Mbeya: Baadhi ya Mifumo ya utoaji huduma kwa viziwi inakiuka Sheria za nchi na Mikataba ya Kimataifa

Mbeya: Baadhi ya Mifumo ya utoaji huduma kwa viziwi inakiuka Sheria za nchi na Mikataba ya Kimataifa

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
Katika makala iliyopita, tuliona ukubwa wa tatizo la ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama katika vituo vya matibabu katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Katika mfululizo wa makala hii, leo tutaangazia kiini cha mgogoro huu wa kibinadamu na kisheria.

Sehemu ya kwanza ~ Mbeya: Wenye changamoto ya kusikia wanapitia wakati mgumu katika Vituo vya Afya

Wakati Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ikionyesha Mkoa wa Mbeya unaviziwi 12,000 na Halmashauri ya Jiji la Mbeya pekee inaviziwi 3,800, ukweli ni kwamba mifumo ya utoaji huduma inakiuka sheria za nchi na mikataba ya kimataifa.

Kisheria, Kifungu cha 5(1) na (3) cha Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2010 kinapinga marufuku ubaguzi wa aina yoyote na kuagiza mamlaka kutoa huduma kwa kuzingatia mahitaji maalum ya makundi haya. Hata hivyo, uhalisia huo uko kimya kabisa, na matakwa ya Sera ya Afya ya Mwaka 2007, Ibara ya 5.3.5 inayotaka kuwepo kwa huduma jumuishi.

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, anasema wazi kuwa hakuna mpango mkakati madhubuti uliowekwa kutekeleza sheria hiyo.

Nguzo ya pili ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 inasisitiza kuhusu huduma jumuishi ambapo taifa litahakikisha huduma za afya na elimu zinapatikana kwa wote. Lakini kwa nini sheria hizi hazitekelezwi?

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Aika Temu, anataja kikwazo cha mfumo katika utoaji wa huduma:

Aika Temu: "Kusiana na swala la wakalimani wa lugha za alama, hasa kwa kundi la watu wenye ulemavu wa uziwi au tuseme viziwi, kwa mkoa wetu bado of course ni changamoto. Tunao wakalimani ambao tumekuwa tukifanya nao kazi, hasa tunapokuwa tunawahitaji. Lakini tunaona bado kuna changamoto ya uwepo wa hawa wakalimani katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya.

"Ni kweli wanahitajika kwa sababu kundi la viziwi ni kubwa. Na kwa mfano, hata sio tu katika vituo vya kutolea huduma za afya, pia hata katika taasisi mbalimbali, kwa sababu na wenyewe ni kundi la watu ambao wanahitaji huduma kutoka kwenye taasisi mbalimbali. Kwa hiyo, tumekuwa tukiendelea kuwatumia hawa wakalimani pale inapohitajika.

"Tunaona umuhimu wa wao pia kuwa sehemu ya ajira kwenye serikali. Kwa hiyo, tunaisi serikali pia kuona umuhimu wa kuwa na ikama of course ya hawa watu wakalimani wa lugha za alama kwenye taasisi mbalimbali ili hawa viziwi waweze kupata huduma stahiki moja kwa moja."


Tatizo hili linavunja pia misingi ya mikataba ya kimataifa ya haki za watu wenye ulemavu (UNCRPD) katika Kifungu chake cha 25 kinachowagiza nchi wanachama kuwapachia watu wenye ulemavu huduma za afya za kiwango sawa na wengine, zikiwemo huduma za mawasiliano zinazotakiwa mahali pa kutolea huduma za matibabu.

Faraji Mbuilwa, mkalimani wa lugha ya alama kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, anaongeza kuwa upungufu huu unachangiwa na uchache wa vyuo vya ufundi nchini.
20260416_123224.jpg
Faraji Mbuilwa: "Wakalimani wako wachache kutokana na taaluma yenyewe. Taaluma hii dada ni ngumu kidogo, lakini licha ya ugumu, kundi lenyewe ambalo tunalijudumia pia lina changamoto. Kwa hiyo unahitaji uwe na moyo wa hali ya juu sana ili uweze kufanya kazi. Na kwa bahati mbaya sana sisi lugha tunayotumia, tunatumia lugha ya mikono.

Sign language ni mikono. Kwa hiyo, watu wengi wanapractise, lakini kuja kufanya ile kazi yenyewe inakuwa ni ngumu. Ndio maana hapa Mbeya ukienda sasa hivi, ukienda mpo polisi, vituo vya afya, hakuna mkalimani.

