KIFO cha Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe kinazidi kuibua mengi baada ya mke wake wa kati Dotto Mohamed kukana maelezo ya mke mdogo Mariam Wangwe kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitelekeza familia.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dotto alisema kauli ya Mariam ni nzito mno kuitoa sasa kwani anaamini matukio yanayoendelea baada ya kutokea msiba huo, ndiyo yanayoweka pazia la mawasiliano kati ya Chadema na familia ya Marehemu.
"Sijaisoma taarifa yote ila mtoto wangu ameniletea gazeti ambalo bado ninalo. Mimi ninashindwa kufikiria wala kuwaza kuanza kukilaumu Chama kwamba kimetutelekeza kwani ni mapema mno kufanya hivyo na wote bado tuko kwenye majonzi," alisema Dotto na kuongeza:
Nasema nashindwa kukilaumu chama kwa sababu tangu kutokea kwa msiba huo hakuna aliyetulia, familia bado ina majonzi, chama chenyewe bado kinalia na hata jamii inaendelea kumlilia Wangwe nasema familia yangu bado ina imani na chama na hatuwezi kukilaumu sasa," alisema.
Dotto alisema anaamini Chadema inaongozwa na watu wenye busara hivyo hawezi kuinenea mabaya kabla ya kuridhika kwamba viongozi hao wameanza kupingana na busara hiyo.
"Ninihitaji muda kupima hekima ya chama kabla sijakihukumu kwani kinyume chake nitakuwa sijakitendei haki," alisema.
Alisema mpaka sasa bado anaamini kuwa Chadema iko sambamba na familia ya marehemu Wangwe kwani hata kwenye arobaini iliyofanyika kijijini Komakorere chama hicho kilituma wawakilishi.
Mke huyu wa pili wa Chacha Wangwe anaishi jijini Mwanza na jana alikuja jijini Dar es Salaam kuwachukua watoto wake wawili waliokuwa wakiishi na Mariam, mke mdogo wa Wangwe.
Jana Dotto aliiambia Mwananchi kuwa katika safari yake hiyo pia amepanga kukutana na Mariam na kuzungumza naye ili ajue kiini cha shutuma zake kwa Chadema.
"Kuja kwangu Dar es Salaam ni pamoja na kuwachukua wanangu wawili ambao wamekuwa wakiishi na Mariam; katika ujio huo tutakaa tuzungumze anieleze kwa nini ameamua kuzungumza maneno hayo sasa,".
Alisema hata kama Mariam atafanikiwa kumshawishi aamini maneno yake, bado atahitaji muda kukubaliana naye kwani anaamni kuwa bado ni mapema mno kutoa shutuma hizo.
"Sisi bado tuna imani na Chama na hatuwezi kujua chama kinatuwazia nini hivyo narudia: ni mapema mno kutoa shutuma hizo kwani wote bado tuko kwenye majonzi," alisisitiza.
Akizungumzia kauli ya Dotto, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema ndiyo aliyotarajia kusikia kutoka kwa familia ya marehemu Wangwe.
"Nafikiri kauli hiyo ndiyo niliyotarajia kutoka kwa familia ya Wangwe ninayemfahamu kwa sababu kama utakumbuka tangu mwanzo wa msiba, sisi (CHADEMA) tulikuwa tukisakamwa sana lakini tulikaa kimya kwa busara ili tusimkamate mchawi asiyetuhusu," alisema.
Dk Slaa ambaye alisisitiza kwamba hamfahamu Mariam kama mke wa marehemu Wangwe, alisema anasikitishwa na kauli yake ambayo anaamini kuwa imelenga kukichafua chama.
Hiki anacholalamikia kwamba Chadema hawakuhudhiria arobaini ya mume wake, nashindwa kuelewa. Kumbuka mimi nina miaka 60 na tangu nianze kufahamu arobaini, najua zinafanyika mahala alikozikwa marehemu.
Wangwe alizikwa Komakerere na arobaini yake ilifanyika huko na Chadema tulituma mwakilishi. Hii arobaini aliyoifanya Mariam na Profesa Wangwe Dar es Salaam hatukuijua wala wao hawakutaka Chadema iijue," alisema.
Akifafanua alisema ingawa Mariam alitoa taarifa ya arobaini aliyoifanya Dar es Salaam, waalikwa katika taarifa hiyo ni wabunge kwa majina yao na sio Chadema kama taasisi.
