JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Maxence Melo ambaye ni Mkurugenzi wa JamiiForums, jana Aprili 25, 2022 alikuwa katika kituo cha E FM Radio akielezea mambo mbalimbali kuhusu taasisi yake, harakati, mijadala na mambo mengine mengi.
Hizi ni sehemu ya nukuu ya yale aliyozungumza Maxence Melo:
“Hitaji la Jamii Forums wakati inaanzishwa lilikuwa ni kutengeneza kitu ambacho kingeweza kufanya wananchi nao wapate kufunguka, waelezee hisia zao, isiwe wao tu kupokea habari/taarifa, yaani kuhabarishwa kama inavyoainishwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri.
“Miaka hiyo kulikuwa na kundi kubwa la vijana ambao walikuwa wakiambiwa ‘vijana ni taifa la kesho’. Matukio kama ya ufisadi yalikuwa yakitokea. Ubinafsishaji ulikuwa umepita na mali za umma zikachukuliwa na watu binafsi”
Niliacha kazi mwaka 2010
“Mwaka 2010 niliamua kuacha kazi niliyokuwa nimeajiriwa na inanilipa vizuri ili nisimamie mtandao, na wakati huo hatukuwa tunaingiza kipato chochote hadi miaka miwili baadaye.
Jamii Forums itaenda kwenye Nchi 8 tofauti
“Sehemu ya mpango mkakati wa Jamii Forums ni kuwa tumepanga kwenda kwenye nchi nane tofauti kuanzia mwaka huu (2022).
Nilipelekwa Keko nikipigania haki ya faragha
Wiki moja baada ya uchaguzi wa mwaka 2015, tulianza kupata barua kutoka Polisi wakisema wanahitaji taarifa za wanachama wetu, baadaye tukawa tunaata barua kutoka sehemu mbalimbali zote zikihitaji taarifa za wateja wetu.
“Japo barua zilikuwa zikionekana zina mwandiko wa aina moja lakini zilikuwa zikitoka sehemu tofauti. Tulivyoona barua zimezidi tukaenda Mahakama Kuu kwa kuwa tuliona tunakoenda itakuwa ni kuvunjwa sheria ya nchi.
“….Ilifika siku ya siku nikapigiwa simu na mtu ambaye kwa sasa siwezi kumtaja kwa kuwa ana cheo sana, alinikiambia NAKUHITAJI, UTAKE USITAKE UTAKUJA NA TUTAKUFANYA CHOCHOTE, nikamwambia ninakuja.
“Nilienda na Mwanasheria ambaye walimwambia aondoke, nikakaa sentro kwa muda mrefu, baadaye nikaenda Keko, lakini tulichokuwa tukipigania ni haki ya faragha.
Nimeshasamehe walionifanyia ubaya
“Nilipelekwa Mahakamani nikanyimwa dhamana, nikapelekwa Keko kwa muda, kila wiki nikawa nipo Mahakamani, baadaye nilitoka kwa dhamana, nikawekewa masharti magumu, sikutakiwa kutoka nje ya Dar bila kibali, hata nilipofiwa Bukoba sikuruhusiwa kwenda.
“Nilipoteza marafiki wengi, wapo waliokuwa wanaamini napambana na Serikali kitu ambacho hakikuwa kweli, pamoja na yote nimeshasamehe.
“Hukumu ilitoka na Hakimu akasema haoni kesi. Baadaye nilipata kesi nyingine ambayo niliikatia rufaa kwa kuwa ilinitaka nilipe Sh milioni tano au kwenda jela….
Taarifa za mtu ni utu wake
“…Nilipopata kesi kuna hakimu aliwahi kuniita Mahakamani na kuniuliza “Max kwanini upo Mahakamani?” aliuliza hivyo kwa kuwa licha ya yeye kuwa hakimu na anasikiliza kesi lakini alikuwa hajui kwa nini nipo pale yaani hakuelewa aina ya kesi zangu.
“Hakimu mwingine akaniambia kwani nikiwapa hao Polisi hizo taarifa za watu wanazohtaji nitapungukiwa nini?
“Unajua suala la faragha ni jambo ambalo wengi hawaelewi, data za mtu ni utu wa mtu, ukizitoa hivihivi kwa kuwa kuna mtu amehitaji ni kitu ambacho kinaweza kuutoa utu wako.”
Tanzania hakuna sheria ya ulinzi
“Simu yako na mitandao inakujua kuliko mpenzi wako, inakujua kuliko mtu mwingine yeyote, taarifa zako zikifika kwa watu wengine inaweza kuharibu maisha yako.
“Kwa sasa hivi lazima uwepo utaratibu wa kisheria (kuhusu ulinzi wa taarifa za watu), isiwe ilimradi watu wameamua kuongea tu.
“Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 16 ambayo imeagiza mamlaka ya nchi kutunga utaratibu, mpaka sasa hakuna utaratibu huo.
“Hatuna sheria za kulinda faragha za watu na data za watu zikichukuliwa zinatumikeje, hatuna Sheria ya Personal Data Protection kwa Tanzania.
“Kulikuwa na muswada mwaka 2014 (kuhusu ulinzi wa data), mpaka leo bado ni muswada.
Nampongeza Rais Samia, sheria ipo njiani
“Nampongeza Rais Samia kwa kuwa ameonesha dhamira ya dhati kuhakikisha sheria hiyo inatungwa, nampongeza Magufuli na hata CCM kwa kuweka wazi kuwa kufikia mwaka 2025 kuwe na sheria hiyo tayari.
