Lunyungu
JF-Expert Member
- Aug 7, 2006
- 8,873
- 1,906
Hii ni makala ya Padri Karugendo inayopatikana hapa: http://www.freemedia.co.tz/daima/2008/3/23/makala6.php
NI vizuri kwamba Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amejitokeza na kuelezea kwa ufasaha tuhuma zinazolenga kumtupa kwenye kapu la mafisadi.
Asingejitokeza, tungemshangaa kama tunavyowashangaa wanaonyoshewa vidole wakakaa kimya. Waraka wa Mbowe, aliousambaza kwenye vyombo vya habari unajitosheleza.
Walio wengi tumeelewa na kukubali kwamba yeye si fisadi na wala si mwizi, bali alikopa fedha NSSF, kitu ambacho ni cha kawaida. Hata kabla hajajieleza tulishabaini kwamba hizi ni njama za wajinga wachache.
Tunafahamu kwamba hizi ni njama za watu wanaotumiwa kuchafua majina ya watu kwa malipo ya vijisenti vichache. Tunafahamu kwamba hizi ni njama za watu wasioheshimu taaluma zao za uandishi wa habari.
Tulishuhudia uhuni huu wakati wa kumchagua mgombea wa urais kupitia CCM. Baadhi ya wagombea walichafuliwa na kupakwa matope.
Tunawafahamu waandishi hawa wanaoandika kwa kuweka chumvi kila habari. Ni wale walioandika kwamba Edward Lowassa, alipokewa kwa magari 400 kule Arusha, wakati alipokewa kwa magari 80.
Ni aina ya waandishi walioshindwa kuandika chochote juu ya maandamano ya vijana ya kulaani vitendo vya Richmond, yaliyofanyika siku ile Lowassa alipopokewa kishujaa nyumbani kwao.
Ndio hao hao wanaosema Mbowe, anadaiwa sh milioni 1,200, wakati yeye alikopa sh milioni 15 na amelipa zaidi ya asilimia 75. Wanaandika bila utafiti, wanaandika bila kutafakari, wanaandika ili walipwe!
Kwao pesa ndizo zinabainisha uongo na ukweli. Hawa ni aina ya waandishi wasiotambua maana ya mkopo na wizi?
Mbowe alikopa NSSF, mafisadi waliiba BoT! Ina maana hawaoni tofauti?
Ni makusudi! Ni kutaka kuandika ili walipwe! Hawa ni waandishi wa hatari.
Mauaji ya kimbali nchini Rwanda, yalichochewa kwa kiasi kikubwa na waandishi wa namna hii. Ni jambo la muhimu na la haraka kwa Watanzania kuwakataa waandishi hawa hatari.
Tuyasusie magazeti yao, maana wana nia mbaya ya kutupotosha, wana nia mbaya ya kutaka kuuficha ukweli na kuutukuza uongo. Wanachuja mbu na kummeza Ngamia!
Mbowe, aligombea urais wa taifa letu Mwaka 2005. Kampeni zilikuwa nzito, alipasua anga kwa anga na kuwa tishio kwa wale waliokuwa wakipiga kampeni nyumba kwa nyumba wakigawa vitenge na chumvi.
Kama shutuma hizi anazobambikiwa leo zingekuwa na maana yoyote, basi zingejitokeza wakati wa uchaguzi mkuu.
Mbona hakuna hata chombo cha habari kilichosema juu ya deni la NSSF wakati huo? Deni hili si la leo na wala si la 2005 ni la zamani kabisa. Mbona halikujitokeza wakati ule na badala yale linakuja kujitokeza leo wakati wapinzani wakiwa katika jukwaa wakifichua wizi mkubwa unaoendelea katika taifa letu?
Mbona linajitokeza leo baada ya Mbowe kujitokeza kwa nguvu kupinga ufisadi?
