DOKEZO Mbolea Feki tunayopewa Wakulima Tabora ni chanzo cha kifo cha zao la Tumbaku, Waziri wa Kilimo fanya jambo

DOKEZO Mbolea Feki tunayopewa Wakulima Tabora ni chanzo cha kifo cha zao la Tumbaku, Waziri wa Kilimo fanya jambo

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'

Torra Siabba

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2016
Posts
243
Reaction score
287
Hivi Waziri wa Kilimo yupo kweli? Maana sisi wakulima wa Tumbaku hapa Tabora tunapitia changamoto na taabu kubwa sana ambazo kama zisipofanyiwa kazi sisi tutaacha kulima zao hilo na Taifa litapata hasara kubwa ya kukosa fedha za kigeni kutokana zao la Tumbaku kuanguka.

Iko hivi, sisi wakulima wa zao la Tumbaku kutoka katika Wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui tumetapeliwa baada ya kupewa mbolea feki ya kupandia zao hilo la kimkakati.

Ipo hivi, mbolea feki ambayo tunaletewa inaua zao, zinapunguza ubora wa tumbaku na zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa wakulima wenyewe hii ni hatari kubwa baada ya kupewa mbolea iliyochakachuliwa.

Hazina virutubisho vya kutosha kwa ukuaji bora wa zao hilo la tumbaku jambo linalosababisha mimea kuwa dhaifu, kukosa ukuaji mzuri na kusababisha ukuaji wa tumbaku kuwa dhaifu na kupunguza uzalishaji wa zao hilo.

Kwa mantiki hiyo ni wazi kwamba kuna mamlaka zimepewa kusimamia zoezi hili la kusambaza mbolea kwa wakulima wa zao hilo lakini badala ya kusambaza hizo mbolea wao wanajinufaisha na kupeleka mbolea afeki ambazo zinasababisha uzalishaji wa zao hilo kushuka, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe tafadhali sana waangalie hawa wakulima maana wanao mchango mkubwa kwa taifa.

Hivi majuzi Waziri Bashe alinukuliwa kwenye vyombo vya habari kwenye ziara ya Makamu wa Rais aliyoifanya Tabora, akieleza ya anawafahamu wanaotorosha zao la tumbaku kutoka kwa wakulima tena mbele ya Makamu wa Rais, akaenda mbali na kusema atawataja sasa, je, intelijensia yake imeshindwa kutambua kampuni zinazoleta mbolea feki kwa wakulima na kusababisha uzalishaji wake kushuka?

Wote ni mashahidi ya kwamba Zimbabwe ndiyo nchi ya kwanza kuongoza kwa kuzalisha zao la Tumbaku kwenye Bara la Afrika ikifuatiwa na Tanzania, na Mwaka 2024 nilisikia imeweka tageti ya kuzalisha tani milioni 120, sasa kwa kitendo cha Wakulima kupewa mbolea feki tutafikia tageti hizo?

Kwahivyo Wizara ya Kilimo inayo kazi ya kufanya kwenye hili maana wakulima tulio wengi tunateseka na hasara ya kupoteza mazao yetu kisa pembejeo ambazo hazina ubora.

Kwa Tanzania ukichunguza kwa umakini huu Mkoa wa Tabora unaweza kuongoza kwa kuzalisha zao la Tumbaku tena kwa zaidi ya 80% ya zao hilo sasa kama wakulima wanaweza kuzalisha robo tatu ya zao la kibiashara kwa nchi nzima ambalo linauzwa wa dola inakuwaje tunapewa mbolea ambayo haina ubora?

Mamlaka za kilimo ziko wapi? Iko haja kwa Waziri ambaye anaishi Nzega na pia ni Mbunge wa eneo hilo aingilie kati wakulima tupewe mbolea zenye ubora kwa lengo la kuzalisha Tumbaku kwa wingi.

Suala hilo lina uhusiano mzuri na udhibiti mbovu wa kusimamia uingizwaji wa mbolea hii inachangia wingi wa mbolea feki sokoni hasa maeneo yasiyokuwa ya udhibiti wa kutosha kama Tabora kwahivyo TBS wanalojukumu la kuhakikisha mbolea hizi hazipiti hadi kutufikia sisi wakulima moja kwa moja bila wao kujua.

Sisi wakulima kupitia viongozi wetu wa vyama vya msingi kwenye mkoa huu wa Tabora tumejaribu kumuuliza Mrajisi wa Vyama vya Msingi Mkoa wa Tabora, Venance Msafiri lakini cha ajabu ni kwamba hataki kabisa kulizungumzia kwa kuogopa au kwa kulinda cheo chake, maana tumeshalalamika lakini hajachukua hatua yoyote katika kutusaidia kuhakikisha tunapata mbolea yenye virutibisho inayoweza kutusaidia kukuza tumbaku yetu.

Wakati nikiendelea kutafakari nikaongea na Mkulima Mwenzangu wakulima wa zao hilo mkazi wa Sikonge, Tabora ambaye alijitambulisha kwa jina la Mabula Ismail (sio jina lake halisi) akisema msimu huu wa kilimo unaoanza Agosti amelima hekari 20 ambapo matarajio yake ilikuwa ni kuvuna zaidi ya gunia 200 za tumbaku.

Anadai kutokana na kupewa mbolea feki ya kupandia anasema hana uhakika wa kupata hata gunia 50 katika heka zote hizo maana mbolea imenyauka na hakutegemea kupata hasara kama ambayo ameipata kwa msimu huu wa zao hilo.

Pamoja na kwamba kwa sasa Serikali imejipambanua kwa kuajiri Maafisa Ugani katika kila halmashauri kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo lakini huyu tunamuonea kwa kuwa mmoja wa Maafisa Ugani kwenye Wilaya moja Tabora alisema mbolea inakuja kwa maelekezo mpaka kwenye vyama vya msingi na kugawiwa kwa wakulima.

Hivyo basi, kama serikali inao mpango wa kukomesha mbolea feki lazima maafisa Ugani wapewe meno katika kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji wa zao hili ili mwisho Tanzania iwe nchi ya kwanza kuzaisha zao la Tumbaku kwa Afrika nzima.

Mjumbe hauawi.... Alamsiki
 
Back
Top Bottom