Na. M. M. Mwanakijiji
Tunajaribu kuaminishwa kuwa tunahitaji maridhiano. Kwamba, tumekosana kiasi kwamba ili tuweze kupatana ni lazima tukae chini na kukubaliana kupatana. Manabii uchwara wa maridhiano wanataka taifa zima lipige magoti na kuanza kufukiza ubani kwenye madhabahu waliyoitengeneza wao; madhabahu yenye unyevu wa damu. Tatizo kubwa ambalo wajumbe na mabalozi hawa wa ulaghai hawataki kulisema ni kitu gani wao wametukosea sisi, au wamewakosea wengine.
Kutwa kucha, wanaimba wimbo wa ulazima wa maridhiano lakini hawako tayari kusema sisi tumewakosea nini wao. Na kama kinachozungumzwa ni CHADEMA NA CCM ni lazima ijulikane wazi kuwa hawa watu walikosana nini hasa hadi waitane kwenye kile kinachoitwa "meza ya mazungumzo" au kama ninavyoiona mimi - meza ya kusalimu amri. Kama CCM na CHADEMA ndio waliokosana kama inavyodaiwa kutokea Zanzibar kati ya CCM na ACT-Wazalendo basi wawe wa kweli kwanza.
CHADEMA imeikosea nini CCM? Kama mifano mbalimbali iliyokuwa inatolewa kwenye kesi ya Tundu Lissu na viongozi wenzake unaweza kuamini kabisa kuwa kuna uovu mkubwa sana umefanywa na CHADEMA. Yaani, inawezekana kabisa wanasiasa kutoka CHADEMA hawatakiwi kutoa mawazo, kujenga hoja, kupinga serikali au kuwa na misimamo tofauti na ile ya Chama tawala. Lakini, wanapotaka maridhiano ni lazima tuwaulize - kwani CHADEMA Iimewakosea nini nyinyi CCM?
Leo hii mwenyekiti wa CHADEMA yuko mahakamani kwa tuhuma za kudai wataenda 'kukijambisha' kwenye uchaguzi mkuu. Kwamba, kauli hizi za 'kukinukisha' inaweza kuwa ni uhaini. Kana kwamba ni makosa kuwafanya watu waichukie CCM na watake kuitoa madarakani. Imefika mahali kuna watu wanaamini kabisa kuwaza, kupanga na kufanya mikakati ya kisiasa ya kuitoa CCM madarakani ni makosa na ni uhaini. Kwamba, taifa zime tunatakiwa tukubali kuwa CCM ndio mtawala wetu wa milele na hisia yoyote ya kuichukia na kutaka kuitoa madarakani ni sawasawa na kutenda dhambi fulani ambayo watu wanatakiwa kuungama na kufikia toba!!
Na kama ni kinyume chake ni lazima tuulize; wao CCM wameikosea nini CHADEMA? Hili labda haliwezi kuwa na mjadala mkubwa kwa sababu CHADEMA wanaweza kuorodhesha vitu 100 ambavyo wamekuwa wakitendewa na serikali ya Chama cha Mapinduzi kiasi kwamba labda ni CCM ndio inahitaji kuwapigia CHADEMA magoti na kuomba maridhiano.
Lakini, kama maridhiano haya si ya vyama vya siasa bali kati ya wananchi na watawala wao ni wazi kubwa maswali yale yale lazima yaulizwe. Kwani wananchi wameikosea nini CCM? Matukio ya Oktoba 29 na mauaji yaliyofanyika baadaye ni makosa makubwa ambayo Watanzania wamewafanyia watawala wetu? Je, vijana kuandamana na kutaka kuidai nchi yao na kukataa mfumo mbovu wa uchaguzi ni dhambi dhidi ya CCM kiasi cha mamia kati yao kuuawa na mtu yeyote asiwajibishwe hadi leo?
Kwenye taifa na mazingira ambayo watu wanaishi katika hali ya kuviziana inawezekana vipi watu wakaridhiana? Leo hii mtu akisimamishwa na polisi hata kama anaulizwa nyumbani kwa Katibu Kata watu watakodoa macho kwa sababu hawajui litaishaje. Leo, hii unasikia polisi wameuawa au wamekufa watu hawana tena "wapumzike kwa amani" badala yake watu wanagongeana bia!! Watu tumekaa kuviziana na kuogopana! Kuna maneno sasa hivi watu hawatakiwi kuyasema hadharani na wakawa salama!
Wale wanaoitwa "viongozi" pamoja na vimulimuli na ving'ora vyao ni wazi kuwa wanajua hawako salama. Watu wamejipanga mstari na kuimba mapambio na qasida ili wasionekane wabaya au wenye mbinu mbaya. Huko ndani wanaviziana na kuogopana na wameshajifunza kwa yaliyomkuta Ndugai na Nchimbi; hakuna aliyesalama kati yao. Huko upinzani na wenyewe wanaogopana na kuviziana - ya Lema na Heche yanatukumbusha yalikoanzia ya kina Kaborou na Zitto! Upinzani bila migogoro ya ndani hauwezekani kama vile CCM bila makundi haiwezekani!
Ndiposa, swali lazima liulizwe - kwenye mazingira ya maviziano, maridhiano yanawezekana vipi? Kwenye siasa za kunyemeleana, kuelewana kutatokea vipi? Jibu langu ni rahisi - haiwezekani hadi mmoja ashindwe kwenye uchaguzi kihalali kabisa - ndipo maridhiano ya kweli yanaweza kutokea. Nje ya hapo, ni kusumbua ubongo wetu kama taifa!!! Hamtaki?