Leo nimepata taarifa kuwa eneo ilipokuwa kambi ya vijana Igumbilo MKoani Iringa Vigogo wa UVCCM wakiongozwa na Katibu Mkuu wao taifa, wamegawana viwanja na vingine kuviuza. HIstoria ya eneo hilo inaonesha ilikuwa ni sehemu ya Mashamba makubwa ya Tumbaku ambayo yalitaifishwa na serikali toka wa Wagiriki.
Tukio hilo likanifikirisha juu ya "uhalali" wa hao viongozi wa UVCCM kugawana hivyo viwanja vya Igumbilo. Ikumbukwe kuwa kabla ya mwaka 1965 kulikuwa na vyama vingi vya siasa mpaka pale TANU ilipotumia madaraka ya kidola kuviua. Kwa maana nyingine TANU na ASP vilipoungana mwaka 1977 vilikuwa tayari ni vyama dola. Kwa maana hiyo viwanja hivyo vya Igumbilo asili yake ni Umma na wala si CCM
Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, CCM kikiwa ndicho chama pekee cha siasa nchi, kilijichagulia jinsi kitakavyobakia ndani ya mfumo wa vyama vingi. Njia mojawapo ikaona ili kiwe salama ni kujimilikisha mali zote za umma zenye muelekeo wa kisiasa na kuzigeuza mali zake.
Lakini ni baada ya mwaka 1995 kwenye uchaguzi Mkuu ulioshirikisha vyama vingi vya siasa ulipofanyika, ndipo CCM ilipotanabahi kuwa ili iendelee kuwa madarakani ni lazima ipanue wigo wake wa kumiliki mali zilizokuwa za Umma ndani ya mfumo wa chama kimoja. Hapo sasa CCM ikapora haki ya umma ya kuvimiliki viwanja vyote vikubwa vya mpira na kuvifanya kuwa vyake. Nakumbuka Miaka michache iliyopita Amos Makala akiwa ni Mchumi wa CCM taifa aliwakumbusha wana CCM wenzake kuvitafutia viwanja hivyo hati za umiliki kwani CCCM haiwezi kukaa madarakani milele.
Kwa maneno ya Makala inaonesha kwamba CCM haikuwa inavimiliki viwanja hivyo kihalali, bali ilitumia mamlaka ya kidola kuvitangaza kuwa vyake bila hata aibu. Ukichanganya na eneo la SUKITA pale jangwani CCM imepora mali nyingi za umma bila haya wala huruma. Kama kweli Ndugu Rais, John Pombe Magufuli ni jasiri na anataka kupambana na uhalifu na uovu uliojaa katika jamii yetu, basi arudishe mali nyingi za umma zilizoporwa na CCM!