nje na kuandaa mazingira ya nje ya nyumba. Usifanye ukarabati wa aina moja kwa wakati mmoja.
Kwa kufanya ukarabati wa tofauti tofauti tofauti utaweza kukamilisha ukarabati na maboresho ndani ya siku chache.
Tatu.
Tafiti na fuatilia sana kuhusu ukarabati bora na maboresho ya nyumba.
Jifunze kwa bidii. Uliza kutoka kwa mafundi tofauti tofauti. Soma ripoti nyingi za ukaguzi wa nyumba. Kuwa na fundi mmoja mzoefu sana kwenye eneo la ukarabati na maboresho ya nyumba.
Waombe wawekezaji wengine wakupe mawasiliano ya mafundi wanaofanya ukarabati kwa ubora wa hali ya juu sana. Hawa watakusaidia kukamilisha ukarabati wenye tija kwako.
Nne.
Pata Ripoti Namba 2.
Kamwe usiwe mfuasi wa ripoti namba 1. Ikiwa fundi mmoja atakupa ripoti namba 1 na kukuambia kuwa ukarabati utakamilika ndani ya siku mbili (2).
Kinachofuata ni kutafuta ripoti namba 2 kutoka kwa fundi mwingine ambaye pia ni mzoefu kwenye ukarabati wa nyumba za kuuza ndani ya miaka miwili (2).
Ripoti zote mbili (2) ni lazima zigusie maeneo matatu (3) kama ifuatavyo;-
✓ Makisio ya jumla ya gharama za ukarabati kwa kuainisha kila mahitaji ya gharama ndogondogo.
✓ Makisio ya idadi ya waajiriwa wa ukarabati na maboresho ya nyumba.
✓ Makisio ya jumla ya idadi za siku za kukamilisha ukarabati.
Tano.
Uliza maswali kutoka maduka ya vifaa na malighafi ya ujenzi.
Wauzaji wa maduka ya vifaa vya ujenzi maarufu kama HARDWARE STORES wana uzoefu mkubwa kuhusu ukarabati wa nyumba. Hivyo hawa ni chanzo kizuri pia cha kupata taarifa sahihi na maarifa sahihi kuhusu ukarabati wa nyumba.
Hakikisha unalenga mambo matatu (3) niliyo orodhesha kwenye kipengele namba 4 wakati wa kuwahoji wauzaji wa vifaa vya ujenzi.
Kwa walio wengi watakujibu maswali yako kwa uaminifu mkubwa wakiamini utakuwa mteja wa vifaa vyao na malighafi wanazouza.
Sita.
Tafuta vyanzo kutoka kwenye mtandao wa intaneti.
Usisahau kujifunza kutoka kwenye mtandao wa intaneti. Huko yapo mambo mengi ambayo ukiunganisha na maarifa uliyopata utafanikiwa kwenye zoezi lako la ukarabati wa nyumba.
Mwongozo Wa Kufahamu Muda Wa Umiliki Wa Nyumba.
Hii ni kwa ajili ya wawekezaji kwenye nyumba za kuuza ndani ya miaka miwili (2) tu (flipping houses). Mwongozo huo ni kama ifuatavyo;-
Moja.
Tafuta dalali mzoefu.
Hakikisha unakuwa na dalali mbobezi kwenye ardhi na majengo. Huyu atakukutanisha na mtandao mkubwa wa wawekezaji kwenye ardhi na majengo.
Usiuze nyumba bila dalali ukiamini kila kitu kitakwenda sawa. Waulize wawekezaji wengine kuhusu dalali ambaye ana jina kubwa la huduma za udalali wa viwanja, mashamba na nyumba.
Mbili.
Toa zawadi kwa dalali bora.
Mpe mkakati maalumu dalali wako. Mpe ahadi ya kumuongezea asilimia ya kamisheni baada ya kukamilisha kazi yake kwa ubora wa hali ya juu kulingana na mahitaji yako.
Mfano wa ahadi; nitakulipa 6% ya kamisheni, badala ya 5% endapo utapata mnunuzi wa kununua nyumba hii kwa shilingi milioni hamsini (50) ndani ya siku 30.
Ahadi hii iandike kwenye mkataba kati yako na dalali wako ili kumhakikishia kuwa wewe ni mwekezaji mwaminifu. Usimpe maneno matupu.
Tatu.
Tangazo la mauzo kabla ya kukamilisha ukarabati.
Hakikisha unaanza kutangaza kuuza nyumba yako kabla ya kukamilisha ukarabati na maboresho ya nyumba yako.
Matangazo ya kuuzwa kwa nyumba huchukua muda mrefu, hivyo ni muhimu sana kuanza kutangaza mapema.
Tangulia na ukarabati wa urembo wa nje ya nyumba. Mara baada ya kukamilisha ukarabati wa urembo wa nje ya nyumba, mwambie dalali aanze kutangaza kuuzwa kwa nyumba yako.
Nne.
Panga bei ya kuuzia nyumba yako.
Dalali wako anatakiwa kuzingatia makundi matatu (3) ya bei za kuuzia nyumba kama ifuatavyo;-
✓ Bei ya haraka. Hapa ni pale muuzaji anatakuwa tayari kuuza nyumba kwa punguzo la bei kutokana na hamasa aliyonayo.
✓ Bei ya wastani. Hii ni bei ambayo muuzaji huuza kulingana na bei ya kuuzia sokoni aina ya nyumba anayouza.
✓ Bei ghari. Hii ni bei ya kuuzia ambapo muuzaji hawezi kuuza kwa punguzo la bei kwa kulinganisha na bei ya kuuzia nyumba hiyo ya uwekezaji.
Rafiki yako,
Aliko Musa.
Mbobezi wa ardhi na majengo.
Whatsapp/phone calls; +255 752 413 711