Mlango wa Pili
Mirengo ya Kizalendo na Mapinduzi
Mapinduzi yalikuwa, kwa kiasi fulani ni kisasi dhidi ya utumwa, yaliofanywa na watu na kufanyiwa watu ambao hawahusiki na utumwa. -Yasmin Alibhai-Brown
Fikra ya uzalendo ya Pan-Africanism ambayo ilikuwa ikiongozwa na hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa kila asiye "Muafrika" ni mgeni Afrika na kwa hiyo asiyekuwa na asili yenye kutoka bara la Afrika basi ni mgeni Zanzibar hata kama alizaliwa na alikuwa na mizizi mirefu ndani ya nchi hiyo. Na aliyekuwa ana asili ya Kiafrika na hata kama hakuzaliwa na wala hana mizizi mirefu Zanzibar basi ana haki zaidi juu ya kuitawala Zanzibar kwa sababu ni "Muafrika."
Neno "Afrika" linatokana na neno Ifriqiya, ambayo kihistoria ilikuwa ni jimbo la Kaskazini ya Afrika katika nchi ambayo leo inajulikana kwa jina la Tunisia. Ibn Khaldun, mwanafalsafa wa historia maarufu duniani na baba wa sayansi ya jamii (sociology) aliyeishi miaka 676 nyuma, anamtaja katika kitabu chake Mfalme wa zamani wa Yemen Afriqus b. Qays b. Sayfi, ambaye "aliishi wakati wa [Nabii] Musa au labda kidogo kabla yake" na kuwa wanahistoria wanajisemea kuwa ndie alieivamia "Ifriqiyah".1 Ibn Khaldun hakuwa anashuku kuwepo kwa mfalme kutoka Yemen ambaye akijulikana kwa jina la "Afriqus" ambalo inawezekana sana likawa moja wapo wa asili ya jina la "Afrika." Wako wenye kusema neno "Afrika" linatokana na lugha ya kienyeji ya Afrika ya Kaskazini iitwayo "Berber."2 Lini bara la Afrika lilianza kujulikana kwa jina la "Afrika" ni jambo liloanzishwa na wakoloni wa kizungu na ni suala linahohitajia kuthibitishwa kwa ushahidi wa kiutafiti.
Fikra zilizozagaa ni kwamba Zanzibar ni ya Muafrika mweusi mwenye asili ya bara peke yake kuliko Muafrika mwingine yeyote hata kama amezalika huko Zanzibar kwa daraja nyingi. Fikra hii inatokana na fikra nyengine iliyokalishwa kwenye fikra za wengi yakuwa "Bara la Waafrika" ni Bara la watu weusi tu, na
Mlango wa Pili
12
labda tuseme la Mungu Mweusi. Na watu weusi wenyewe ni wanaotokana na asili ya Kibantu na Wabantu wenyewe wawe hawana asili au uhusiano wa karibu na Waarabu.
Na mizizi ya "Waafrika ni Wabantu peke yao" inalitenga kundi kubwa la Waafrika wa Afrika ya Kaskazani, Ethiopia, Somalia, Djibouti, Eritrea, Mauritius, wazungu wa Afrika Kusini, au Zimbabwe, Kenya, pamoja na Mayahudi na Wahindi wazalendo wa Afrika, na makabila yote ya kibinaadamu ambayo yana chimbuko lao Afrika.
Hapana shaka yoyote kuwa Afrika imedhulumiwa na Waafrika weusi bado hawajachukuwa dhamana ya kushiriki kwa machifu na makabila yaliyoshiriki kuwatia utumwani Waafrika wenzao. Haya yameelezwa kwa ufasaha ndani ya kitabu Zanzibar: Kinyang'ayiro na Utumwa na mwaka 2009 kimetoka kitabu muhimu chenye kichwa cha maneno It's Our Turn to Eat (Sasa ni Zamu Yetu Kula) ambacho kinaelezea kwa undani namna ufisadi ulivyokumbatiana na ukabila nchini Kenya.3
Historia yote na kharita (ramani) zenye kulionyesha bara la Afrika kabla halikupewa jina la "Afrika" huonekana kuwa haina maana. Kwa hiyo kharita za miaka ya 1860 na za nyuma sana kabla ya hapo, zenye kuonyesha eneo la Afrika Mashariki kuwa likijulikana kama ni "Ethiopia" au mwambao wa "Azania" au "Sudan" au "Zinjibar" huonekana ni dalili tosha za ushahidi wa ubeberu kabla ya "Waafrika" kujitawala baada ya Wazungu kulipa bara lote jina la "Afrika."
