BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 525
- 1,257
Mbunge wa Jimbo la Madaba, Dkt Joseph Kizito Mhagama ameishauri Serikali kuisaidia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) maarufu kwa jina la Benki ya Kilimo katika mtaji zaidi ili kukuza kilimo Nchini Tanzania.
Akizungumza Bungeni Jijini Dodoma amemuomba Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kutatua tatizo hilo kwa kuwa kufanya hivyo kutamaanisha kukuza kilimo Nchini.
Huyu hapa Mbunge anaelezea wakati akichangia mchango wake kuhusu Bajeti kwa mwaka wa Fedha wa 2022/2023:
“Tunapoongelea kilimo kuna mambo mawili muhimu, kwanza ni soko na tija. Tija maana yake ni ufanisi katika kilimo kulinganisha na gharama ulizotumia kuwekeza.
“Tija katika kilimo inakuja tunapotumia teknolojia ya kilimo, ambapo kuna mambo manne ya teknolojia: Mbinu bora za kilimo, zana bora, pembejeo na huduma za ugani.
“Katika eneo hili la tija tumefanya vizuri sana katika maeneo ya huduma za ugani, pili ni katika mbinu bora za kilimo, mfano leo maeneo ya Songwe, Katavi, Ruvuma na kwingineko huwezi kuwafundisha kulima mahindi, wanajua aina ya mbolea na mahitaji mengine.
“Bado tuna changamoto katika zana bora za kilimo na kwenye pembejeo. Changamoto ya kwanza ni mitaji ambayo ndiyo itamsaidia mkulima kupata pembejeo, matrekta….
“Katika hilo, Benki yetu ya TADB ambayo ilikusudiwa kutatua tatizo la mitaji kwenye kilimo kwa wakulima wadogo na wakubwa, benki hii bado ina changamoto kubwa mbili, kwanza haina mtaji wa kutosha, katika utafiti wangu nimeambiwa mtaji mzima wa Benki ya Kilimo ni Tsh. Bilioni 268.
“Kama 60% ya Tanzania tunategemea kilimo, kama kila Mtanzania atakopa kwa ajili ya kilimo katika benki hiyo atapata Sh 7,000 tu, mtaji huu ni mdogo sana, huwezi kuleta mapinduzi kwa kutegemea benki hiyo, namuomba Waziri wa Kilimo atafute fedha za kuongeza na kuwekeza mtaji wa benki hiyo.
“Changamoto ya pili ni sera ya mikopo ya Benki ya Kilimo, sera za mikopo ya TADB, zinafanana na benki nyingine za kawaida.
"TADB ilikusudiwa kuwa benki ya uwekezaji, ningepewa nafasi ya kupendekeza jina ningependekeza iitwe Tanzania Agricultural Investment Bank kwa sababu tunapoteza ‘focus’.
“Ukienda kuangalia mitaji ya TADB wanatoa mikopo ya muda mfupi, thamani ya fedha inayotolewa ni ile ambayo unanunua mazao leo uyauze kesho.
“Uwekezaji kwenye kilimo unahitaji muda. Nasisitiza kuwa Waziri afanye linalowezekana kubadilisha benki hiyo, najua uwezo huo anao.”