Maneno ni mtaji

Maneno ni mtaji

GoldDhahabu

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2023
Posts
7,189
Reaction score
10,375
Katika moja ya tafiti zilizofanyika nchini Marekani, ilibainika kuwa mafanikio ya mtu kikazi yanategemea:
1. Ufanisi katika taaluma aliyo nayo asilimia 15

2. Ufundi wa kuzungumza asilimia themanini na tano.

Hii inamaanisha, mtu mwenye ufaulu wa "first class" lakini si fundi wa kuongea anaweza kuongozwa kazini na mtu mwenye ufaulu wa mwisho kabisa lakini mwenye kujua jinsi ya kutumia ulimi wake.

Anayebisha, akaulizie Elimu ya Joseph Kasheku Msukuma. Ni darasa la saba lakini anashikilia nafasi inayotamaniwa na maprofesa.

Hata Dr. Jakaya Mrisho Kikwete hakuwa "mkali" sana darasani(Chuo Kikuu). Kufanikiwa kwake kuwa Rais wa Tanzania kulichangiwa kwa sehemu kubwa na uwezo wake wa kuongea kwa ufundi.

Maneno huweza kubadilisha mitazamo ya watu, wakakupenda au wakakuchukia.

Maneno huweza kusababisha huzuni kwa watu waliokuwa na furaha wakawa na huzuni, au watu walio katika majonzi wakasahau majonzi yao.

Najua ninachokisema. Nilishaona si mara moja wala mara mbili! Nilishafanya hayo si mara moja wala mbili. Nilishasoma hayo kwenye vitabu mbalimbali si mara moja wala mbili. Maneno!!! Maneno hubadili mambo na vitu!

1. Wakati tulipokuwa "wavulana", mmoja wa rafiki zangu alimtembelea ndugu yake aliyekuwa amelazwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa. Aliingia na baiskeli mpaka ndani ya uzio wa hospitali kinyume na "Sheria" ya mahali husika.

Kwa utaratibu wa mahali hapo kipindi hicho, baiskeli zilizokuwa zikiingizwa ndani ya uzio zilikuwa zikikamatwa na kutaifishwa.

Alipotoka wodini kumwona nduguye, akamkuta tayari mlinzi ameshaiona baiskeli yake na kuitia "nguvuni".

Huyo kijana alijua mlinzi alimaanisha nini, na alijua si utani. Na, alipobaini kuwa huyo mlinzi ni wa kabila moja na yeye, alimwambia kikwao(kilugha), "Baba, mimi ni mzaliwa wako wa kwanza. Naomba unisamehe".

Huyo kijana alisema hivyo akimaanisha kuwa huyo mlinzi anaweza kuwa rika moja na baba yake, na kwa kuwa yeye alikuwa wa kwanza kwa babaye, alimchukualia huyo mlinzi kama baba yake.

Ingawa huyo mlinzi hakuwa akimfahamu huyo kijana, lakini alipoangalia kulia na kushoto na kujiridhisha kuwa hakukuweko na mtu aliyemwona, alimwambia huyo kijana aichukue baiskeli yake na kuondoka kwa haraka sana.

Kwa nini huyo mlinzi aliamua kukiuka utaratibu wa kazi yake kwa kumsaidia mtu asiyemfahamu?

Ni kwa sababu ya maneno! Huyo kijana alivyotamka vile, huyo baba alimwona mwanawe wa kwanza kwenye fikra zake, na kujihoji kama ingelikuwa ni mwanawe "Dogo Janja" ndiye aliyefanya hilo kosa angemfanyeje?

Jibu alilolipata ndilo lililomfanya aichukue hayo maamuzi ya haraka.

2. Kijana mmoja wa Sekondari alifanya kosa lililopelekea walimu wake wafikilie uamuzi kuwa adhabu pekee inayomstahili ni kufukuzwa shule.

Ripoti ilipomfikia mkuu wa Shule, aliridhia uamuzi wa walimu, na hivyo akaagiza huyo mwanafunzi aitwe ofisini kwake kwa ajili ya kuagwa rasmi. Ilikuwa ni shule ya "boarding".

Akiwa anajua anachoenda kukutana nacho, huyo mwanafunzi aliitikia wito wa mkuu wa shule akiwa amejihami na kauli ambayo ndiyo ilikuwa silaha yake ya mwisho, ingawa Kamati ya walimu ilishatoa hukumu kuwa adhabu pekee anayostahili ni kufukuzwa.