Kusema kwamba mkopo wa Mbowe unaifilisi NSSF ni kichekesho. Hata aliyeandika haya kama ni msomi, mtu makini, anayefanya utafiti na kuchambua masuala mbalimbali katika jamii yetu ni lazima ajicheke mwenyewe na kujidharau.
Kila siku tunayaona mambo makubwa ya NSSF, hawa wanajenga majumba makubwa kila sehemu ya Tanzania, kama wamefilisiwa na Mbowe wasingekuwa wanafanya chochote kile.
Hata hivyo kutokana na maelezo ya Mbowe, deni analodaiwa limelipwa zaidi ya nusu. Kama si utata uliojitokeza NSSF angekuwa amemaliza kulilipa.
Kuna watu wa kusemwa juu ya NSSF na wala si Mbowe. Kuna tunaowafahamu ambao walinunua nyumba za NSSF kwa bei ya chini na baadaye kuziuza kwa bei ya juu.
Walijua kabisa kwamba wanazinunua nyumba hizo kwa bei ya chini. Walifanya hivyo kwa kushirikiana na NSSF kwa lengo la kupata chochote kama ulivyo utamaduni wetu Watanzania wa kuiuza nchi yetu kwa vijisenti vichache.
Ni kama ilivyo mikataba yote ya taifa hili, mikataba mibovu yenye lengo la kuwanufaisha wageni na kuwakandamiza wananchi. NSSF ina kashifa zake na ufisadi mwingi, deni la Mbowe ni tone dogo kwenye bahari kubwa!
Mbali na vyombo vya habari, kuna baadhi ya vyama vya upinzani vinamshambulia Mbowe. Mwenyekiti wa SAU, anatoa ujumbe wa wazi kwamba yeye ni kibaraka wa CCM, amekuwa akifanya hivyo siku zote.
Watanzania wanafahamu, wala hana haja ya kujificha nyuma ya wapinzani. Huyu hatusumbui hata kidogo. Ni Watanzania wachache sana wanaoweza kumsikiliza na kuamini kile anachokisema.
Nimekuwa nikimheshimu sana mchungaji Mtikila. Huyu akisema watu wanasikia. Lakini nimemshangaa jinsi alivyochanganya mambo. Badala ya kumaliza upande mmoja ambao uko wazi kabisa, upande wenye ushahidi usiopingika wa ufisadi, anamgeukia Mbowe.
Inawezekana kapitiwa, maana mtu makini kama alivyo Mchungaji Mtikila, si wa kutoona tofauti kati ya mkopo na wizi. Mbowe, alikopa na hakatai kulipa. Mafisadi wameiba na bado wanajificha, eti wanarudisha fedha walizoziiba kimyakimya.
Walio wengi wameiba na kuwekeza nje ya nchi. Mbowe, amekopa na kuwekeza hapa hapa, ametengeneza ajira kwa vijana wetu, analipa kodi, ni kati ya wafanyabiashara wanaolipa kodi kwa muda na kwa uaminifu na kutoa mchango katika ujenzi wa taifa. Haiwezekani kwamba mchungaji Mtikila halioni hili!
Sitaki kuamini kwamba hizi ni propaganda za CCM, maana chama kikongwe kama CCM, hakiwezi kufanya propaganda za kijinga kama hizi. Mwana CCM aliye makini ni lazima afanye jitihada za ziada kukisafisha chama chake badala ya kutaka kufunika madhambi makubwa yaliyofanywa na wana CCM na maswahiba wake.
Mbinu za kutumia vyombo vya habari ili Watanzania wafumbe macho juu ya Richmond, EPA na mengine ni mbinu zilizopitwa na wakati.
Kama ufisadi uliojitokeza katika taifa letu ungekuwa ni wa mtu mmoja ama wawili, basi wapambe wangeweza kuufunika kwa kumpakazia Mbowe. Bahati mbaya ufisadi huu ni mkubwa sana. Ni ufisadi wa kutisha, ni ufisadi unaofunga wimbo wa nchi yetu ni masikini.