Tawi la uafrika ni mtu mweusi lina mzizi mrefu katika kuyakana makabila mengine ya Kiafrika ambayo yaliwasili mwambao wa Afrika hata kabla ya kuwasili Wabantu Pwani ya Afrika ya Mashariki. Anaelezea Profesa Ibrahim Noor Shariff:
Kuna baadhi ya watu wanafikiri kuwa "Waafrika" wote ni "Wabantu" na kuwa kila asiyekuwa Mbantu ni mgeni Afrika Mashariki. Ukweli ni kuwa "Wabantu" ndio katika waliofika Afrika Mashariki, khasa sehemu za Pwani karibuni kabisa. Kwa mfano, "Wabantu" Wagiriama wamewasili "Giriama" Kenya kama miaka mia tatu iliyopita. (Soma kitabu cha chifu wao R. G. Ngala kiitwacho "Nchi na Desturi za Wagiriama." E. A Literature Bureau. 1949. Ukurasa wa 2).4
`Mohamed Said ni msomi wa kwanza kabisa aliyeweza kuweka mkono wake juu ya mpigo wa moyo wa propaganda ya TANU kuhusu suala la Ubantu na wasio Wabantu, yaani, Waislamu. Kwa mujibu wa Mohamed Said:
Katika mwaka 1955, kikundi cha TANU Bantu kiliundwa makhsusi kukabiliana na tatizo la udini kutokana na hisia za baadhi ya Waislam ndani ya TANU. Tangu kuundwa kwa TANU, kulikuwa na hisia ya kupinga Ukristo ndani ya chama. Tatizo hili la udini lilikuwa likichemka pole pole na chini kwa chini ndani ya TANU.
Ilikuwa kazi ya kikundi cha TANU Bantu kuwafichua na kuwapiga vita wanachama wa TANU waliokuwa na hisia kama hizo. Bantu ilifanikiwa sana katika
Mirengo ya Kizalendo na Mapinduzi
13
hili hadi kudiriki kupiga marufuku mamkuzi ya Waislam ya "Asalaam Alaikum" (Amani iwe juu yako) baina ya Waislam kwa msingi kuwa ilikuwa inawabagua Wakristo na hivyo inawatenga…Mamkuzi yale ya Kiislam yalionekana kama yanakwenda kinyume na imani ya TANU na ilishauriwa kuwa "salaam aleikum" ipigwe marufuku isitumike. Ikiwa mathalan kwa kusahau Muislam mmoja atatoa salaam kwa Muislam mwenzake, kwa kawaida angejibiwa "Alaikum salaam" maana yake "Amani iwe juu yako pia." Badala ya majibu haya mazuri, majibu yaliyobuniwa na Bantu yalikuwa-"Ahlan tabu" maana yake-"ah tabu tu!"5
Lengo la Bantu Pan-Africanism si kuutumikiya uhakika wa historia au kuwapenda Waafrika na kuwachukiya Waarabu, bali ni kulipuuza suala zima la makabila, tamaduni, na staarabu na dini ya Kiisilamu zilizokuwepo Afrika ya Mashariki kabla ya kuwasili kwa Wabantu na khasa kwa Ukristo kutoka Ulaya. Mgeni mmoja kutoka Umoja wa Mataifa aliyekwenda kuitembeleya taasisi ya kihistoria ya kitaifa iliopo Dar es Salaam, alisikitishwa sana kuona historia ya Waarabu Tanzania imeshirikishwa na kitu kimoja tu: utumwa. Wanahistoria na wataalamu wa ilimu ya athari (archaeology) wanashindana na kuukiuka au kuuficha ukweli wowote ule wenye kuonyesha kuwa hakujakuwepo makabila yasiyo ya Kibantu Afrika ya Mashariki kabla ya kuwasili kwa Wabantu.
Ile historia ndefu ya Bahari ya Hindi yenye kuiunganisha Afrika ya Mashariki na ya Kati na Bara Arabu, Uajemi, Bara Hindi, Uchina, Misri, n.k, huwa inaonekana haina maana kwa sababu haikidhi haja na hoja za kisiasa. Au kama itatambulikana itakuwa kujengea hoja kuwa ilikuwa historia ya kibeberu iliyokuwa na kituo chake Zanzibar. Marejeo ya historia ya Afrika ya Mashariki yaliyoandikwa na akina Ibn Battuta, au Muruj al-Dhahab wa Ma'adin al Jawhar cha Al-Masudi, au Kilwa Chronicles iliopo jumba la makumbusho la Uingereza, hayapitiwi na wasomi wengi wa Tanganyika waliojazwa na kujaa chuki dhidi ya makabila mengine yasiyo ya Kibantu ya Afrika ya Mashariki.