Alisema pamoja na kasoro hiyo wabunge wa Chadema Suzan Lyimo na Grace Kihwelu walihudhuria kwa kofia zao lakini waliwakilisha chama kwa salamu ambazo zilisomwa na Lyimo katika hafla hiyo.
"Mimi Dk Slaa nilialikwa kwa ubunge wangu na sio ukatibu mkuu wa Chadema na Mbowe alialikwa kwa jina lake na sio uenyekiti wa Chadema vivyo hivyo wabunge wengine. Sasa Chadema inapolaumiwa tunashindwa kuelewa," alisema na kuendelea
"Mimi namshauri Mariam akutane na wazee wamshauri kwanza badala ya kukurupuka na kutoa maneno ya kukipaka matope chama. Yeye anataka athaminiwe, atathaminiwaje kama yeye Mariam hataki kukithamini chama," alihoji
Kauli ya Dotto na Dk Slaa imekuja siku tatu baada ya mke wa tatu wa Marehemu Wangwe kuzungumzia utata wa kifo cha mumewe na kukitupia lawama Chadema kwamba kimeitelekeza familia baada ya kifo hicho.
Mariam alienda mbali zaidi na kumtaka spika wa Bunge Samwel Sitta kuchunguza kifo hicho akidai kuwa haridhiki na uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi.
Wangwe, mwanasiasa machachari aliyepata umaarufu kwa kuibua hoja tata bungeni, alifariki dunia katika ajali ya gari wakati akisafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kuhudhuria mazishi ya mfanyabiashara na mbunge wa kwanza wa jimbo la Tarime Bhoke Munamka.
Lakini mazingira ya kifo chake yalizua utata mwingi baada ya kuchukuliwa kama agenda ya uchaguzi mdogo katika kampeni zinazoendelea sasa jimboni humo kumpata mrithi wa kiti chake.
Tayari Jeshi la Polisi limemfungulia mashtaka Deus Mallya aliyekuwa akisafari na marehemu kwa tuhuma za kusababisha mauaji hayo.
Lakini mke huyo mdogo wa Wangwe anaona juhudi hizo za polisi ni ndogo na hivyo, serikali na Spika Sitta hawana budi kuongeza uzito wao.
Sipendi mambo haya yaishe hivi hivi," alisema mama huyo. "Familia ya Wangwe haijaridhishwa na namna polisi wanavyofuatilia kifo cha Wangwe."
"Wasiwasi wangu ni uchunguzi unaofanywa na polisi kwani hawajawahi hata kufika kuniuliza kuhusu kifo cha Wangwe nikiwa kama mke wake.Labda maelezo yangu yangewasaidia kwa kiasi fulani.
Akizungumzia hali ilivyokuwa katika kipindi cha kuelekea kifo cha mumewe, Mariam alisema mambo yalikuwa magumu sana nyumbani, hasa baada ya Wangwe kusimamishwa nafasi yake ya makamu mwenyekiti wa Chadema.
Pia Mke wa pili wa marehemu Chacha wangwe,Doto amesema cha msingi ni viongozi kusaidi kulea watoto tisa aliowaacha marehemu ambao ni Zakayo na Rhobi (1 ambao ni mapacha, Bob (17), Pendo (16), Beatrice, (15) na Wangwe mwenye miaka 14 ambao ni watoto wa mke mkubwa nayeitwa Ghati.
Kwa yeye Doto ana watoto wawili, Mwajuma (11) na Ghati (6) wakati Mariam ana mtoto mmoja anaitwa King (1).
Naye Beatrice Charles, anaripoti kuwa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dar es Salaam kimemtaka katibu wa chama hicho, Wilbroad Slaa kumuomba radhi mjane wa marehemu chacha Wangwe kwa kutomtambua kuwa ni mjane wa Chacha Wangwe.
Akizungumza na waandishi wa habari Jiji jana katibu wa vijana Wilaya ya Kinondoni Mauld Mkwanji alisema Dk Slaa anapaswa kumuomba radhi mjane huyo kutokana kutomtabua.
Kauli hiyo imetukwaza sana sababu marehemu Wangwe hakuwa msiri na wakati wa uhai wake alimtambulisha mkewe wake kwa viongozi wa chama na walikuwa wanamfahamu vizuri sasa iweje wasimtambue, alisema Mkwanji.
Alisema kitendo cha Dk Slaa kutomtambua mjane huyo ni kutomtendea haki na kwamba anapaswa kumuomba radhi.
Alisema kitendo cha katibu huyo kinaweza kuendeleza chuki katika familia hiyo.