Mamlaka Tanzania zaifungia Mwananchi kuchapisha habari mtandaoni kwa 'ukiukaji wa kanuni'
Chanzo cha picha,MCL
Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) imesitisha kwa muda huduma za maudhui ya mtandaoni za Mwananchi Communication Limited (ML) kwa 'ukiukaji wa kanuni'
Katika tangazo lake kwa umma TCRA imesema imesitisha leseni ya huduma za maudhui ya mtandaoni dhidi ya kampuni ya habari ya MCL nchini humo, kwa ukiukaji wa kanuni ya mwaka 2020.
TCRA imesema tarehe 01 Oktoba 2024, MCL ilichapisha maudhui mjongeo na sauti (audio-visual kwenye mitandao yake ya kijami, maudhui yaliyozuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020.
''Maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa taifa’’, imeeleza taarifa ya TCRA , iliyotumwa kwenye mitandao yake ya kijamii:
''Umma unaarifiwa kuwa, kufuatia kuchapishwa kwa maudhui yaliyokatazwa na yanayopingana na sheria, TCRA imesitisha kwa muda leseni za huduma za maudhui mtandano za Mwananchi Communication Limited (The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na Mwanaspoti) tangu tarehe ya kutolewa taarifa hii, wakati masuala mengine ya kiusimamizi yanafanyiwa kazi,’’ limehitimisha tangazo hilo.
Mwananchi Communication Limited imesemaje?
Kufuatia kuondolewa kwa leseni hiyo, MCL imetangaza kuondoa maudhui yake ya michoro kwenye mitandao yake ya kijami.
Kupitia gazeti lake la lugha ta Kiingereza The Citizen, kampuni hiyo imesema: ‘’Tumeamua kuondoa michoro iliyoshirikishwa Oktoba 1, 2024 kwenye mitandao ya kijamii (X na Instagram), kwa kuwa ilionyesha matukio yaliyoibua hofu kuhusu usalama wa watu binafsi nchini Tanzania.’’
''Uamuzi wetu wa kuondoa katuni unatokana na kusababisha tafsiri mbaya ambayo ni kinyume na nia yetu’’, taarifa hiyo iliongeza.
Maudhui yaliyoiweka MCL lawamani ni ya katuni ambayo ilikuwa ikionesha raia wa nchi hiyo wakilalama kwenye runinga juu ya matukio ya watu kutekwa na kuuawa nchini humo. Katuni hiyo ilikuwa ikimuonesha mtu ambaye alikuwa akitizama runinga ambaye wengi wametafsiri kuwa ni Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.
Matukio ya watu kutekwa, kupotezwa na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha yamezua gumzo katika miezi ya hivi karibuni nchini Tanzania.
Chanzo.BBC