Katika toleo letu la jana ukurasa wa mbele, tulichapisha habari yenye kichwa cha habari `Duh! Maumivu, hivi ndivyo mashangingi yanavyofilisi.' Habari hiyo ambayo chanzo chake ni uchunguzi wa gazeti hili, ilijikita zaidi kueleza jinsi utitiri wa magari ya kifahari aina ya VX-V8 na mengineyo ya aina hiyo maarufu kama mashangingi yanayotumiwa na viongozi waandamizi serikalini yanavyoligharimu taifa mabilioni ya fedha kila mwaka.
Habari hiyo imeeleza kwa kina bei ya shangingi moja pamoja huduma zake kwa ujumla na kubainisha kuwa ni mamilioni ya fedha hutumika kila mwaka ambazo kama viongozi wakiamua, zinaweza kuelekezwa kwenye maeneo mengine ya huduma za kijamii. Tanzania imebarikiwa kwa kuwa na rasilimali lukuki yakiwamo madini, ardhi, vivutio vya watalii na sasa imegundulika gesi mkoani Mtwara, kuzitaja kwa uchache.
Rasilimali hizi zikitumika kwa maslahi mapana ya taifa, Tanzania haipaswi kuitwa maskini! Haipaswi kuitwa hivyo kwa sababu ina kila nyenzo muhimu ya kuundoa umaskini isipokuwa tatizo liko kwa wachache wanaopewa dhamana ya kuzisimamia. Lakini kwa bahati mbaya, baadhi ya viongozi wenye dhamana hizo, badala ya kuweka maslahi ya Taifa mbele, hutanguliza ubinafsi.
Tumeshuhudia baadhi ya viongozi baada ya muda mfupi wakishakabidhiwa madaraka hubadilika haraka kimaisha. Utakuta mahekalu yanasimamishwa mithili ya uyoga maeneo mbalimbali ya miji kama Masaki, Oysterbay, Mikocheni, Mbezi Beach na mengine kama hayo katika miji mingine maarufu hapa nchini.
Wengi wamegeuza utumishi wa umma kama `ulaji' na matanuzi tena bila kuwafikiria hata wananchi wanaowaongoza. Tunajiuliza kwa mfano, hivi gari inayomfaa waziri, naibu wake, wakurugenzi na vigogo wengine wa serikali, ni mashangingi tu? Inasikitisha kuona nchi kama Tanzania ambayo kila uchao tunaimba kuwa ni maskini, viongozi wake wanatanua kwa magari ya kifahari na kuendelea kuwaumiza walipa kodi ambao baadhi yao hushindia mlo mmoja kwa siku.
Shukrani za pekee zimwendee Rais Dk. John Magufuli, kwa hatua ambazo ameanza kuzichukua katika kukabiliana na hali hiyo.
Mara baada ya kuanza kazi mapema mwezi uliopita, Rais Dk. Magufuli amechukua katua kadhaa za kubana matumizi yasiyo na tija. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kuzuia sherehe za wabunge kupongezana, iliyowezesha kuokoa zaidi ya Sh. milioni 200 zikanunua magodoro na vitanda 300 Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Vile vile, Rais Dk. Magufuli amepiga marufuku sherehe ya Siku ya Uhuru iliyokuwa ifanyike Desemba 9, mwaka huu na kuwezesha kupatikana kwa fedha za upanuzi wa barabara ya Morocco na Mwenge, Dar es Salaam. Aidha, amezuia maadhimisho ya Siku Ukimwi Duniani, yaliyokuwa yafanyike kitaifa mkoani Singida Desemba Mosi na kuagiza fedha za shughuli hiyo zitununue dawa za waathirika wa ukimwi.
Hayo yote yamefanyika katika kipindi kifupi kisichozidi mwezi mmoja tangu aingie madarakani. Tumejifunza kitu kikubwa kwamba, kumbe inawezekana isipokuwa kinachokosekana miongoni mwa watendaji wa serikali ni dhamira ya dhati ya kulijenga taifa.
Tungewaomba viongozi wetu serikalini, sasa muachane na kasumba ya kutaka kutumia magari ya kifahari na matumizi yasiyo na tija ili taifa hili liwe la asali na maziwa kwa wote.
Mungu Ibariki Tanzania.
Source: Nipashe