Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Bw.Zelothe Stephen aliwataja watuhumiwa wawili kuwa ni Mchungaji wa kanisa la Pentekoste Idiwili,Cosmas Mwasenga (39) na Luseshelo Mwashilindi (38) ambao walikutwa na viungo vinavyodhaniwa vya maeneo ya mikono wakipita kutafuta wateja huku wakiviita kwa jina la ¡viungo vya Kunguru mweupe¢.
Kamanda Stephen alisema kuwapolisi walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu kuwepo watu waliokuwa wanatafuta wateja wa viungo hivyo vya albino katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Makunguru na Mwanjelwa wakitamka jina la kunguru mweupe.
Alisema kuwa polisi baada ya kupata taarifa hiyo waliweka mtego kwa kujifanya wanunuzi ambapo baada ya kupata bei hiyo walikwenda kuchukua viungo hivyo kwa mtuhumiwa Mwashilindi na kuvikuta huku vikiwa vimefungwa kwa mafungu mawili yaliyokuwa na vipande vinne vya viungo hivyo vikiwa vimewekwa katika karatasi.
Aidha Kamanda Stephen alisema kuwa baada ya kuwakamata watuhumiwa wote wawili walikwenda kufanya upekuzi katika nyumba ya Mchungaji Mwasenga na kufanikiwa kukuta chupa ya dawa ya sindano ya kutibu binadamu aina ya Penicilline na maji yake sanjari na koti jeusi.
Kamanda Stephen alisema watuhumiwa wamekamatwa na watafikishwa mahakamani muda wowote baada ya uchunguzi kukamilika na kwamba viungo hivyo vinatarajiwa kufikishwa kwa mkemia mkuu kwa uchunguzi zaidi.
Katika tukio jingine Kamanda Stephen alisema Bw.Saimon Masawe (42),mkazi wa Ivumwe (Baba mzazi wa kijana mwenye ulemavu wa ngozi) pamoja na balozi wa mtaa wa Ivumwe wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhusika kumnyoa nywele kijana huyo sanajri na kutowajibika kumlinda mlemavu huyo wa ngozi.
Kamanda Stephen alisema kuwa mnamo februari,5 mwaka huu majira ya saa 12.45 asubuhi kijana huyo aliamka na kwenda shuleni lakini baada ya kufika umbali wa mita 400 na kubakisha mita takribani 600 alivamiwa na kukamatwa na watu watatu wakiwemo wanaume wawili na mwanamke mmoja na kumficha karibu na tanuri la matofari.
Alibainisha kuwa kijana huyo alidai kuwa alikalishwa katika kaaratasi la nailoni na kuanza kunyolewa nywele zake za katikati na kubakishwa nywele za pembeni mithili ya mtu mwenye upara ambapo wakati zoezi hilo linaendelea alipita mtu akiwa katika baiskeli akiendelea na safari zake bila kujuwa kilichokuwa kinatendeka na ndipo watu hao waliingiwa na hofu na kukimbia.
Kamanda huyo alifafanua kuwa kabla ya kukimbia watu hao walimchanja kwa wembe chale mbili ndogo katika mkono wake wa kushoto na kumtelekeza kijana huyo ambaye baadaye aliondoka kuelekea shuleni akiwa ameficha kichwa chake kwa kofia bila kumweleza mtu yeyote hadi aliporejea nyumbani na kumweleza mama yake mzazi aliyetajwa kwa jina la Upendo masawe (40).
Alisema kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo Mama huyo aliwaita majirani pamoja na balozi kuwasimulia mkasa huo na ndipo walipochukua hatua ya kutoa taarifa polisi ambapo baada ya kumhoji baba yake mzazi alidai aliondoka mapema alfajiri kuelekea shambani na kurudi usiku na kukuta taarifa hiyo.
Kamanda Stephen alisema kuwa baada ya mahojiano hayo polisi wanamshikilia baba wa kijana huyo kwa uzembe wa kutomfuatilia kijana wao huku wakijuwa kuwa maisha yao yapo hatarini ambapo balozi ametiwa mbaroni kwa kutowajibika ipasavyo kuhakikisha mlemavu huyo analindwa muda wote kuanzia nyumbani hadi shuleni mpaka anarudi nyubani.
Hata hivyo kamanda Stephen alifafanua kuwa kama ilivyoamua serikali kupania kuwalinda kwa nguvu zote watu wenye ulemavu wa ngozi na ndivyo viongozi wengine na wananchi kwa ujumla wakiwemo wazazi wanavyotakiwa kuwajibika.
source:
Dullonet Tanzania | Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste akamatwa na viungo vya Albino.