Katika utangulizi wa kitabu chao Mapambano ya Ukombozi Zanzibar, B.F. Mrina na W.T. Matokke wa Chuo Kikuu cha Chama, Kivukoni, wanafafanuwa kuwa: "Madhumuni ya kuandika kitabu hiki ni kujaribu kukusanya pamoja data kwa ajili ya kuweza kufundishia. Jitihada zilizofanywa zilikuwa na lengo la kupata maandishi ambayo yanaweza kutumiwa na walimu na wanafunzi katika Vyuo vya Chama Cha Mapinduzi."6
Pia katika sifa iliyopewa kitabu na kampuni ya uchapaji, Tanzania Publishing House, ni hii propaganda bila ya kizoro ambayo nainukuu kwa urefu:
Historia ya Afrika ni hadithi ndefu ya mapambano ya wananchi wake dhidi ya ubeberu ili waishi katika ardhi yao kwa amani na ustawi. Visiwa vya Unguja na Pemba havikukwepa adha ya kuwa sehemu ya uwanja wa mapambano hayo na kwa vizazi vingi vimekuwamo katika harakati moja baada ya nyingine hadi Mapinduzi ya 1964 yaliyokatilia mbali minyonyoro ya ukoloni mkongwe na kuashiria maisha mapya.
14 Mlango wa Pili
Mapambano ya Ukombozi Zanzibar ni kitabu cha kwanza kuchapishwa kinachofuatilia kwa undani safari ndefu ya wananchi wa Zanzibar kuelekea ukombozi tangu majilio ya kwanza ya wageni kwenye pwani ya Afrika Mashariki yapata miaka 2000 sasa….Ndugu Mrina na Ndugu Matokke wamefanya utafiti wa hali ya juu uliowawezesha kutalii sehemu nyingi za historia ya Zanzibar ambazo hazijaguswa na mwandishi mwingine yeyote. Matokeo yake ni kitabu cha lazima kwa wanafunzi wa historia na siasa katika ngazi zote.7
Bila ya kutowa ushahidi wa marejeo yoyote yale, Mrina na Matokke wanakiri kuwa "Pwani ya Afrika Mashariki ilikuwa imefikiwa na wageni kutoka sehemu za mashariki ya mbali yapata miaka 500 kabla ya kuzaliwa Kristo."8 Katika safari yao ndefu ya "utafiti wa hali ya juu" Mrina na Matokke hawakutaka kujuwa nini kimeandikwa katika kitabu maarufu duniani The Periplus of the Erythrean Sea kilichoandikwa miaka 2000 iliyopita kuwepo kwenye pwani ya Afrika Mashariki kwa karne nyingi tawala za kifalme za Arabuni ya Kusini na kuwa Waarabu "walikuwa wameingiliana na kuowana na wenyeji na wakiifahamu pwani nzima na lugha zilizokuwa zikizungumzwa."9
Mrina na Matokke hawakujali kuyapitia matokeo ya utafiti makini wa wanahistoria na mabingwa wa ilimu ya athari (archaeology) au hata Biblia yenye kumtaja Kush na watu wa kutoka ustaarabu wa Kikushi ambao wanaiunganisha Afrika Mashariki na Somalia, Ethiopia na Bara Arabu. Lakini hilo halikuwa lengo lao na ndio maana safari yao haikuwapeleka huko. Lengo lao lilikuwa kupiga siasa na kuziharibu akili za walimu na wanafunzi kutoka Zanzibar na Tanganyika.
Misafara ya masomo ya dhiki na dhuluma
Hadithi dhidi ya Waswahili na Waarabu ambazo hazitegemei aina yoyote ile ya ushahidi zimekithiri kama uyoga kunako vichwa na nyoyo zenye kuipa jina baya Dola ya Zanzibar ili ipatikane sababu ya kuiangusha au kuizuwia isije juu. Yako mambo mtu akisema hapohapo hutakiwa ushahidi na hoja mpaka msikilizaji aridhike na kuna mambo hayahitajii hata chembe moja ya ushahidi midamu makapi ya hoja yanaonekana.