Alipofika ofisini kwa mkuu wa shule, na kufahamu kuwa anatakiwa kuondoka shuleni hapo, alimwambia hivi mkuu wa shule: "Baba, mimi ni mwanao wa mwisho. Sina pa kwenda! Naomba unipe nafasi ya mwisho".
Aliyasema hayo kisha akaanza kueleza jinsi familia yao ilivyo masikini na changamoto zinaziokabili familia yao.

Kwa jinsi alivyojieleza, hata kama una moyo mgumu kama jiwe, utamhurumia tu.

Mkuu wa shule aliamua kubadilisha maamuzi, na kumkabidhi kwa mmoja wa walimu ili afanyiwe "counseling" na kufuatiliwa kuona mabadiliko yake

Na kweli, alibadikiko na kuwa "good boy", mpaka akaanza kupewa "vyeo" shuleni. Aliyekuwa afukuzwe, akaishia kuwa mwanafunzi pendwa anayeaminiwa na walimu wake.

3. Kipindi fulani, nilimtembelea mama mmoja aliyekuwa amefiwa na pacha wake. Sikuwa nimewasiliana naye tokea msiba utokee, japo miezi kadhaa ilikuwa imeshapita tokea nduguye afariki.

Nilipomjulisha kuwa nilienda kumpa pole, alijikuta anaanza kulia tena. Kauli yangu ilimkumbusha "msiba" aliyokuwa ameshausahau. Ilibdi nitafute jinsi ya kumhamisha kwenye hiyo hali.

Kwa kuwa ni Mkristo, aliamini kuwa nduguye yupo Mbinguni, mahali ambapo ndiyo hatma ya Wakristo.

Kwa lengo la kumhamisha kutoka kwenye majonzi, nilimwuliza maswali kadhaa.

Kwanza, nilimwuliza mahali ndugu yake alipo kwa wakati huo, na akaniambia anaamini kwa asilimia zote kuwa yupo Mbinguni.

Nikamwuliza tena, kati ya Mbinguni na duniani ni wapi kuzuri, akajibu ni Mbinguni.

Swali lililofuatia ni kuwa yeye akifa anatarajia kwenda wapi, akanijibu
Mbinguni.

Aliponiambia hivyo, nilimwuliza, "Kwa hiyo unamwonea ndugu yako wivu?"

Hiyo kauli ilimfanya acheke, na kubaini kuwa alikuwa analizwa na ubinafsi. Hakuwa na sababu za kumlilia mtu aliyepo mahali pazuri ambako naye anatamani siku moja aende.

Tokea hapo, tuliongea kwa uhuru kabisa, wala hakuwa na majonzi tena.

4. Miaka ya nyuma, kijana mmoja alinifuata na kunijulisha kuwa matokea ya kidato cha Sita yametoka na amefeli. Wakati alipotamka tu kuwa kafeli, akaangua kilimo.

Nilitulia kwa muda nikamwacha alie kwanza. Alipotulia, nilimwuliza, "umefeli au hujafikia lengo?"

Kabla ya matokeo kutoka, kwa sababu ni miongoni mwa vijana waliokuwa karibu nami, nilimjulisha kuwa maishani, kuna utofauti wa kufeli na kutokufukia lengo. Kupata "zero" kwenye mitihani si kufeli. Ni kutokufukia lengo. Ni pale tu unapokubali kuwa umeshindwa na hivyo huna sababu ya kujaribu tena ndipo unapokuwa umefeli. Kwa hiyo hapaswi kupokea hata hukumu ya Baraza la Mitihani kuwa kafeli ikiwa yeye hajajiweka kwenye kundi la waliofeli.

Nilipomwuliza kama kafeli au hajafikia lengo, alivuta pumzi na kusema hajafikia lengo. Pamoja na kuwa alipata "division zero", lakini aliweza kuiweka hiyo hali katika tafsiri chanya kuwa huko si kufeli, bali ni kutokufukia lengo.

Nilikuwa nafahamiana na wazazi wake, kwa hiyo aliponiambia kuwa lengo lake ni kujiendeleza hadi Chuo Kikuu, nilienda kuzungumza na baba yake na kumwambia kama anaweza kumsaidia , afanye hivyo kwa sababu kufeli kwake si uzembe, ni "bahati mbaya" tu. Nilikuwa namfahamu. Alikuwa na jitihada sana katika kujisomea.

