BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Maofisa BoT kutaja vigogo
Mwandishi Wetu Septemba 3, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
Ni walioshinikiza kupitishwa kwa nyaraka feki
MAOFISA wa Benki Kuu (BoT) ambao wanatajwa kuhusika katika mchakato wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika benki hiyo, sasa wanaelezwa kujiandaa kupasua bomu kwa kuwataja vigogo halisi waliohusika na wizi huo.
Habari zinaeleza kwamba, baada ya mchakato wa kuwachukulia hatua za kisheria kuanza, maofisa hao wakiungwa mkono na watumishi wengi wa BoT, wametishia kumwaga hadharani yote wanayoyafahamu kuhusu wizi huo ulioligharimu taifa Sh bilioni 133.
"Wamesema wao walijua kuwa iko siku watatolewa kafara, hivyo walikusanya ushahidi wote na walikuwa makini katika kupitisha kila dokezo lililohusu upitishaji wa fedha hizo na sehemu zote walitekeleza maelekezo ya mkubwa wao wa kazi na kwa kupitia idara ya sheria ya BoT," anasema ofisa mmoja wa BoT aliye karibu na maofisa hao.
Akitoa mfano wa nyaraka zote zilizopitisha takriban shilingi bilioni 40 zilizochotwa na kampuni moja tu ya Kagoda Agricultural Limited, maofisa hao walitaka uhakiki wa wanasheria wa BoT, kabla ya kutaka tena baraka za aliyekuwa Gavana, Dk. Daudi Ballali, ambaye naye anaelezwa kufanya hivyo kwa maelekezo ama shinikizo kutoka kwa wanasiasa.
RAIA MWEMA imeona baadhi ya nyaraka hizo za mawasiliano ambazo moja kwa moja zinaonyesha jinsi maofisa hao walivyotaka ushauri kwa wanasheria na idhini ya Gavana kabla ya wao kutoa maelekezo kwa watekelezaji wengine.
Mfano katika moja ya nyaraka za kupitisha malipo ya Kagoda Agricultural Limited za mtajwa mmoja, Imani Mwakosya, ambaye alikuwa akikaimu kitengo cha mikopo, alimtaka mkuu wa idara ya sheria kuhakiki kwanza nyaraka za idhini ya kununua deni (Deed of Assigment) za kampuni hiyo kabla ya kuendelea na mchakato wa malipo na kabla ya kuwasilisha kwa Gavana kwa uidhinishaji.
"Tafadhali thibitisha uhalali wa nyaraka husika kabla ya kupeleka maombi haya kwa Gavana kwa uhakiki wake na uidhinishaji," anaeleza Mwakosya katika dokezo lake la Oktoba 21, 2005 kwa Katibu wa Bodi ambaye naye siku hiyo hiyo aliandika kwa kusema;
"Ninathibitisha kwamba nyaraka zilizoambataniswa ni halali na zinakidhi matakwa ya kisheria. Nyaraka hizi zinaweza kutumika na BoT kuidhinisha malipo husika."
Baada ya mwanasheria kuandika dokezo hilo, siku hiyo hiyo (Oktoba 21, 2005) Mkurugenzi wa Fedha za Nje, alimuandikia Gavana kwa ufupi akisema, "ukiamua unaweza kuidhinisha malipo haya," na Gavana Ballali siku tatu baadaye kuidhinisha kwa neno moja tu, "approved" (imepitishwa).
Habari za awali kutoka kwa BoT zinaeleza kwamba, dokezo hilo lilichelewa kwa siku tatu kutoka Oktoba 21, 2005 hadi Oktoba 24, 2005 kwa Gavana Daudi Ballali (Marehemu) kutokana na kusita kwake kupitisha malipo hayo hadi alipokutana na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, akiwa na mwanasiasa mmoja na Ofisa Mwandamizi wa Serikali na kuagizwa kuidhinisha.
"Hata Mkurugenzi wetu (wa Fedha za Nje) alisita na alimwelezea Gavana wasiwasi wake kuhusu malipo hayo na ndio maana katika dokezo lake alimwambia wazi mkubwa wake kwamba kama akiamua anaweza kuidhinisha badala ya kumwambia ni halali idhinisha," kinaeleza chanzo chetu ndani ya BoT.
RAIA MWEMA limeona dokezo ambalo Mkurugenzi wa Fedha za Nje alilofikia hatua hata ya kuandika neno, ‘what is this?' (nini hichi?) akihoji maelezo kutoka kwa maofisa wa chini yake kuhusiana na malipo ya Kagoda Agricultural ambayo yalikosewa kwa kuandikwa wakaandika Euros badala ya fedha za Ujerumani (Deutch Marks) ambazo ndizo zilizopo katika nyaraka za madai.
Makosa hayo yalihojiwa pia na wakaguzi wa kampuni ya Ernst &Young ambao walishangazwa mno na jinsi mabadiliko hayo yalivyofanyika kwa haraka kwa wakurugenzi wanaoishi Ujerumani kuwasiliana kwa siku chache na wenzao wa Tanzania na kurekebisha makosa hayo na baadaye kurudisha nchini nyaraka husika. Makosa hayo yalisaidia kugundulika kuwa zilikua nyaraka za kughushi.
Pamoja na taarifa za wanaochukuliwa hatua kuelezwa kuwagusa maofisa wasiozidi watano, habari za ndani ya BoT zinaeleza kwamba wanaotajwa kuhusika katika mchakato huo ni wengi zaidi na ambao waliorodheshwa moja kwa moja katika ripoti ya wakaguzi iliyowasilishwa serikalini.
