Marekani imewawekea vikwazo maafisa wakuu katika mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC akiwemo kiongozi mkuu wa mashitaka Fatou Bensouda.
Waziri wa masuala ya kigeni nchini humo Mike Pompeo alishutumu mahakama hiyo kwa kujaribu kuwashtaki raia wa Marekani.
Mahakama hiyo iliopo mjini Hague kwa sasa inachunguza iwapo vikosi vya Marekani vilifanya uhalifu nchini Afghanistan.
Marekani imeikosoa mahakama hiyo tangu ilipoanzishwa na ni miongoni mwa mataifa mengi ambayo hayajatia saini mkataba wa raia wake kushtakiwa na mahakama hiyo.
Balkess Jarrah , wakili mkuu katika shirika la haki za kibinadamu la Human Rights Watch alishutumu vikwazo hivyo kama aibu kwa Jukumu la Marekani kutoa haki kwa waathiriwa wa uhalifu.
Hatua ya Bw Pompeo iliashiria "upotoshaji wa vikwazo vya Marekani, unaolenga kuwaadhibu wanyanyasaji, na badala yake kuwalenga wale wanaoshtaki uhalifu wa kivita", alijibu ujumbe wa twitter.
Ikiwa mahakama ilioanzishwa kupitia azimio la Umoja wa Mataifa 2002, ICC inachunguza na kuwashtaki wale wanaohusika na mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, kuingilia kati iwapo mataifa yameshindwa kuwachukulia hatua waliohusika.
Je, mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ni ipi?
Azimio hilo lilipitishwa na mataifa 123, ikwemo Uingereza.
Lakini Marekani pamoja na China india na Urusi zimekataa kujiunga nayo , huku baadhi ya mataifa ya Afrika yakiishutumu kwa kuwalenga sana viongozi wa Afrika.
Je, vikwazo hivyo ni vipi?
Rais Donald Trump alitoa agizo mwezi Juni, ambalo linaruhusu Marekani kuzuia Mali ya wafanyakazi wa ICC na kuwazuia kuingia katika taifa hilo.
Akiwahutubia wafuasi wake siku ya Jumatano, bwana Pompeo alisema kwamba bi Bensouda na Phakiso Mochokochoko, mkuu wa Idara ya Mamlaka, na kitengo cha Ushirikiano, walipaswa kuwekewa vikwazo kupitia agizo lake.
Akiishutumu mahakama hiyo kama taasisi iliofeli na fisadi , alisema kwamba wale wanaoendelea kuwaunga mkono maafisa hao pia wanahatarisha kuwekewa vikwazo.
Wizara hiyo pia ya Marekani pia imezuia utoaji wa visa kwa wafanyakazi wa ICC wanaohusika na juhudi za kuwachunguza wanajeshi wa Marekani.
Maelezo ya picha,
Mahakama ya ICC ilisema kuwa haitazuiwa na vitisho vya Marekani kufanya majukumu yake
Wakati Rais Trump alipotoa agizo hilo la rais mwezi Juni, mahakama ya ICC ilipuuzilia mbali kile ilichokitaja vitisho zaidi na vitendo vya kulazimisha, dhidi yake.
''Shambulio lolote dhidi ya ICC pia linawakilisha shambulio dhidi ya waathiriwa wa uhalifu , wengi ambao mahakama hiyo inawakilishi matumaini yao ya mwisho ili kupata haki'', ilisema taarifa yake.
Je, Fatou Bensouda ni nani?
Kama waziri wa haki wa zamani nchini Gambia, taifa analotoka, bi Bensouda alitarajiwa kumrithi Luis Moreno Ocampo kama mkurugenzi wa mashtaka katika mahakama hiyo baada ya kuhudumu kama kaimu wake wakati wote huo.
Awali aliwahi kuhudumu kama mshauri mkuu wa masuala ya kisheria katika jopo la mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa mataifa ambayo iliwahukumu viongozi wakuu wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda 1994.
Huku akihusika katika kupanua uchunguzi wa ICC ili kuangazia mizozo kwengineko hatua iliomfanya kuadhibiwa na Marekani, Afrika ndio lengo lake kuu.
Maelezo ya picha,
Mahakama ya kimataifa imekuwa ikikosolewa vikali hivi karibuni na Marekani.
Kesi zote za ICC zimekuwa zikiangazia viongozi wa Afrika na kiongozi mmoja wa wapiganaji kutoka nchini DRC , Thomas Lubanga, alikuwa mtu wa kwanza kuhukumiwa kwa uhalifu wa kivita na ICC 2012.
Lakini Bensouda pia alishindwa na misururu ya kesi, ikiwemo kuwachilia huru kwa aliyekuwa rais wa Ivory Coast Lauirent Gbabgo aliyeshtakiwa kwa mashtaka ya uhalifu wa kivita 2019 na kuondolewa kwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu dhidi ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta 2014.
Je, ICC inachunguza nini?
Mahakama ya ICC ilianza kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita yaliotekelezwa nchini Marekani na mengine katika mzozo wa Afghanistan mapema mwaka huu.
Kulingana na Mchakato wa sheria ya ICC, mahakama hiyo inaweza kutoa waranti za kukamatwa kwa washukiwa wanaolazimika kuwasili mbele ya mahakama hiyo inapopata ushahidi wa kutosha na kuwatambua.
CHANZO CHA PICHA,AFP
Maelezo ya picha,
Bwana Pompeo aliapa kuwalinda Wamarekani dhidi ya Mahakama ya ICC
Baadaye itaamua iwapo kuna ushahidi wa kutosha kwa kesi kusikilizwa. Wakati huo, Bwana Pompeo aliapa kuwalinda Wamarekani, akiitaja mahakama hiyo kuwa taaisi isiowajibika inayojifanya kuwa bodi ya kisheria. Ripoti ya 2016 kutoka kwa ICC ilisema kwamba kulikuwa na sababu za kutosha kuamini kwamba jeshi la Marekani liliwatesa washukiwa katika eneo moja la siri linalosimamiwa na shirika la CIA. Afghanistan ni mwananchama wa mahakama hiyo lakini maafisa wameonesha pingamizi yao kuhusu uchunguzi huo.
Shukrani kwa bbc