Sam Gidori
Senior Member
- Sep 7, 2020
- 165
- 417
Upi mtandao sahihi zaidi wa kijamii unaoweza kuutumia kutangaza biashara yako mtandaoni?
Tangu kuvumbuliwa kwa mtandao wa intaneti miaka 60 iliyopita, mapinduzi ya teknolojia yamerahisisha mawasiliano kwa kiasi kikubwa. Moja ya mabadiliko hayo ni uwezo wa kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi kupitia mitandao ya kijamii. Mtandao wa kwanza wa kijamii ulianza kutumika rasmi mwaka 1997, ukiwa na lengo la kuwakutanisha watu mtandaoni kwa lengo la kufahamiana na kuwasiliana. Lakini matumizi ya mitandao ya kijamii yamebadilika, yakihusisha Zaidi matangazo ya kibiashara.Katika sehemu ya kwanza, tuliangalia faida za kutumia mitandao ya kijamii kibiashara, hasa kutokana na wingi wa watumiaji wa mitandao hiyo. Baada ya kufahamu faida za kutumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara yako, swali utakalokuwa ukijiuliza ni ‘Je, ni mtandao gani sahihi wa kijamii wa kutumia katika kutangaza biashara yangu?’
Kuna mitandao ya kijamii Zaidi ya 100 duniani, lakini mitandao mikubwa ya kijamii yenye watumiaji wengi zaidi duniani si zaidi ya mitandao 10. Hakuna gharama yoyote ya kujisajili katika mitandao ya kijamii, na mtu yeyote mwenye uwezo na kifaa cha intaneti anaweza kujiunga na mitandao hii ya kijamii.
Kabla ya kufanya uamuzi wa mtandao sahihi wa kuutumia kutangaza biashara yako, tuangalie mitandao mikubwa mitano ya kijamii inayopatikana katika eneo la Afrika Mashariki, pamoja na faida na hasara zake utakapotumia kutangaza biashara yako.
1. Facebook
Mtandao wa Facebook ulianzishwa kwa lengo la kuwasiliana na ndugu na marafiki, hivyo mwonekano na mpangilio wa vifaa vyake umewekwa kwa lengo la kuunganisha marafiki. Facebook ina watumiaji hai takriban bilioni 1 kila siku, bila shaka ni moja ya mitandao inayotumika zaidi duniani. Hata hivyo, mtandao wa Facebook unafaa kibiashara, hasa kutokana na wingi wa watumiaji wake na maboresho ya mwonekano wa kibiashara yanayoendelea kufanywa na mtandao huo, hasa kwa upande wa matangazo ya mtandaoni.
Zaidi, mtandao wa Facebook ni sehemu nzuri ya kuwasiliana na wateja wako. Unaweza kuanzisha kundi katika mtandao wa Facebook ambapo unaweza kukutana na kujadili na wateja wako, kuwauliza maswali na kuwafahamisha moja kwa moja kuhusu biashara yako.
Faida za Kutumia mtandao wa Facebook kibiashara
- Uwezo wa kuwafikia wateja wengi
- Uwezo wa kuchagua aina ya wateja unaoweza kuwafikia
- Uwezo wa kuwasiliana moja kwa moja na wateja
- Uwezo wa kufanya uchambuzi baada ya kuchapisha matangazo (analytics)
Hasara za kutumia mtandao wa Facebook kibiashara
- Matangazo ya kibiashara ya Facebook yanahitaji gharama kubwa kulinganisha na mitandao mingine ya kijamii
- Inahitaji kuwekeza muda wa kutosha ili kukutana na wateja wako
- Pale ukurasa wako wa mtandao wa Facebook unapofungiwa ni ngumu kuurejesha.
2. Instagram
Mtandao ulioanzishwa kwa lengo la kushirikisha picha mwaka 2010 umejizolea umaarufu mkubwa hasa kwa vijana, ukiwa na zaidi ya watumiaji hai bilioni 1 kwa siku, na kuufanya kuwa moja ya mitandao inayoongoza duniani kibiashara. Licha ya kuanza kama jukwaa la kushirikisha picha, Instagram imepelekea mapinduzi katika matangazo ya biashara kwa kuweka mfumo mzuri wa matangazo na kuuza bidhaa mtandaoni, ikiwemo mfumo unaokuwezesha kufuatilia bidhaa kwa kuonesha sehemu mbalimbali za bidhaa hiyo ndani ya picha moja.
