SoC03 Mbinu shirikishi kuinua kiwango cha uwajibikaji nchini Tanzania

SoC03 Mbinu shirikishi kuinua kiwango cha uwajibikaji nchini Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

tpaul

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2008
Posts
24,225
Reaction score
22,632
Ukilinganisha na watu kutoka mataifa mengine ya Afrika Mashariki na Kati, watanzania sio wavivu kama inavyodhaniwa. Kinachokosekana tu ni mpango madhubuti na endelevu wa kuhimiza uwajibikaji miongoni mwao.

Baada ya kufanya utafiti wangu kimyakimya, nimegundua kuna jambo dogo tu linaloksekana kuunganisha nguvukazi ya watanzania inayopotea bila kutumika. Hili ni kama bomba la maji linalovuja. Idara ya maji wasipoliziba, maji yatapotelea njiani bila kuwafikia watumiaji.

Mara nyingi ukipita mitaani, hata nyakati za asubuhi, utakuta vijana na baadhi ya watu wazima wamekaa vijiweni kiubwete wakinywa kahawa na kupiga soga ambazo hazina tija kwa mendeleo ya taifa. Katika makundi hayo kuna mengine yanajadili mambo ya mpira, hasa kuhusu timu za Simba na Yanga na baadhi ya timu za Uingereza. Aghalabu, utawasikia wakiongelea mambo ya maendeleo ya taifa au mipango mkakati ya mtu mmoja mmoja kujiletea maendeleo. Nguvu kazi hii inayopotea bure ikunganishwa na serikali kufanya kazi zenye tija na zenye kuingiza kipato, taifa hili litapiga hatua kubwa za maendeleo ndani ya muda mfupi sana.

Ukitembelea nchi za Ulaya na Marekani ni nadra kuwakuta watu wamekaa kwenye makundi wakijadili mambo yasiyokuwa na tija kwa maendeleo yao na mataifa yao. Hata suala la ulevi lipo chini sana kwenye nchi hizo ijapokuwa nyingi zipo ukanda wa baridi ambapo tungetegemea kuwaona wakinywa pombe kali kupasha miili joto. Badala yake viwanda vyao hutengeneza pombe hizo na kuzisafirisha kuja Afrika kunywewa na vijana wetu, kitendo kinachochangia kuangamiza nguvu kazi na kudidimiza uchumi wa taifa.

Nimeanza kujenga hoja kwa kuonyesha udhaifu ulipo ili nitakapotoa mbinu zitakazowezesha kuongeza uwajibikaji miongoni mwa hii nguvukazi inayopea bure tuelewane vizuri. Ni rahisi. Serikali ipo kila mahali. Na lengo la serikali yoyote ile ni kuboresha maisha na ustawi wa raia.

Ikiwa raia wapo na wana uwezo wa kufanya kazi kujenga taifa lao lakini hawafanyi hivyo kwa hiyari yao yenyewe, serikli inao wajibu wa kuwapanga na kuwatumia kuzalisha mali itakayoinua uchumi wa taifa. Katika hatua za mwanzo wanaweza wakaona labda serikali inawapangia cha kufanya lakini kadri muda utakavyoenda na matunda kuonekana, watarudi kuja kuishukuru serikali kwa mkakati huo madhubuti.

Kwa kuwa serikali imekita mizizi yake kutoka Ikulu ya Chamwino hadi kijijini Mtakuja, ni suala tu la kujipanga na kuiweka vizuri nguvu kazi kwa kutumia nguvu kidogo tu. Zoezi hili litaanzia ngazi ya mtaa au kijiji. Kwenye mtaa au kijiji, kuna watendaji wa mitaa/vijiji, na vitongoji, wajumbe wa serikali za mtaa, wenyeviti wa serikali za mtaa na mabalozi wa nyumba 10.

Kila balozi atapewa jukumu la kufanya sensa ya nguvukazi kwenye eneo lake na kuiwasilisha kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa au kitongoji. Kisha hawa viongozi watawasilisha orodha hiyo kwa mtendaji wa mtaa. Na watendaji wa mitaa watawasilisha orodha hiyo kwa mtendaji wa Kata atakayechambua orodha ya nguvukazi ambayo haishiriki kazi yoyote badala yake wanazurura tu na kupiga soga au kufanya uhalifu mitaani.

Kwa upande wa mijini zoezi hili litahitaji nguvu kubwa kwa sababu ya uwepo wa mateja, wapiga debe, wacheza kamari, ombaomba wanaozurura ovyo na magenge mengine yasiyoeleweka.

