Katika pita pita zangu asubuhi hii, nikasema nikae kidogo kwenye kijiwe cha kahawa, nichangamshe kinywa na kufurahia upepo mwanana wa alfajiri. Watu walikuwa kwenye gumzo, kila mmoja akitoa maoni yake juu ya hali ya maisha, siasa, na bila shaka, mpira wa miguu. Lakini ghafla, mada moja iliyoibuka ilinifanya nishtuke – eti rushwa ya ngono inatawala soka la Tanzania, hasa katika timu kubwa!
Nikatulia kidogo nikitafakari. Kwa haraka haraka, akili yangu ilikataa wazo hili. Hivi kweli kuna wanawake wenye mamlaka ya juu kiasi cha kuwalazimisha wachezaji wa Simba au Yanga kulala nao ili wapewe nafasi ya kucheza? Wazee wengine waliokuwa kwenye kijiwe nao wakaonekana kushangaa kwa mtazamo kama wangu. Lakini mtoa mada hakukata tamaa:
"Naona hatuelewani," akasema kwa msisitizo. "Wachezaji wanaliwa mchicha ndio wanapata mkataba."
Kijiwe kizima kikasema kwa mshangao mkubwa: "Astaghafillulah!"
Mzee akaendelea kueleza kwamba si jambo la ajabu kwa watu wenye mamlaka katika soka – iwe ni makocha, mawakala, au viongozi wa timu – kutumia nafasi zao vibaya na kuwatumia wachezaji vijana kwa tamaa zao binafsi. Akaongeza kuwa, kama ilivyo katika sekta nyingine, kuna watu wenye tabia za ajabu ambao huona vijana kama vyombo vya kufanikisha matamanio yao badala ya vipaji vya kuendelezwa; Hapa nikakumbuka Kuna mchezaji fulani alitoka Yanga kwenda Azam kwa ugomvi na sahizi anarudi, nikakumbuka interview yake alivyokuwa anajing'atang'ata kwamba alikuwa "anateseka" nikasema kimoyo moyo "labda ndio mambo hayo"
Kwa haraka nikaanza kuwaza jinsi sekta ya muziki nchini ilivyojaa uvumi wa wasanii – wa kiume na wa kike – wanaolazimika "kulipa fadhila" kwa njia ambazo si za kawaida ili wapate nafasi ya kung'ara. Na hapo ndipo nikajiuliza, je, kuna uwezekano kwamba hata katika soka mambo haya yanatokea? Je, kuna wachezaji ambao wameathirika na mfumo huu lakini hawana pa kusemea?
Nikakumbuka hadithi za kimataifa za wachezaji kama Andy Woodward, aliyefichua unyanyasaji wa kingono alioupitia akiwa kinda huko Uingereza, au yale madai yaliyowahi kumkumba Sepp Blatter, aliyekuwa Rais wa FIFA, kuhusu tabia zake zisizofaa. Kwa Afrika, hizi habari hazisikiki sana – lakini hilo linamaanisha hazipo?
Labda kuna ukweli fulani ndani ya gumzo la kijiwe hiki. Labda bado tunaishi katika jamii inayodhani kuwa rushwa ya ngono ni tatizo la wanawake pekee, huku vijana wa kiume wakilazimika kunyamaza kwa hofu ya kudharauliwa au kupoteza ndoto zao. Lakini je, tunapaswa kupuuza madai haya kwa sababu yanaonekana kutovutia macho yetu kwa haraka?
Swali linabaki: Je, kuna watu wanaoliwa viboga kwa tamaa za mafanikio? Na kama jibu ni ndio, tunafanya nini kama jamii kuhakikisha kuwa soka, muziki, na sekta zingine zinabaki safi kwa vipaji vyote vinavyoinuka?