Ukienda vituo vingine vyote vya afya, hakuna mkalimani. Ukienda mahakamani, hakuna mkalimani. Ukienda kokote kwenye huduma muhimu ambazo hawa kama binadamu wa kawaida wanatakiwa kuzipata, kuna uchache sana wa wakalimani. Lakini la pili, fursa.

Wakalimani wengi unakuta hata ngesoma, wakati mwingine watu wanaifanya hii kama ni huduma ya bure. Sasa unakuta mtu ni binadamu, anahitaji awe na mahitaji, afanye kazi, lakini pili aweze kuishi.

Jambo la tatu, vyuo vilivyoko Tanzania ni vichache sana vinavyofundisha lugha ya alama. Kwa hiyo mpaka kumpata mtu aende chuo na amalize, afanye, na kwa bahati mbaya kozi hii ni ya muda mrefu sana. Ili uweze kuwa mahiri, ni lazima uwe umefanya na umesoma kwa muda mrefu."

Kwa upande wake, Aneti Isaya, Mkurugenzi wa Shirika la Wajasiriamali Wanawake Viziwi Tanzania, ambaye ni mlemavu wa kusikia akiongozwa na mkalimani wa lugha ya alama Namaani Gideon, anasema taaluma ya ukalimani haijatambuliwa kama taaluma rasmi, ndio maana vijana wengi hawajaona fursa hiyo.

Aneti Isaya: "Anazungumzia kuhusu uchache wa wakalimani katika sekta ya afya, kwa nini? Sababu kuu ni ukosefu wa mifumo rasmi ya mafunzo na vyeti vinavyotambulika kitaifa katika ukalimani wa afya. Taaluma hii bado haijatambuliwa vya kutosha kama ajira rasmi nchini. Hivyo vijana wengi hawaoni kama fursa ya kazi. Uelewa mdogo wa umuhimu wa huduma za ukalimani katika afya unachangia kupunguza uelewaji katika sekta hii."

Hoja kuhusu ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika mipango ya maendeleo imewahi pia kujitokeza ndani ya Bunge. Mwaka 2026, Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha watu wenye ulemavu, Nasria Nassir Ali, alichangia mjadala wa Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Muda Mrefu katika Kikao cha Nane cha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13. Katika mchango wake, Mbunge huyo alitumia lugha ya alama akifikisha hoja zake Bungeni, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanazingatiwa katika mipango ya maendeleo ya taifa.

Nasria Nassir Ali: "Mheshimiwa Nasria Nassir Ali atafuatiwa na Mheshimiwa Josephine Joseph Gekacha. Mheshimiwa Mwenyekiti, awali yote kama nilivyosema, nashukuru kwa fursa ambayo umenipa. Lakini pia namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kuwepo mahali hapa siku ya leo. Kwa anza kabisa, niipongeze serikali kwa jitihada kubwa sana katika kuboresha miundombinu.

"Naomba niongeze kidogo, niombe serikali iboreshe zaidi miundombinu. Kwenye vituo vya afya kuwe na wakalimani. Ikitokea mtu ambaye ni kiziwi anaumwa, kawaida binafsi huwa sipendi kutumia mkalimani kwa sababu ya usiri wa changamoto zangu za kiafya. Kwa hiyo, pendekezo langu ningeomba pia watoa huduma wa afya wapewe mafunzo ya lugha ya alama ili kuweza kurahisisha mawasiliano na kuwa na usiri."

Mwanasheria kutoka Shirika la Msaada wa Kisheria la TAWLA, James Sambuka, anahitimisha kwa kusisitiza kuwa udhaifu wa kiutawala hauwezi kuhalalisha ukiukaji wa haki za kisheria za wananchi.

James Sambuka: "Utaratibu umewekwa vizuri wa kuwawezesha hawa watu wenye ulemavu kuweza ku-access hizo huduma mbalimbali. Lakini changamoto inapokuja ni kwenye upande wa utekelezaji. Inaonyesha kabisa sheria inasema inasema hivi, serikali bado haijaweka mfumo rasmi wa hawa watu au wakalimani kuwa na ajira rasmi. Kwamba wakimaliza kusoma waende wakaajiriwe serikalini, labda kwenye sekta za afya, mahakama na nini, ndio maana unakuta kuna upungufu wa watu au wakalimani."

Sheria zipo, lakini zimesimama kwenye makaratasi. Katika makala wetu ya tatu na ya mwisho, tutaangazia masuluhisho ya kimkakati yakayovunja ukimya huu.

Pia soma ~ Taasisi na Serikali ziwekeze katika mafunzo ya watoa huduma kwa wenye changamoto ya kusikia

Andiko la: Mwanaisha Makumbuli
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 

Attachments

Back
Top Bottom