Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
Mbunge Twaha Mpembenwe Afika Kibiti Kutoa Pole, Rais Samia Suluhu Hassan Kutuma Misaada ya Kibinadamu Kusaaidia Wahanga wa Mafuriko
Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mkoa wa Pwani, Mhe. Twaha Ally Mpembenwe amefanya ziara ya kuwatembelea wananchi wa Kata, Vijiji, vitongoji na mitaa katika Wilaya ya Kibiti kwaajili ya kutoa pole kutokana na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimeathiri makazi ya watu, mashamba na miundombinu mbalimbali.
Akiambatana na viongozi wengine Chama na Serikali wa Wilaya ya Kibiti, imewalazimu kutembea kwenye mvua na kwa kutumia mtumbwi kuvuka eneo moja kwenda eneo jingine ili tu kuwafikia wananchi wengi kujua hali zao na kujua aina ya misaada wanayopaswa kupewa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na wananchi, Mbunge Twaha Ally Mpembenwe amesema kuwa wananchi watakaoona hawawezi kukaa maeneo hayo kutokana na mafuriko kuzidi wasisite kutoa taarifa ili wapewe eneo salama la kujihifadhi wao na mali zao ili waendelee kuwa salama.
"Nimewasiliana na uongozi wa Serikali Mkoa wa Pwani ambao wameshatoa maelekezo Wilayani kufanya tathmini ya hali halisi jinsi ilivyo. Tumefanya kikao na Serikali imeridhia. Mheshimiwa Rais anawapa pole sana kwa mafuriko yaliyotokea" - Mhe. Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Jimbo la Kibiti
"Kuna watu wanapita huku mitaani kuchukua orodha na kuandika majina, naomba msiwadharau kwasababu ni maelekezo ya Serikali kuweza kupata orodha ya watu kamili waliokuwa wameathirika na kadhia hii ili sasa Serikali iweze kutoa Msaada" - Mhe. Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Jimbo la Kibiti
"Pamoja na yote, Mheshimiwa Rais anawapa pole, naye ameridhia kuwapa misaada ili iweze kuwafikia kuanzia wiki ijayo kama vyakula na magodoro. Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa ndiyo wanajukumu sana kuhakikisha vitu vinawafikia" - Mhe. Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Jimbo la Kibiti
"Mimi mtoto wenu nimeacha shughuli za Bunge nikasema nije kuungana nanyi na tayari tumeshatekeleza jukumu la kuwasemea kuhakikisha mnakuja kupata msaada. Nimeanza kupitia Mtanga, Usimbe, Ruma, King'ong'o, Visiwani na kipoka" - Mhe. Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Jimbo la Kibiti
Vilevile, Mhe. Twaha Mpembenwe amesema kuwa wananchi watakaoona hawawezi na mazingira ni magumu sana watoke waende nyumbani kwake maana kwake ni nyumbani kwao na wanaweza wakakaa siku kadhaa wakati Serikali inafanya utaratibu wa kuhakikisha inawatafutia maeneo ya hifadhi ya muda na baadaye wajue kitu cha kufanya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wazee na viongozi mbalimbali wa Visiwani Wilaya ya Kibiti wamemshukuru sana Mbunge wao, Twaha Mpembenwe kwa kuacha ratiba za Bunge na kufika kuwapa pole kwani ndiye Mbunge pekee ambaye amefanya hivyo tofauti na Wabunge waliotangulia kuwepo maeneo hayo ambao hawakuweza kufika kwao kuwajulia hali kipindi cha uongozi wao.