Ijumaa April 1, 2022
Dodoma, Tanzania
ABDULRAHMAN KINANA ATAKA KUIMARISHWA HAKI NDANI YA CCM ILI HAKI PIA ITENDEKE NJE YA CCM
Abdulrahman Kinana akihutubia mkutano maalum wa CCM leo mjini Dodoma .
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Samia Suluhu Hassan ameongoza kikao Cha Mkutano Mkuu maalum ambacho kimemchagua wa asilimia 100 kanali mstaafu Abdulrahaman Kinana kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara.
Mkutano huo ambao uliwakusanya wajumbe na viongozi mbalimbali wastaafu wa Chama na Serikali umepitisha mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuhusu marekebisho ya katiba ya chama hicho ya mwaka 1977 toleo la 2020
Akiongea kwenye Mkutano huo uliofanyika jana Jijini Dodoma Rais Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kutenda haki kwa kila mwanachama ili kuinua zaidi haki na maendeleo .
Akiongea mara baada ya kuchaguliwa leo, Makamu Mwenyekiti was CCM Abdulrahman Kinana alimshukuru Mwenyekiti wa CCM taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumpa imani kubwa ya kumtaka kufanya tena shughuli za chama .
“Juzi uliniita nikawa najiulia nimeitiwa nini, nikajua ni katika kusalimiana. Rais akaniambia nataka uwe Makamu Mwenyekiti, nikamwambia sina hiari, sina budi kukubali, napenda kukuhakikishia Mwenyekiti nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kufikia matarajio yako,niseme sitokuangusha”
Kinana pia amemshukuru Kamati Kuu kwa kupitisha jina lake, pamoja na wajumbe wa Halmashauri kuu kwa kupitisha na kuidhinisha jina lake na kusema wamempa imani kubwa na kwamba amejifunza mengi kutoka kwao.
“Kama mzee Philip Mangula asingeamua kustaafu, basi leo nisingekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi”
Makamu Mwenyekiti anayechukua hatamu toka kwa Philip Mangula amewashukuru Wenyekiti wote kuanzia Baba wa Taifa mpaka sasa Rais Samia Suluhu Hassan .
Kadhalika ametumia nafasi hiyo kuahidi kwenda kusimamia Chama kuwa imara kidemokrasia na kusimamia haki ya kuchaguliwa bila upendeleo na haki.
"Tukiweza kuimarisha haki ndani ya CCM, tutaweza kuimarisha haki nje ya CCM na kwa waTanzania wote "amesema Kinana .
Makamu mwenyekiti (bara) mpya ameeleza kuwa Tanzania ni nchi inayosimamia na kutetea haki hivyo lazima kusimamia haki na kuikataa dhuluma
"Lazima tutambue kuwa CCM sio mali ya Serikali japo serikali hizi mbili ya muungano na ile ya Zanzibar zinatokana na CCM, lakini pia hatupokei maelekezo kutoka Serikalini ila serikali inaelekezwa na sisi,"amefafanua na kuongeza kuwa "Serikali isithubutu kutunyanganya hiyo haki kila mwana CCM ana wajibu wa kuitetea serikali lakini inapovunja sheria tuna haki ya kuongea, tusiseme kwa kukejeli wala kufoka tuna vikao vya Chama, tutawaelekeza yale yaliyosemwa na ilani , si sawa mwanachama kwenda hadharani kuisema Serikali yake vibaya" amesema Kinana
Licha ya hayo amewataka viongozi wa CCM kuujenga utamaduni wa kuwatembelea wananchi na kuwasikiliza matatazio yao ili waendelee kuwachagua kwa sababu watatambua kuwa wanawajali na kujali shida zao kwa kuzifanyia kazi kwa njia ya kuzitatua changamoto.
"Nina hakika nitapata nafasi ya kutembelea kila mkoa kuzungumza na wanachama kwa niaba ya mwenyekiti wetu kama Katika inavyosema, nakuahidi utumishi uliotukuka sio utukufu wa kujikweza"amesema.
Licha ya hayo amezungumzia masuala yanayokwamisha maendeleo ya nchi na kueleza kuwa kichaka cha ukabila, kichaka cha udini na kichaka cha ubara na visiwani haviendani sawa na chama hicho.
Tunaweza kutofautiana kwa mengine lakini sisi ni wamoja “Lazima wanachama wawe huru kutoa mawazo, hakuna mwenye hakimiliki ya mawazo, lazima tumsikilize kila mwananchi, na wanachama wakimchagua mtu kwani sisi ni nani wa kupinga” anasema
Amesisitiza kusimamia Demokrasia na kusema ni lazima kusimamia haki.
“Nimekuwa nikimsikia Rais akisisitiza mara zote katika kusimamia haki, nilimsikia akisema vyeti peke yake siyo sifa, vyeti viendane na uadilifu, kukubalika. Nchi hii inajulikana kwa haki ndani na nje ya Nchi”anasema
Awali akimuelezea Kinana kabla ya zoezi la kupiga kura mmoja wa makada wa chama hicho na aliyewahi kushika nafasi za juu katika awamu mbalimbali kwenye serikali ya chama cha CCM, Steven Wasira amesema kuwa Kinana anazo sifa za kuwa makamu mwenyekiti wa CCM kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya ndani ya serikali na chama kwa ujumla hususani wakati chama hicho kilipopoteza mvuto na kukabiliwa na upinzani mkali kutoka vyama vya siasa mnamo mwaka 2012.
AJENDA ZA MKUTANO
Moja ya ajenda Kuu za mkutano mkuu maalum wa chama Cha Mapinduzi (CCM) ni pamoja na marekebisho yaliyofanywa wakati wa uongozi wa Hayati John Pombe Joseph Magufuli aliyewaondoa makatibu wakuu wa mikoa kuingia katika vikao vya Halmashauri kuu kwa kile kilichoelezwa kupunguza gharama.
Aidha ajenda kuu ya mkutano huo maalumu ilikuwa ni kuiidhinisha jina la kada wa chama hicho Abdulraham Kinana lililopitishwa na Kamati kuu ya CCM na hatimaye kupigiwa kura ya ndio na wajumbe wa mkutano mkuu huo maalumu, ambao mbali na ajenda hiyo pia mkutano huo ulifanya marekebisho ya vifungu na kanuni katika katiba yake ikiwa ni pamoja na sehemu ya nane ya marekebisho kwenye ibara ya 91 kifungu kidogo cha kwanza mpaka cha tisa kama anavyoelezea Katibu mkuu wa CCM Daniel Chongolo.