Nilupomjulisha baba yake hilo, yeye naye aliniunga mkono kuwa hata yeye anaamini mwanye amefeli kwa bahati mbaya. Alikuwa akimwona jinsi alivyokuwa akijisomea akiwa likizo, mara nyingi alikuwa akisoma mpaka Usiku wa manane. Alikuwa tofauti na ndugu zake wengine. Hakuwa na "time" na TV. Yeye alikuwa ni wa kusoma sana hata wenzake walipokuwa wakijiburudisha kwa TV.

Kwa kuwa huyo kijana hakuwa amefeli bali alikuwa hajafikia lengo, alijipanga upya, akajiendeleza kwa kutumia matokea ya"form four" kwa sababu ya "form six" yasingemsaidia chochote kwa kuwa alipata daraja sifuri, mpaka hatimaye akafika Chuo Kikuu, na sasa ana kazi yake "nzuri".

5. Dr. Napoleon Hill, kwenye kitabu chake cha "The Laws Of Success", anaeleza jinsi maneno ya mlinzi "yalivyomvunjavunja" hadi akawa mpole. Mlinzi hakuwa msomi kama yeye, nafikiri, hakuwa akijua hata kusoma na kuandika.

Anaeleza kuwa siku hiyo, alikuwa ofisini kwake kwenye jengo kuliko na ofisi yake, majira ya Jioni kuelekea Usiku akiandika.

Wakati akiendelea na zoezi hilo, alishtukiz
ia taa imezimwa, akalzimika kushuka ghorofani hadi penye swichi kuiwasha. Inaelekea kipindi hicho, swichi zilikuwa zinakaa sehemu moja, pengine. Pamoja na kuiwasha, alimwambia mlinzi asizime taa kwa sababu bado yupo ofisini.

Haukupita muda mrefu baada ya taa kuwashwa, ilizimwa tena. Alishuka na kuiwasha.

Baada ya muda kupita, hilo lilijirudia kwa mara nyingine. Safari hii, kabla ya kuiwasha taa, alimfuata mlinzi na kumzaba vibao.

Katika hali ya kushangaza, mlinzi, huku akionekana kuwa na utulivu kana kwamba hakuna kilichotokea" alimwambia, "lakini leo Asubuhi tuliongea vizuri sana".

Kauli hiyo ilimfanya Napoleon Hill aone aibu na hivyo kurudi ofisini kwake haraka sana. Hakuweza kuendelea kuandika, alikaa akitafakari alichokifanya na jinsi mlinzi "alivyorespond". Maneno ya mlinzi yalimwumiza kuliko makofi yake yalivyomuumiza mlinzi. Maneno yanaumiza kuliko ngumi ya Mandonga Mtu Kazi.

Napoleon aligundua kuwa katika suala la "self control", mlinzi kamzidi mbali sana. Yeye alimwadhibi kwa makofi, lakini mlinzi akampiga kwa maneno, na akashinda.

Taratiibu, na katika hali ya unyonge, alishuka hadi chini na kumwita mlinzi na kumwomba msamaha kwa kile alichokifanya.

Mlinzi alimjibu kuwa asiogope kwa sababu mud huo wako wawili tu, hakuna mtu aliyewaona, na yeye hatasema kwa mtu yeyote.

Hiyo kauli "ilimmaliza" kabisa na kuanzia siku hiyo, aliamua kutokukubali kutawaliwa na hisia/hasira.

Mlinzi asiyejua kusoma wala kuandika alimfundisha somo kubwa kwa vitendo.

Mifano ni mingi inayoonesha kuwa kwa maneno sahihi, unaweza kubadilisha hali ya mambo na ya watu.

Unaweza kutumia maneno sahihi ukawasiaida wengine!

Unaweza kutumia maneno sahihi kwa manufaa yako binafsi na yakakufikisha mbali.

Maneno ni rasilimali muhimu, na kila mtu anayo.

Tunatofatiana tu jinsi tunavyoyatumia.
 
Nakubaliana nawe asilimia zote, maana hapa ofisini Kuna kiumbe anajua kuongea Kuliko hata kufanya kazi, Na boss anamkubali Zaidi yeye Kuliko wanaojituma Na kazi:
 
Hongera kwa andiko lenye kujenga.
 
Japo sipendagi nyuzi zenye episode ila huu ningetamani uweke episodes kwakweli maana mrefu sana
 
Tafuta elaa usije kuwa chawa.........
Daimond vs babalevo
Alikiba vs mwijaku
Gsm vs manara
Samia vs chawa wa mama
Watu wakimyaaa ndo wananafasi kubwa sana ya kuwin mambo yao........
 
Back
Top Bottom