Kuna vijana naamini wamehamasika kutafiti na kuandika upya historia ya uhuru wa Tanganyika na kwa kweli nawapongeza na nawatakia kila la kheri katika juhudi zao hizi.
Nimesoma makala moja ya Mangi Chief Thomas Marealle kwa bahati mbaya nimekuta kuna baadhi ya mambo mwandishi hakuyafanyaia utafiti wa kina.
Nimemwandikia baadhi ya mambo kama njia ya kumgutua na kumtia moyo:
''...katika hili bandiko la Chief Marealle kuna mambo unahitaji kuyapitia upya ili ipatikane ithibati ya ulichoandika.
Nimebahatika kumsoma Chief Marealle katika Nyaraka za Sykes barua binafsi ambazo akiandikiana na Ally Sykes.
Kwa ajili hii basi nimeweza kufahamu hata kile alichokuwa anakiamini ndani ya nafsi yake katika uongozi wa harakati za kudai uhuru.
Kuna barua moja Chief Marealle alikuwa anamuonya Ally Sykes kumtahadharisha na hali ya baadae baada ya uhuru.
Marealle alifika UNO lakini hakuwa mjumbe aliyetumwa kuwawakilisha Watanganyika.
Kuna jina moja umealiandika la mwanasheria kutoka Bermuda "Earl Seymour," naamini ulimkusudia Earle Seaton.
Earle Seaton pia nimekutananae ndani ya Nyaraka za Sykes akiwa mshauri wa TAA kuhusu "mandate territories."
Earle Seaton ana historia ya kutukuka katika harakati za uhuru wa Tanganyika hasa kwa TAA.
Abdul Sykes katika taatifa yake ya mwaka wa 1950 akiwa Katibu wa TAA kamtaja Seaton kama mtu aliyetoa msaada mkubwa kwa Constitutional Development Committee.
Abdul Sykes, Earle Seaton kama mwanasheria na Japhet Kirilo akiwa kiongozi wa Meru Citizens Union walifanya kazi pamoja kufikisha tatizo la Ardhi ya Wameru UNO 1952 na Kirilo akazungumza UNO Seaton akiwa mkalimani wake.
Yapo mengi.
Hotuba ya Mwalimu Nyerere UNO 1955 inatokana na waraka wa TAA Political Subcommittee ambao ndani ya waraka huu kuna mchango mkubwa wa Seaton.
Waraka huu ulijadiliwa mwaka wa 1954 katika kuasisi TANU na ni mapendekezo yaliyowasilishwa na TAA Political Subcommittee kwa Gavana Edward Francis Twining mwaka wa 1950.
Ningependa kukufahamisha pia kuwa Chief Marealle na Abdul Sykes walikuwa marafiki wakubwa.
Abdul akimtania Marealle akimwita, "King Tom," akimwambia Waingereza wanakataa kumwita yeye King ili asifanane na mfalme wao King George.
Mwaka wa 1951 Chief Marealle alichaguliwa kuwa Rais wa Tanganyika African Government Servant Association (TAGSA) Ally Sykes akiwa Katibu na Rashid Kawawa, Dr. Wilbard Mwanjisi, Michael Lugazia, Steven Mhando wakiwa katika Kamati.
Yapo mengi ningeweza kukueleza lakini nakuomba pitia upya historia ya Chief Marealle.''
View attachment 1245766
Earle Seaton na Julius Nyerere