Ni ufisadi unaowaingiza watu wengi, viongozi wengi, makampuni mengi, chama tawala, Serikali na watu wengi kutoka nje ya nchi.
Ufisadi huu umeamsha hasira za wananchi. Watu wamegundua kwamba wakati viongozi wetu wanatulisha kasumba kwamba nchi yetu ni maskini, na kutulazimisha kuuimba wimbo huu usiokuwa na mwisho, wao walikuwa wakiogelea kwenye utajiri wa kutisha.
Wamekuwa wakitumia pesa za taifa letu kujitajirisha wao, familia zao na marafiki zao.
Wakati viongozi wetu wakituhimiza kujenga sekondari za kata, watoto wao si kwamba wanasoma nje ya nchi bali wanaishi maisha ya peponi, baadhi yao wamekuwa wakiruka kutoka London kwenda Cape Town Afrika Kusini kwenye sherehe za Birthday, wengine wanaendesha magari ambayo hata Wazungu hawataweza kuyaendesha.
Je, kumpakazia Mbowe, kutatoa ukweli kwamba Rostam Aziz, si Mtanzania asilia? Kwamba hakuzaliwa hapa na wala hajawahi kuomba uraia? Itaondoa ukweli kwamba mbali ya kuwa mbunge, kinyume cha sheria ameshika nafasi nyeti kwenye chama tawala?
Kwamba amekuwa akikingiwa kifua na viongozi wa juu serikalini? Serikali yetu imekuwa na msimamo mkali juu ya wahamiaji haramu kiasi cha kuwafukuza hata Watanzania wenye asili ya Rwanda na Burundi, Watanzania wenye vyeti vya uraia vinavyotambuliwa na serikali, lakini serikali hiyo hiyo inawafumbia macho wageni wanaohujumu uchumi wetu!
Mbowe hakuchota pesa kutoka NSSF, hakuiba kutoka NSSF, alikopa. Hili ni jambo la kawaida. Mafisadi wa EPA, hawakukopa, waliiba! Hawa niwezi! Wanaopitisha mikataba mibovu kwa kupokea chochote ni wezi, wanapokea rushwa. Huwezi kuwaweka hawa kapu moja na Mbowe.
IGP Mwema amewafananisha mafisadi na magaidi, amesema hawakamatiki. Hawa huwezi kuwalinganisha na Mbowe. Vinginevyo ni kumdhalilisha na kumkosea haki.
Hata kama kuna njama za kumhujumu Mbowe na wapinzani, njama hizi zimefanyika kijinga. Ni bora hawa wanaoandaa njama hizi wakatambua kwamba Tanzania ya jana na juzi si sawa na ya leo.
Watu wameanza kufumbua macho, watu wameanza kuhoji. Watu wana uwezo wa kuchambua fisadi na asiye fisadi. Leo hii watu wana uwezo wa kuchambua uongo na ukweli.
Mbowe, umesema tumekusikia, tumekuelewa na kukuamini.
Usitetereke! Endeleza mapambano hadi kieleweke!
Nipigie: +255 754 633122
Karugendo unasema ? Haya nadhani wenye masikio na waelewa wamesha elewa .Tuendelee kuwapa wapiga kura Elimu.Jambo moja ambalo washabiki na wanachama wa CCM hawajui ni kwamba Kila chombo cha habari na watanzania kwa ujumla wameichoka CCM.Ndiyo maana unaona hata Jambo watu wanasema mawazo yao wabanakia kuitwa wana Chadema ama wapinzani .No jibu ni kwamba Watanzania wamechoka sana na CCM uozo wake dawa ni CCM kutumia Vyombo vya usalama na kukakia Katiba ya Kikoloni kuwa madarakani lakini wakiweka ngoma sawa CCM wanaujua ukweli kwamnba wamesha chokwa .