Kwa mfano, R. K. Mwanjisi kwenye kijitabu chake Abeid Amani Karume utakuta ameandika kuwa:
Kuna mambo mengi sana ambayo yalitendeka nchini Unguja na Pemba na ambayo hayana budi yathibitishwe kwa ushahidi kamili, na kuandikwa kwa makini.
Kuna nyumba Unguja iitwayo "Mambo Msiige" ambayo baada ya kumalizika kujengwa wale Waafrika walioijenga waliuwawa wote ili wasiige maarifa ya ujenzi wa nyumba kama ile.
Yasemekana pia kuwa wake za Waarabu siku hiyo wakifurahi huwaambia mabwana zao "mie sijapata kuona mtoto anavyokaa tumboni mwa mwanamke,
Mirengo ya Kizalendo na Mapinduzi 15
nataka kuona hivi leo." Basi bwana wa Kiarabu hutuma watumwa wake wamlete mama wa Kiafrika mja mzito na akapasuliwa tumbo kumwonyesha bibi mkubwa jinsi mtoto anavyokaa tumboni! Kisha maiti ya yule mjakazi wa Kiafrika ikatupwa shimoni!
Yasemekana kuwa wakati huo Mwarabu akitaka kuhakikisha ikiwa gobori lake lina nguvu humwambia mmoja wa watumishi wake apande mnazi. Akiisha fika juu yule "Bwana" alifyatua gobori lake, kisha "Mtumwa" akalia "Yallah" akaanguka chini na kufa. Kiisha yule Mwarabu akaja na kuipiga teke ile maiti na kusema "Ama, hivi kafa huyu!"
Inasemekana kuwa kuna Mwarabu mmoja alizaa mtoto na mtumwa wake Mwafrika. Jambo hili lilipojulikana yule Mwarabu akachukua kisu akamwua yule kijakazi wake na kumtumbukiza chooni!10
Hizo ni sumu kali ndani ya kijitabu ambacho lengo lake ni kuzielezeya habari za maisha ya Mzee Abeid Amani Karume kwa wasomaji ambao wanatakiwa wafahamu kuwa:
Unguja na Pemba imepita katika tanuri la moto wa utumwa, udanganyifu wa wafanya biashara na washika misahafu, utawala wa kigeni, ubaguzi wa rangi, utetezi, juhudi za uhuru, mapinduzi na ujamaa.11
Cha Mwanjisi ni kijitabu kidogo kilichotungwa kwa ajili ya wasomaji wa kawaida. Mambo yalizidi kuwa hatari wakati kasumba kama za Mwanjisi zilipoingizwa ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Zanzibar. Na hayo yalifanywa na Wazanzibari Waafrika Waislamu ambao walitekwa akili na hadithi za utumwa zisizokuwa na hata chembe moja ya uthibitisho. Angalau Mwanjisi alitahadharisha kuwa hadithi zake kuhusu ushenzi na mambo maovu kabisa ya Waarabu waliyowafanyiya Waafrika "hayana budi yathibitishwe kwa ushahidi kamili, na kuandikwa kwa makini."
Akina Luteni Kanali Musa Maisara Kheri, mkuu wa uandishi na muandikaji wa utangulizi, Maalim Ubwa Mamboya Ismail, Mwenyekiti wa halmshauri ya uandishi wa kitabu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania, 1964–1974, Zanzibar na ndugu zao wengine wa Kiislamu walioshiriki kwenye uandishi wa kitabu hicho, hawakuiyona haja wala madhara ya kuitumiya sumu ya hadithi zisizo na uthi-bitisho wowote midam sumu hiyo iliwapa uhai wenye utukufu wa kidunia. Mafunzo ya dini ya Kiislamu na ule msemo wa Imam Ali usemao "Utukufu hupatikana kwa kumtumikia Muumba na mwenye kuutafuta kwa viumbe hatoupata" haukuwa na maana yoyote kwao.
Jambo la kupendeza lilikuwa kwamba mpaka mwaka 1974 kulikuwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Zanzibar. Zanzibar ikijilinda wenyewe. Mambo makubwa zaidi ni yale yenye kuwasononesha wale waliohusika katika kushiriki kuwauwa ndugu zao ambao leo wameshakuwa watu wazima na kesho kuna kukutana na Muumba wao. Kitabu hicho kiliandikwa chini ya uwenyekiti wa