“Nasema hiyo kwa kuwa CCM waliiweka kwenye ilani yao suala hilo la ulinzi wa data za watu kwenye ilani yao.”
Tunapeleka Muswada wa Sheria kwa Serikali
“Jamii Forums kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Tanzania Bara na Visiwani, tumetengeneza muswada wa mfano na tunaenda kuikabidhi Serikali kuwa sisi tunapendekeza hivi.
“Taarifa za watu ziwe na utaratibu maalum, zikichukuliwa zinakwenda wapi na zinatumika kwa njia gani, sheria inatakiwa kueleza taarifa zinaweza kuchukuliwa na mtu au watu kwa matumizi yapi na watazitumia kwa muda gani…
Tuna sheria mbovu ya makosa ya mtandao
“Tuna sheria ya makosa ya mtandao ambayo ni mbovu, sheria inataja ‘kwa kudhamiria’, nani ambaye anaipima dhamira? Sheria hiyo inaua ubunifu hasa kwa vijana.
“Ni wachache sana ambao wanaweza kusoma sheria kwa ajili ya kujilinda kabla hawajaanza harakati zao. Kuisoma sheria siyo kitu rahisi.
“Sisi Jamii Forums tumeshirikiana na wadau wengi na kukusanya maoni ya wadau zaidi ya 500 mapendekezo ya sheria mbalimbali. Tunaamini yatafanyiwa kazi.
“Tumeona Serikali imeonesha nia ya kweli ya kufanya mabadiliko ya sheria na pia nalipongeza Jeshi la Polisi kwa kupunguza kamata kamata.
Huwezi kuzuia mitandao
“Ukitumia sheria sana kuthibiti (watu mitandaoni) unaweza kufanikiwa kwa watu wa ndani lakini wale wa nje watafanya.
“Kuna makosa ambayo wakifanya watu wa nje hata majirani hakuna cha kuwafanya, lakini vijana wa ndani ya nchi wakifanya wanaona hawawezi kupiga hatua. Hauwezi kuzuia mitandao.
“Ukipambana na teknolojia itakuumbua, hata ikitokea mambo ya ‘tunazima internet’ haitasaidia, tunakoeleka utamiliki simu bila kuwa na line ya simu.
Sikubaliani na YouTube kuwa TV
“Kanuni kuhusu YouTube ni TV sikubaliani nayo, naipinga, nafikiri tuheshimu taaluma ya habari, tunaharibu maana nzima ya TV, naamini hata YouTube wenyewe hawajui kuwa wao ni TV.”
Tumepokelewa mataifa mengine
“Jamii Forums tutakwenda mataifa mengine, wapo ambao tumeshazungumza nao, tumekaribishwa, wengine hawajatukaribisha lakini tutaenda.”
“Tumeshaanza kuandaa watu kwenye mataifa mengine kuanzia mwaka 2020 ili waelewe taifa lao, huu mwaka 2022 tumeona ni mwaka sahihi wa kufika huko kwenye nchi nyingine. Hata kama itatokea wametuzuia kwa maana ya mamlaka sisi tutaingia kwa njia nyingine, siwezi kueleza hapa mikakati yetu lakini tutakuwepo huko kwenye mataifa mengine tunakotaka kwenda.
Tuna haki ya kuhoji
"Kazi yetu sisi ni kukumbushia siyo kuchukua hatua, tuna haki ya kuhoji kwa nini hatua hazichukuliwa, najua kuna gharamza za kulipa kwa kazi hiyo. Hatutakiwi kuchekacheka na wanaokula mali ya umma.
"Vyama vyote vya kisiasa vinavyopata ruzuku ni mali yetu sisi wananchi, tuna haki ya kuhoji, ndio maana Ripoti ya CAG ni haki yetu kuuliza imefanyiwaje kazi.
Watatokea kutuminya wakati wa uchaguzi
"Kuhusu matumizi ya mitandao nitoe mfano, Jamii Forums tuna washiriki wengi wakiume, takwimu zinaonesha wengi wao ni wenye umri wa miaka 18 hadi 44.
“Mwaka 2025 tunatarajia kuwa na watumiaji wa digitali zaidi ya milioni 50. Tunajua ikifika muda huo wapo waadui watatokea kutaka kutuminya, hiyo ni popote duniani wakati wa uchaguzi.
Wanawake wanafanyiwa ukatili, watu wanacheka
"Ukuaji wa digitali unaenda kwa kasi lakini kuna makosa mengi ya kimtandao ambayo yanawalenga wanawake na tunayaona ni ya kawaida, unaweza kuwa unacheka kumbe unafanya kosa.
"Mfano unaweza kusikia kuna connection, utafurahia lakini jua unafanya kosa, mfano angekuwa mama yako au dada yako? Tunashiriki dhambi ya kumuonea mtoto wa kike. Tuwahamishe washiriki tusitumie nafasi hiyo kuwadhalilisha"
Bilionea wa Tanzania atatokana na Digitali
“Bilionea mkubwa Tanzania ndani ya miaka mitano hadi kumi ijayo atatokana na digitali.
Gharama zetu ni ndogo
“Inawezekana watu hawatanielewa, Tanzania tuna gharama ndogo za bando, lakini je wanachokipata kama GB ndiyo kile kinachotakiwa hilo ni jambo lingine."
Source: EFM