Faida za kutumia mtandao wa Instagram kibiashara:
- Mwonekano mzuri wa bidhaa kwa kutumia picha na video unaoweza kumvutia mteja
-Instagram ni maarufu zaidi kwa vijana ukilinganisha na Facebook
- Instagram imetengenezwa mahsusi kwa ajili ya simu, hivyo ni rahisi zaidi kuwafikia wateja wengi wanaotumia simu.
- Instagram imeanzisha mfumo wa 'Checkout' unaowezesha kulipia bidhaa au huduma moja kwa moja kutoka katika akaunti yako ya Instagram, mfumo ambao unarahisisha sana biashara mtandaoni bila kulazimika kwenda kwenye tovuti kwa ajili ya kufanya malipo.
Hasara za kutumia mtandao wa Instagram kibiashara
- Takwimu za mtandao wa Instagram zinaweza kupotosha. Idadi ya 'followers' inaweza kuwa kubwa lakini wasiwe na mwingiliano wa kutosha na bidhaa au huduma yako.
- Inahitaji kuwekeza nguvu na ubunifu mkubwa katika kuchapisha mara kwa mara
- Instagram hairuhusu kuweka kiungo (link) katika chapisho lako, hivyo utalazimika kuwek kiungo katika 'bio.' Kiungo katika chapisho kitakuwepo tu pale chapisho lako litakapokuwa limelipiwa (Ad).
3. Twitter
Mtandao wa Twitter ni moja ya njia nzuri ya kutangaza biashara yako. Twitter inazuia idadi ya maneno katika chapisho, hivyo kumfanya mtumiaji kuwa mbunifu kwa kutafuta maneno machache kuielezea biashara yake bila kuwa na 'kelele' nyingi. Hata hivyo, Twitter inakuwezesha kutengeneza 'uzi,' njia ambayo inakuwezesha kuongeza chapisho chini ya jingine, hivyo msomaji huweza kufuatilia mwendelezo wa chapisho. Hata hivyo, Twitter ni nzuri zaidi kwa ajili ya kuwafanya wateja wako kuwa na ufahamu au uelewa kuhusu bidhaa yako, hasa kwa kuwatumia watu wenye ushawishi katika mtandao huo (influencers).
Faida za kutumia mtandao wa Twitter kibiashara
- Matangazo ya Twitter huwafikia wateja wengi zaidi kwa asilimia 3 ukilinganisha na mtandao wa Facebook.
- Twitter inakupa urahisi wa kuwafikia wateja wengi zaidi kwa kuwatumia watu wenye ushawishi katika mtandao wa Twitter (influencers).
- Unaweza kuwafikia walengwa kwa kutumia hashtags '#' na tagging '@'
Hasara za kutumia mtandao wa Twitter kibiashara
- Mtandao wa Twitter unapokea maudhui mengi, hivyo ni rahisi kwa maudhui ya biashara yako kutoonekana kwa urahisi ikiwa hautatumia njia ya ubunifu kuwasilisha maudhui yako
- Inahitaji kuchapisha walau maudhui kadhaa kwa siku
- Twitter inaweza kukusaidia kupata idadi kubwa ya watu wanaotembelea tovuti yako, lakini si mara zote wateja hao wakanunua bidhaa au huduma waliyoiona katika mtandao wa Twitter.
4. YouTube
Mtandao wa YouTube umetengenezwa kwa ajili ya video, ukiwa na watumiaji hai zaidi ya bilioni 2 kwa mwezi. Kwa sasa YouTube si sehemu ambayo watu huenda kutafuta burudani pekee, bali ni sehemu ambayo watu huenda kujifunza vitu vipya, hivyo kuwekeza katika kutangaza bidhaa au huduma yako ni njia nzuri ya kuwafanya watu wajifunze kuhusu bidhaa au huduma yako.
Unaweza kutumia mtandao wa YouTube kuielezea bidhaa yako kwa namna ambayo itamfanya mtazamaji kuvutiwa na kuendelea kuitazama video tofauti na kutumia maandishi mengi kuelezea jambo hilohilo. Matangazo ya YouTube yamerahisishwa sana, ambapo, tofauti na siku za nyuma, sasa unaweza kutumia matangazo yanayopotea ndani ya sekunde kadhaa yenye kiunganishi kinachoweza kumwelekeza mtu katika tovuti yako.
