Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 23,526
- 34,057
View: https://youtu.be/RWa5mN3dgSI?si=ft38Wy6v-jqDon9N
MAULID YA MAFUNGO SITA MNAZI MMOJA YATIMIZA MIAKA 100
KAMATI YA MAULID YA DAR ES SALAAM 1926
Baada kuunda African Association, mwaka 1933 Kleist na baadhi ya rafiki zake wengine walianzisha Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika).
Kabla ya kuanzishwa kwa Al Jamiatul Islamiyya, Kleist alikuwa mwanakamati wa Kamati ya Maulidi ya Dar es Salaam.
Kleist alikuwa mwanakamati kuanzia mwaka wa 1926 na akadumu ndani yake hadi mwaka 1940 alipojitoa kwa ajili ya matatizo yaliyozuka. Kisa hiki tutakieleza hapo baadae.
Hii ilikuwa kamati iliyowakusanya watu maarufu wa mjini.
Kazi ya kamati hii ilikuwa ni kutayarisha maulidi ya kila mwaka ya kusheherekea kuzaliwa kwake Mtume Muhammad, (Rehema na Amani Iwe Juu Yake).
Sherehe hizi zilikuwa muhimu sana hasa katika miji ya Kiislam iliyoko pwani kama, Lamu, Mombasa, Tanga, Pangani, Mikindani, Kilwa, Mtwara na Lindi.
Waislam kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ya Mashariki kuanzia Barawa, Somalia walialikana katika miji hii ya Kiislam kuja kusheherekea kuzaliwa kwa Mtume.
Kleist kwa sababu ya kipaji chake katika uongozi alichaguliwa kuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya.
Alikuwa na ujuzi ambao uliwa hasa mahali pake katika shughuli za kuendesha ofisi.
Alikuwa anajua kupiga chapa, hati mkato, alikuwa kijua kuzungumza Kiingereza na alikuwa tayari ndiye katibu wa African Association, akikiongoza chama kwa ufanisi wa hali ya juu kabisa.
Al Jamiatul Islamiyya hawakuwa na haja ya kuhangaika kumtafuta katibu, walimchagua Kleist kushika nafasi hiyo.
Shariff Salim Omar, Liwali wa Dar es Salaam akachaguliwa kuwa rais wa Al Jamiatul Islamiyya.
Wanachama wengine wa Al Jamiatul Islamiyya walikuwa Ali Jumbe Kiro aliyekuwa Mweka Hazina, Maalim Popo Saleh, Idd Tosiri na Mzee bin Sudi.
(Kutoka kitabu cha Abdulwahid Sykes)