Wanaotajwa kwa nyadhifa zao baada ya Gavana aliyevuliwa madaraka na Rais ni Mkurugenzi wa Fedha na Katibu wa Bodi ambao walikuwa maofisa wawili walioshika nafasi hiyo katika kipindi ambacho fedha za EPA zilichotwa kutoka BoT (2005/2006) akiwamo mmoja aliyekaimu nafasi hiyo.
Wengine wanaotajwa ni maofisa wawili waliongoza kitengo cha sera katika kipindi cha 2005/2006; Naibu Mkurugenzi Idara ya Madeni ambao nao wanatajwa kuwa wawili katika kipindi hicho; Mkuu wa kitengo cha madeni makubwa na ya kibiashara; Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mabenki aliyekuwapo.
Maofisa wanaoonekana katika nyaraka nyingi za EPA ni pamoja na Imani Mwakosya, Esther Komu, Kimela, A.A.Chaula na M. Nderimo ambao kwa kiasi kikubwa wanaelezwa na maofisa wa BoT kwamba walifanya kazi kwa shinikizo kutoka kwa wakubwa zao akiwamo Marehemu Ballali ambaye naye alishinikizwa na viongozi wa juu na wanasiasa.
Wiki hii imeripotiwa kwamba maofisa wanne kati ya watano waliosimamishwa kazi BoT wamefukuzwa kwa madai kwamba walizembea kuzuia upotevu huo mkubwa unaoendelea kuizonga serikali ya Rais Kikwete.
Taarifa za kufukuzwa kwa maofisa hao ndio imeibua sasa hoja ya kutaka kuwataja wahusika wote waliohusika na walioshinikiza kuchotwa kwa fedha za EPA na kwamba sasa wameelezwa kutumia hata vyombo vya sheria kutimiza azma yao hiyo.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba suala la wafanyakazi hao linashughulikiwa kwa kuzingatia mfumo wa kiutawala na kwa uangalifu zaidi kuepuka athari za kisheria kwa serikali na benki.
Hatua ya kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wafanyakazi hao, ilikuwa miongoni mwa hatua zilizoanishwa na wakaguzi na kukubaliwa na Rais Kikwete ambaye naye aliagiza zitekelezwe na kusisitiza katika hotuba yake bungeni wiki iliyopita.
Katika hotuba yake kwa Bunge, Rais Kikwete alisema alikwisha kuiagiza Bodi ya Benki Kuu ichukue hatua za kinidhamu kwa maafisa wote wa Benki Kuu waliotuhumiwa na Mkaguzi ambao wapo chini ya Mamlaka ya Bodi.
Mbali ya kuchukuliwa hatua kwa maofisa hao, Bodi ya BoT ilivunjwa na wengine wapya wakateuliwa, lakini baadhi ya wajumbe walirejea katika nafasi zao kwa nyadhifa zao akiwamo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Katika hotuba yake Rais Kikwete alisema, "Naelewa hoja ya wajumbe wanaoingia kwenye Bodi kwa nyadhifa zao, kuendelea kuwa Wabunge hata pale Bodi inapovunjwa kwa mapungufu au wale Wajumbe wa Bodi waliopungukiwa sifa mnawaondoa kwa kuivunja lakini mmoja ambaye anaingia pale kwa wadhifa wake anaendelea kuwepo.
"Sasa hili tunalitafakari maana kama sheria imekwishamtaja atakuwepo fulani tutampeleka nani badala yake ukaonekana umetekeleza sheria, ni huyo huyo. Kwa hiyo, kama huridhiki nalo hilo fuata taratibu za utawala bora. Tusipokwenda na taratibu hizo nchi hii tutaingiza kwenye mess kubwa na wale wenye mamlaka kama mimi utakuwa unaonea watu kweli. Nikisema kwamba mkamateni fulani, atakamatwa tu."
Katika hotuba yake Rais Kikwete alisema uchunguzi kuhusu kampuni 13 yaliyochota Sh bilioni 90 umekamilika, wakati makampuni tisa yaliyochota shilingi bilioni 42, unalazimika kuhusisha washirika wa mataifa mengine ya nje na hivyo ametoa muda hadi Oktoba 31 kwa kamati aliyoiunda chini ya Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika kukamilisha kazi hiyo.
Rais alisema wamekamata mali za watuhumiwa wote na kwamba "wale watu ambao kwa kweli walikuwa wanaonekana ni matajiri sana wapo katika hali ngumu sana. Wenyewe wanajijua hali zao zilivyokuwa ngumu sana."
Alisema kwa sasa zimekusanywa shilingi 53,738,835,392/= na akaagiza fedha hizo kuingizwa katika mfuko maalumu kwa ajili ya kusaidia sekta ya kilimo zikichanganywa na nyingine zinazotarajiwa kufikia shilingi 64,844,770,688/= .
"Kamati imeomba idhini kuwa madeni hayo yanayoendelea kulipwa yaendelee kulipwa mpaka tarehe hiyo, maombi yao hayo nimeyakubali. Lakini tumekubaliana kwamba itakapofika tarehe 31 Oktoba,2008 mwisho ambaye hakulipa mpaka tarehe 1 Novemba, 2008 awe amefikishwa mahakamani ili Mahakama itusaidie kupata fedha za watu, hatuko tayari kulipa deni la marubeni India, Japan na mtu amekula hela yupo pale Dar es Salaam, hapana," alisema Kikwete.
Hata hivyo, kumekua na hoja kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo wananchi wa kawaida ambao wamesisitiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wote wanaohusika hata ikiwa watalipa fedha walizopata isivyo halali vinginevyo nchi itagawanyika kwa wenye fedha kutochukuliwa hatua za kisheria na walalahoi kujazana magerezani.