1685560006781.png

Vijana wakicheza kamari ya karata (Chanzo: mtandao)

Orodha ya nguvukazi zembe ikishafika kwa mtendaji wa Kata, ataitisha kikao na watu hao na kuwahoji mmoja mmoja ili kujua changamoto zinazowakabili hadi wasishiriki kazi za ujenzi wa taifa. Nafahamu wengi watasema wanakosa mitaji au mashamba ya kulima kujipatia kipato binafsi au familia. Na wengine ni ile tu hurka ya kutega kufanya kazi. Baadhi ya vijana waliorundikana mijini wamekimbia vijijini na kuwaacha wazee wanahangaika na shughuli za kilimo peke yao. Hawana kilema chochote ila tu hawataki kufanya kazi. Hawa ndio wa kuanza nao.

Kwa nguvu kazi ya mjini, ambayo baadhi ya watu wanapenda kuwapachika jina la wazururaji, hawa wachukuliwe na kufanya kazi za umma kama vile kufagia barabara, kuzibua mitaro, kutengeneza bustani, n.k. Kwa mfano, ukitembelea bustani za mjini wakati wote zimejaa watu wasiokuwa na kazi maalumu wanaoishinda na kulala huko bustanini wakizichafua kwa mkojo, kinyesi na vipande vya sigara/bangi.

Iwe ni lazima kabla ya watu hawa kukaa kwenye bustani hizi kwanza wazifanyie usafi. Awepo mtu maalumu kwenye maeneo hayo atakayekuwa anatunza vifaa vya usafi kwa ajili hiyo. Mtu akiingia hapo bustanini kwanza anapewa kipande anasafisha au kupanda maua halafu ndio anakaa kupunga upepo au kupiga soga.

Kazi zipo nyingi ambazo halmashauri za miji, manispaa na majiji wanaweza kubuni ili kuhakikisha nguvu kazi haipotei bure bali inawajibika kujenga uchumi wa nchi.

Nguvukazi sehemu za vijinini na katika miji midogo inaweza pia ikatumika kufanya baadhi ya kazi zinazofanana na za mjini. Kama eneo lipo kijijini, wanaweza kufanya usafi kwenye mashule, zahanati na taasisi nyingine za serikali, kupanda miti na kazi nyingine kadri watendaji wa maeneo hayo watakavyoona inafaa.

Mtu anaweza kujiuliza: bajeti ya kuwalipa hii nguvukazi itatoka wapi? Fedha zipo. Chanzo kimojawapo cha fedha ni halmashauri. Katika halmashauri kuna kiasi cha 10% ya fedha inayotengwa kila mwaka kwa ajili ya vijana. Kama njia ya kupanua wigo wa ajira kwa vijana, 2% ya fedha hizi inatosha kabisa kuwalipa bila tatizo lolote. Ni utashi tu wa serikali kurekebisha sheria inayoongoza mgawanyo wa hizi fedha ili 2% iingie kwenye malipo ya nguvukazi.

Chanzo kingine ni fedha za mfuko wa jimbo. Fedha hizi ni kwa ajili ya kuliendeleza jimbo bila ubaguzi. Hawa vijana wasio na kazi lakini wana nguvu za kufanya kazi watengewe kiasi fulani cha hizi fedha na kulipwa kama posho kwa kazi watakazozifanya.

Lakini pia serikali italazimika kutenga kiasi cha fedha kwenye bajeti yake (Underused Manpower Fund) na kukitumia kwenye halmashauri kwa ajili ya kulipa posho za nguvu kazi.

Kadri muda utakavyoenda wanaweza pia wakajitokeza wafadhii, AZAKI au wapenda maendeleo wengine wakaandika machapisho kwa wafadhili zikapatikana fedha nyingi kuwalipa hawa vijana.

Lengo kuu la ubunifu huu ni kuongeza uwajibikaji miongoni mwa watanzania, hasa wale wenye uwezo wa kufanya kazi lakini hawana mahali pa kutumia nguvu zao kulijenga taifa.

Kazi ya serikali kuu na serikali za mikoa na wilaya itakuwa kuratibu zoezi zima kwa kuweka mikakati kuhakikisha kuwa fedha zilizotengwa hazifujwi na mtu yeyote atakayekiuka achukuliwe hatua kali za kisheria na kinidhamu.

Nawasilisha.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom