Serikali ya Tanzania inaweza kuongeza kipato kutoka kwenye mitandao ya kijamii ikiwa tu itaanzisha utaratibu wa kuwakata kodi watumiaji wote wa mitandao hiyo kila siku. Inaaminika hapa Tanzania kuna watumiaji wa mitandao ya kijamii milioni 14 kwa siku(14,000,000), hizi takwimu sio, rasmi lakini ikiwa zitafanyika takwimu rasmi idadi hii inaweza kuwa kubwa zaidi.
Ikiwa Serikali yako itaamua kuanza kukata kodi ya sh. 200 tu kwa kila mtumiaji wa mitandao ya kijamii kwa siku, TRA itakusanya sh. 84,000,000,000 (Bilioni 84) kwa mwezi, na kwa mwaka itakuwa sh. 1008,000,000,000 (Trilioni 1 na bilioni 1). Hii ni pesa mingi sana ambayo kama ikikusanywa itaweza kuisaidia Serikali katika kupata pesa za kujenga nyumba za waalimu nchi nzima. Kwa mahesabu haya ya haraka haraka, utaona kuwa hii mitandao ya kijamii ni "migodi" iliyolala.
Mfano ikiwa kila nyumba moja itajengwa kwa sh. 50,000,000 (Milioni 50) basi kwa mwaka zitajengwa nyumba 20,160 nchi nzima na baada ya miaka 5 zitakuwa zimejengwa nyumba 100,800 na hapa tutakuwa tumeondoa tatizo la nyumba sio tu kwa waalimu, bali pia kwa askari polisi, askari magareza, madaktari na wanajeshi wetu. Tena tenda hii ya ujenzi wa nyumba hizi wapewe wanajeshi kama walivyopewa ile tenda ya kujenga ukuta wa Mererani. Na uzuri ni kwamba watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaongezeka kila mwaka na hawapungui.
Mheshimiwa Rais Magufuli, nakuomba ulichukue hili wazo na ulifanyie kazi haraka iwezekanavyo kwani huku kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Youtube, Instagram, JamiiForum, snapchat, n.k watumiaji wake, wengi wao wanapesa za kuchezea tu na hazina kazi maalumu. Kuna watu wanashinda kwenye mitandao ya kijamii siku nzima wakipost "ujinga" tu na kutukana wenzao, hivyo itakuwa bora sana kama wakianza kulipia "kodi" maalumu ya kutumia mtandao hiyo kwa siku. Sidhani kama Sh. 200 itakuwa nyingi sana kwa mtu kushindwa kulipia. Mimi binafsi nipo tayari kulipia hiyo Sh. 200 kwa siku.
Mheshimiwa Rais, nchi hii itajengwa na Watanzania wenyewe na hii ni mbinu mojawapo ya Watanzania kuchangia katika ujenzi wa nchi yao. Mitandao ya kijamii siyo chakula wala siyo maji, hivyo atakayeshindwa kulipa hiyo kodi hawezi kufa wala kudhurika kwa namna yoyote ile.
By Son of Gamba.