2009-03-15 13:56:15
Na Thobias Mwanakatwe, Mbeya
Kwa mara ya kwanza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Zelothe Stephen, ameongea na waandishi wa habari na kusema mchungaji Cosmas Mwasenga anayetuhumiwa kukutwa na viungo vya binadamu pamoja na mwenzake Luseshelo Mwashilindi, walikamatwa na viungo hivyo vinavyosadikiwa kuwa vya albino wakiviuza kwa Sh. milioni 30.
Alisema walikamatwa Februari 13, mwaka huu baada ya polisi kupata taarifa kuwa kuna watu wanauza viungo vya albino na hivyo polisi kuweka mtego uliofanikisha wakakamatwa.
Alisema Februari 12, mwaka huu polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna kikundi cha watu katika mji wa Mlowo wilayani Mbozi wana viungo vya bindamu vinavyodhaniwa kuwa vya albino na kwamba walikuwa wakiwatafuta wateja wa kuvinunua.
Kamanda Stephen alisema watu hao walizagaa kutafuta wateja wa kununua viungo hivyo hadi katika maeneo ya Mwanjelwa na Makungulu jijini Mbeya na ndipo polisi waliweka mtego wa kumtafuta mtu wa kuvinunua ambapo alipotafutwa muuzaji walikubaliana kwa bei ya Sh. milioni 30 na kwamba viungo hivyo vilikuwa vimehifadhiwa nyumbani kwake mjini Mlowo.
Alisema hata hivyo kwa kuwa kiasi hicho cha pesa kilikuwa kikubwa, mnunuzi alimuomba muuzaji ampe muda wa kutafuta pesa zaidi ili kufikia kiwango hicho anachohitaji na ndipo siku iliyofuata Februari 13, polisi walifanya maandalizi na walifika nyumbani kwa Mwashilindi ambaye alitoa vipande viwili vya viungo vya binadamu na papo hapo akatiwa mbaroni.
Alisema polisi walifanya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ambapo alikutwa na viungo vya binadamu vinavyodhaniwa kuwa vya albino, dawa ya bindamu aina ya penincilin, maji ya kuchanganyia dawa pamoja na koti jeusi ambapo alipohojiwa zaidi alidai alikuwa akishirikiana na mchungaji wa kanisa la Pentekoste Idiwili, Mchungaji Mwasenga.
Wakati huo huo, tukio la kukamatwa kwa mchungaji huyo limeendelea kuzua mapya baada ya kubainika kuwa polisi watano walikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwake usiku wa manane bila kuwa na `search warrant`.
Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Idiwili wilayani Mbozi, Sanston Mkondya, katika taarifa yake aliyoiwasilisha kwa tume ya madhehebu ya dini mkoa wa Mbeya ambayo inachunguza suala hilo, alisema maofisa hao wa polisi baada ya kufika nyumbani kwa mchungaji huyo walianza kufanya upekuzi bila kuwa na `search warrant\' kama taratibu za sheria zinavyoelekeza.
Maofisa wa polisi waliokwenda kuendesha upekuzi huo nyumbani kwa mchungaji ni Staff Sajenti Datstan mwenye namba E.276 D/SGT ambaye ni Mkuu wa kituo cha polisi Mlowo, Saff sajenti Daniel (F 679D/SGT), Inspekta Ndimbo na Inspekta Malindisa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Idiwili, Mkondya, ambayo itapelekwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), imeeleza kwamba maofisa hao wa polisi walifika nyumbani kwa mchungaji huyo majira ya saa 7 usiku wakiwa na mchungaji huyo ambaye alikuwa amewekwa chini ya ulinzi.
Baada ya kufika nyumbani kwa mchungaji huyo, Ofisa Mtendaji ambaye alichukuliwa ili kuwa shahidi wakati wa upekuzi aligonga mlango ambapo mke wa mchungaji huyo, Pili Mwembe, alifungua na Mtendaji kuanza kuwatambulisha maofisa hao wa polisi.
Inadaiwa kabla ya kuingia ndani na kuanza kazi rasmi ya kupekua, Ofisa Mtendaji aliwataka maofisa hao kwanza wampatie `search warrant` ambapo hata hivyo hawakuwa nayo lakini baada ya kujitetea waliruhusiwa kufanya upekuzi kwa makubaliano kuwa wataiandika baadaye.
``Baada ya kazi ya upekuzi kukamilika niliwaambia twendeni ofisini kwangu, ili waandike madhumuni ya kumpekuwa Mchungaji Masenga ambapo walikubali na niliwasha taa ndipo wakaandika hiyo `search certificate,`` imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ambayo Nipashe inayo nakala.
Ofisa Mtendaji huyo hata hivyo katika taarifa hiyo pamoja na maelezo yaliyoandikwa na maofisa wa polisi ameeleza kwamba katika upekuzi huo hawakukuta kitu chochote nyumbani kwa mchungaji huyo.
Alisema baada ya siku 12 Mkuu wa Kituo cha polisi Mlowo, Staff Sajenti Datstan alifika kijijini Idiwili ambapo aliulizwa ni sababu gani zilizosababisha kukamatwa kwa mchungaji Mwasenga na kueleza kuwa Mwashilindi na kundi lake la majambazi walipokamatwa na kupekuliwa walikuta koti jeusi ambalo walidai ni la mchungaji huyo.
Tukio la kukamatwa mchungaji huyo limekuwa gumzo kubwa mkoani hapa ambako kila siku mapya yamekuwa yakiibuka ambapo wiki iliyopita mtu mmoja alikwenda nyumbani kwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Zebadia Mwakatage, akimuomba ampe rushwa ya Sh. 150,000 akidai ametumwa na polisi wanaopeleleza kesi hiyo waweze kumuachia huru mchungaji wake.
* SOURCE:
Nipashe