CHADEMA yawasha moto
na Sitta Tumma, Mwanza
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo nchini (CHADEMA), kimesema Tanzania imegeuzwa shamba la mavuno ya mafisadi, pamoja na makampuni ya madini yanayomilikiwa na wawekezaji wageni.
Hali hiyo imetokana na baadhi ya viongozi na watendaji wakuu wa serikali kuanza kujichotea mabilioni ya fedha za umma, ikiwa ni kupitia kampuni za madini ambapo trioni 1.3, zimepotea kutokana na baadhi ya makampuni ya madini ya nje kuliibia taifa na kutokomea na fedha hizo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, wakati akihutubia maelfu ya wananchi mkoani hapa, katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu chama hicho kitangaze hadharani majina 11 ya mafisadi, Septemba 15, mwaka jana.
Mbowe ambaye alitumia muda mwingi kuzungumzia hatima ya vita dhidi ya ufisadi na maendeleo katika taifa hili, alisema makampuni hayo ya madini, yamekuwa yakitumia nafasi zake kuchota mabilioni ya fedha, huku Watanzania wenyewe wakiachwa watupu.
Huku akionyesha kukerwa na ufisadi ndani ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete, alisema katika miaka 10 iliyopita, zaidi ya sh bilioni 850 ziliibwa nchini na makampuni hayo ya kigeni.
Mbali ya hayo, zaidi ya sh bilioni 155, zilipotea miaka ya hivi karibuni, fedha ambazo zimetumika katika mradi wa Meremeta na kutokana na hali hiyo, taifa limekuwa likipoteza fedha nyingi kwa njia ya udanganyifu.
"Jamani wananchi wa Mwanza, makampuni ya madini yamekuwa yakichuma fedha nyingi na kutokomea nazo na kuliacha taifa likiwa jeupe na wananchi wake, licha ya kuwa na rasilimali nyingi," alisema Mbowe.
"Trilioni 1.3 fedha za Kitanzania zimeibwa na makampuni hayo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na zaidi ya sh bilioni 850 pia zimeibwa na makampuni ya kuchimba madini, huku tukijivuna tuna viongozi, hivi kweli tuna viongozi?" alihoji Mbowe.
Kuhusu wizi wa fedha zilizoibwa kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Mbowe alieleza kushangazwa kwake na hatua ya Rais Kikwete kushindwa kuwafikisha mahakamani wahusika waliochota fedha hizo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kuhusu ziara zinazofanywa mara kwa mara na Rais Jakaya Kikwete, Mwenyekiti huyo wa CHADEMA taifa, alieleza wazi wazi kuwa hiyo ni hali ya kujikomba na kujidhalilisha kwa Serikali ya Marekani, kwani ndiyo inayochota mabilioni ya fedha na kuwaacha Watanzania wakiwa maskini wa kutupwa.
"Yeye anaachia mali inakombwa halafu anatoka hapa kwenda Marekani kuomba msaada wakati anaowaomba msaada ndio anaowapa vibali vya kusomba mali ya taifa lake...hii ni aibu na huenda yeye rais halijui hilo.
"Kila mara safari Ulaya, kila mara safari Ulaya...mmh! Huko Ulaya kunani?...utaombaje msaada kila siku tena kwa watu wanaokuibia? Hii ni fedheha kwake na kama hajui alitambue hilo na Watanzania tunadhalilishwa pia," alisema Mbowe huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa yeye alimtaja mbunge mmoja wa CCM kuwa ndiye kinara mkubwa wa ufisadi katika fedha za EPA.
Dk. Slaa alisema, mbunge huyo ndiye kiongozi na injinia wa ufisadi, na kwamba mwaka 2005 alisajili kampuni moja ya kifisadi kisha akachota BoT sh bilioni 40 ndani ya wiki nane, fedha za umma.
"Nasema hivi, tunamfahamu kwa nyendo zake hapo Benki Kuu, akipenda aende mahakamani, lakini habari ndiyo hiyo! Na katika kampuni yake hiyo ya kifisadi alikuja kuimilikisha kwa aliyekuwa mlinzi wake.
"Kampuni hiyo ya kifisadi ilisajiliwa rasmi Septemba 29 mwaka 2005...lakini mtu huyu kwa kutaka kujivua ufisadi wake aliiandikisha kuwa ni mali ya mlinzi wake," alisema Dk. Slaa.
Aidha, alimtaka Rais Kikwete atangaze hadharani sababu za kutomhoji aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali, juu ya upotevu wa fedha hizo za EPA, alhali yeye alikuwa ni mkuu wa taasisi hiyo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alitumia muda wake kuzungumzia suala zima la madini na ufisadi ndani ya sekta hiyo.
Zitto alianza kwa kusema kuwa: "Mikataba yote ya madini haina uhalali wa kisheria, taifa linaibiwa mabilioni ya fedha huku viongozi na serikali kwa ujumla wakishindwa kudhibiti hali hiyo."
Akitolea mfano hai kwa mgodi wa Bulyanhulu, Zitto alisema awali mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na serikali chini ya TAMICO, na baadaye mgodi huo ukauzwa kwa Wazungu kutoka nchini Canada kwa dola za Marekani milioni 20.
Alisema, baada ya Wazungu hao kunufaika na mgodi huo, mwaka 1999 waliuuza kwa dola za Marekani milioni 348, na kwamba ulitumika pia kujenga mgodi wa Buzwagi ambao mkataba wake bado umezua maswali mengi kwa Watanzania.