Faida za kutumia YouTube kibiashara
- Matumizi ya video yanaongeza uelewa na kufanya urahisi wa kuanzisha mazungumzo
- Kutumia mtandao wa YouTube ni njia rahisi ya kuelezea bidhaa au huduma yako hivyo kumrahisishia mtumiaji maamuzi ya kununua bidhaa yako au kutumia huduma yako kwa kujiamini.
Hasara za kutumia YouTube kibiashara
- Kutengeneza video kunaweza kuhitaji gharama kubwa ya uwekezaji wa fedha, muda na ujuzi
- Watazamaji hutegemea video yenye viwango vizuri vya mwonekano na sauti
5. LinkedIn
Mtandao wa LinkedIn sio maarufu kwa watu wengi, hasa kutokana na kuwa lengo la kuanzishwa kwake ni kwaajili ya mawasiliano baina ya wasomi/wafanyakazi* kwa ajili ya kutafuta kazi, lakini LikedIn kwa sasa imepata umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kutumika kuandaa machapisho kwa mfumo mzuri wenye mahitaji yote ya msingi ya uandishi wa blogu.
Unapaswa kufahamu kuwa watu wengi hawataingia katika mtandao wa LinkedIn kununua bidhaa au huduma yako, ila wanaweza kuangalia ushauri wa kitaalamu kuhusu biashara au huduma uliyoichapisha katika mtandao huo.
Faida za kutumia mtandao wa LinkedIn kibiashara
- Mtandao wa LinkedIn unafaa kutangaza maudhui yenye uhusiano na biashara au huduma unayoitoa ambayo unaweza kuyaelezea kwa undani kutokana na uelewa wa watumiaji wa mtandao huo.
- LinkedIn pia ni sehemu nzuri ya kuungana na kufahamiana na watu wenye utaalamu unaofanana kuhusu biashara au huduma unayoitoa
- Ni sehemu nzuri kwa ajili ya kuajiri watu wenye uzoefu kuhusu biashara au huduma unayoitoa
Hasara za kutumia mtandao wa LinkedIn kibiashara
- Mtandao wa LinkedIn haujatengenezwa kwa ajili ya biashara mtandaoni
- Watumiaji wa mtandao wa LinkedIn wamegawanyika katika makundi ya wasomi/wataalamu, hivyo kuwanyima nafasi makundi mengine kutoa mawazo yao kwa uhuru.
Upi ni mtandao mzuri zaidi wa kijamii kwa ajili ya kutangaza biashara au huduma yako?
Hakuna jibu moja kwa swali hili. Hakuna mtandao mmoja wa kijamii unaoweza kutosheleza mahitaji yako yote. Uchaguzi wa mtandao sahihi wa kijamii utakaoweza kuutimia kwa ajili ya kutanagaza biashara yako mtandaoni itategemea na wateja wa bidhaa au huduma yako, aina ya biashara yako na mipango yako ya matangazo ya biashara yako, ikiwamo bajeti na mbinu za kutangaza biashara yako.
Kuwa na akaunti katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya biashara yako ni suala la lazima ikiwa unataka kutangaza biashara yako mtandaoni. Ni muhimu kufahamu kuwa akaunti ya biashara inapaswa kuwa ya kujitegemea, na si akaunti yako binafsi. Ni muhimu kuwa na akaunti katika mitandao tofauti, badala ya kutegemea mtandao mmoja tu, kwa lengo la kuwafikia wateja wenye chaguzi tofauti za mitandao ya kijamii. Kwa ajili ya kujenga picha nzuri ya taasisi au kampuni yako ya biashara, ni muhimu kutumia mtandao wa LinkedIn.
Jambo la muhimu zaidi ni kutumia ubunifu katika kutangaza biashara yako katika mitandao ya kijamii. Kumbuka, mitandao ya kijamii imetengenezwa kwa ajili ya kuwakutanisha watu, na matangazo ya kibiashara huonekana kero kwa watu wengi. Ubunifu wa matangazo yako ndio utakaomfaya mtumiaji kuangalia tangazo lako.
Katika sehemu ya tatu ya makala haya, tutaangalia mambo ya kuzingatia ili kutengeneza machapisho kwa namna ya kuvutia na kumfanya mtumiaji kuacha kile alichokuwa akikifanya na kwenda kutazama bidhaa au huduma yako unayoitangaza.
Unaweza pia kusoma: Kwanini Unahitaji Mitandao ya Kijamii katika biashara yako?
Upvote
3