Mphamvu
JF-Expert Member
- Jan 28, 2011
- 10,702
- 3,319
KOCHA wa Mbeya City, Juma Mwambusi alimaliza mkataba wake wa kuifundisha timu hiyo lakini kumekuwepo na siri kubwa juu ya hatima yake ndani ya kikosi hicho ingawa viongozi wa timu hiyo wanadai kuwa bado ni mwajiriwa wao.
Leo Katibu Mkuu wa City, Emmanuel Kimbe alishindwa kutoa ufafanuzi wa hatima ya Mwambusi huku akisistiza kuwa makubaliano ya mkataba mpya ni siri yao na kocha huyo ingawa taarifa za ndani kutoka City zimeeleza kuwa bado hawajafikia makubaliano ya mkataba mpya.
Mbali ya hilo, Kimbe alisema kuwa hawana presha na Ligi Kuu msimu ujao kwani wanaamini kikosi chao kipo vizuri na usajii wanaufanya unazingatia mahitaji ya timu na mapendekezo ya benchi la ufundi huku akisistiza kuwa kuondoka kwa nyota wao si tatizo ndani ya City.
"Mwambusi bado ni kocha wetu, atumie mkataba wa zamani au mpya hilo ni siri yetu baina ya pande mbili, mwajiri na mwajiriwa, kasi ndani ya timu haijapungua na tutawashangaza mashabiki wa soka msimu ujao, watarajie kuona majina ambayo ni mageni lakini kazi yao ni kubwa.
"Tangu msimu umalizike hatujaondokewa na wachezaji wengi, na haitupi shida kwani tunasajili wengine ambao pia ni bora na wanafaa kuichezea timu yetu, wapo pia wachezaji kutoka timu ya vijana tutawapandisha," alisema Kimbe.
Ingawa Kimbe anasema timu yao imeondokewa na wachezaji wachache lakini mpaka sasa BOIPLUS inafahamu kuwa wachezaji zaidi ya 10 wametimka ambao ni Deus Kaseke, Peter Mwalyanzi, Peter Mapunda, Paul Nonga, Saady Kipanga, Anthony Matogolo, Cosmas Fredy, Ramadhan Abdul, Idrisa Rashid, Deo Julius, David Burhan na Lambon Ashery.
Chanzo: BoiPlus Blog