Kanungila Karim
JF-Expert Member
- Apr 29, 2016
- 20,743
- 25,564
Meneja wa Wakala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ngusa Julius, alibainisha kuanza kwa mradi jana alipozungumza na Nipashe kuhusu suluhisho la adha inayoendelea kuwatesa watumiaji wa barabara hiyo hasa mvua inaponyesha kwa wingi na kusababisha Mto Msimbazi kukata mawasiliano ya barabara.
“Kuna mkandarasi amekuwa akifukua mchanga na tope pale ili kutoa nafasi maji yaweze kupita, bado hakuna mafanikio, kilichopo sasa ni kusubiri upembuzi wa mradi huo ukamilike kisha hatua nyingine zifuate kwa ajili ya utekelezaji," alisema.
Katika eneo hilo, maji ya mvua kutoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo la kibiashara, yamekuwa yakifurika hivyo kuwaweka hatarini watumiaji wa barabara hiyo na mara nyingi Jeshi la Polisi limekuwa likiifunga barabara hiyo katika kipande cha Jangwani.
Hatua hiyo ya Jeshi la Polisi inasababisha usumbufu na gharama kubwa za usafiri.
Richard Abel, mkazi wa Kibamba jijini, alisema hulazimika kuunganisha magari matatu kwa safari moja ili kufika Posta anakofanya kazi.
“Serikali ione jinsi ambavyo inaweza kuhakikisha mpango huo unaanza na kukamilika mapema, hii kero ni kubwa, mbali na kutusababishia gharama, pia inasababisha tutumie muda mwingi kufika mjini na hata kurejea kwenye makazi yetu,” alisema.
Juzi, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, alisikika akizungumzia suala hilo wakati akizungumza na moja ya vituo vya redio jijini, kwamba mpango huo ulitarajiwa kuanza mwaka huu ukihusisha Jiji, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Benki ya Dunia (WB), lakini kuibuka kwa virusi vya corona kulisababisha kusimama kwa muda kwa utekelezaji wake.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mpango huo ukikamilika, mbali na kuondoa adha kwa watumiaji, pia utabadili taswira katika eneo la Jangwani kwa kuwa litakuwa la kuvutia kwa ajili ya mapumziko, michezo na makazi ya watu.
Chanzo: Nipashe