Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
MBUNGE MHE. KENNETH NOLLO NA KASI YA MAENDELEO KATIKA JIMBO LA BAHI MKOA WA DODOMA
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Dodoma Mhe. Kenneth Nollo mwezi Aprili 2023 amefanya ziara katika Jimbo la Bahi na kukagua miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa Jimboni huku akishirikiana na wananchi katika shughuli za kijamii.
Mnamo tarehe 29 Aprili, 2023 Mhe. Nollo alijumuika na Wananchi wa Kijiji cha Msisi kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa Matano na Ofisi tatu Shule ya Msingi Msisi. Mhe. Nollo katika ziara yake aliwashukuru sana wananchi wa Kijiji cha Msisi kwa namna walivyoshiriki kufanya kazi kwa bidii na kukamilisha hatua hiyo mhimu.
Pia, Mhe. Nollo alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha za ujenzi wa madarasa na kutatua kero ya upungufu wa madarasa kwenye shule, Ujenzi wa barabara na daraja
Aidha, tarehe 22 Aprili, 2023 Mhe. Nollo alifanya ziara Kijiji cha Mzogole Kata ya Mpinga ambapo alifanya mkutano wa hadhara na kuongea na Wananchi katika Kijiji ambapo imejengwa Sekondari mpya ambayo imegharimu kiasi cha shilingi Milioni 470.
Serikali imetoa kiasi cha shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kiwango cha Changarawe na ujenzi wa daraja sehemu korofi kati ya Mzogole na Mpinga, ujenzi wa daraja barabara kiwango cha changarawe umekamilika na mkandarasi anaendelea na ujenzi wa daraja.
Katika ziara ya tarehe 20 Aprili, 2023 Mhe. Nollo akiwa Kijiji cha Kongogo alishiriki mkutano wa hadhara uliokuwa na lengo la kutoa ufafanuzi baada ya kutokea kikundi cha baadhi ya watu kupinga kuanza kwa utekelezaji wa Skim ya umwagiliaji ya Kongogo. Skim ya Kongogo imepata kiasi cha Shilingi 5.6 Bilioni ambayo itakuwa na eneo la ekari 1,000 na kazi za umwagiliaji zitafanyika muda wote wa mwaka.
Kazi ya ujenzi wa Skim inafanywa na Kampuni ya CRJE ambayo tayari mkandarasi amefika eneo la kazi (Site). Mhe. Nollo ameendelea kutoa shukurani sana kwa Serikali na Rais Samia kwa kuwapatia mradi mkubwa kwa mapinduzi makubwa kwenye sekta ya Kilimo.
Vilevile, tarehe 19 Aprili, 2023 Mhe. Nollo alifanya mkutano wa hadhara Kijiji cha Nagulo-Bahi na kutembelea kuona ujenzi wa Zahanati ambayo ni miongoni mwa miradi ya Zahanati 13 zilizopo katika hatua ya umaliziaji na zingine zimekamilika ambapo tarehe 20 Mei, 2023 itakuwa ni siku ya ufunguzi wa kutoa huduma.
Aidha, Mhe. Nollo alisema kuwa Kijiji cha Nagulo kimepata shilingi milioni 493 za kujenga Shule mpya ya Msingi itakayokuwa na Madarasa 14 ambapo ujenzi wa Shule hii unatakiwa kukamilika tarehe 30 Juni, 2023.
Wakati huo huo Mhe. Nollo aliwaambia wanakijiji cha Nagulo kuwa wamepata Shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari ya Shule ya Nagulo-Bahi na Shilingi milioni 560 kwa ajili ya mradi wa Maji ambao utatoa Maji kutoka Kijiji cha Uhelela kwa vile wao Kijiji chao kina Maji Chumvi.
Katika ziara ya tarehe 12 April, 2023 Mhe. Nollo alitembelea kuona Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Chali Igongo, Zahanati hii inajengwa na Mfadhili Shirika la Qatar Charity kutoka nchini Qatar. Ujenzi ulianza mwezi februari 2023, Zahanati inatarajiwa kukabidhiwa ikiwa na vifaa vyote mhimu Mwezi Mei 2023. Awali mwaka 2022 Shirika hili lilitoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa wa macho 476 ndani ya Wilaya ya Bahi.