Alfajiri na mapema Vivian Njie mwenye umri wa miaka 89 aliwasha jiko lake la kuni katika mtaa wa Mbende, mji wa mapumziko wa Limbe uliopo Mkoa wa Kusini-Magharibi mwa Cameroon. Safari hii, sufuria iliyokuwa juu ya jiko haikuwa tupu.
Ndani yake, mchele mweupe wa punje ndefu uliotolewa na China ulikuwa ukichemka taratibu. Njie, bibi mwenye wajukuu 15, alikoroga wali huo uliokuwa ukipikwa kwa ajili ya watu 19 wanaoishi katika eneo la nyumba yake.
"Awali, tulikuwa tukipika wali kidogo tu halafu tuliugawa katika sahani tano," alisema. "Leo wajukuu zangu watakula hadi waseme, 'Nimeshiba.' Hilo pekee linanipa amani."
Kwa karibu muongo mmoja, mikoa ya Kaskazini-Magharibi na Kusini-Magharibi mwa Cameroon inayozungumza Kiingereza imekuwa ikikabiliwa na athari kubwa za mgogoro wa silaha wa kutaka kujitenga. Mashamba yameachwa bila kuhudumiwa, barabara za kuelekea sokoni zimekuwa hatari, na eneo la ardhi inayolimwa limepungua kwa asilimia 20 hadi 40 katika maeneo yaliyoathirika zaidi, jambo lililosababisha kupanda kwa bei za vyakula.
Mapema mwaka 2026, mashirika ya kibinadamu yalitahadharisha kuwa watu milioni 2.9 kote Cameroon, wakiwemo watoto milioni 1.5, wanahitaji msaada. Kutokana na mazingira hayo ndipo msaada kutoka China ulifika.
Mwezi Juni, Cameroon ilipokea bidhaa za chakula kutoka China, zikiwemo tani 1,630 za mchele na tani 880 za ngano zilizokusudiwa kwa mikoa iliyoathiriwa na mgogoro.
Hadi sasa, mifuko 9,000 ya mchele imepelekwa Buea, makao makuu ya Mkoa wa Kusini-Magharibi, ambapo usambazaji tayari umeanza. Mifuko mingine 10,700 imepelekwa Bamenda kwa ajili ya kusambazwa katika Mkoa wa Kaskazini-Magharibi.
Huko Limbe, Meya wa Halmashauri ya Jiji, Paul Efome Ngalle, alisimamia makabidhiano ya misaada hiyo kwa viongozi wa jamii, akisema msaada huo umefika wakati jiji hilo likiwa katika hali ngumu sana ya chakula.
"Msaada huu wa mchele kutoka China si chakula tu; ni ishara ya mshikamano," alisema Ngalle. "Makundi mengi yaliyo katika mazingira magumu katika manispaa yetu yameguswa sana na hatua hii."
Katika kituo cha usambazaji huko Buea, familia zilijipanga foleni zikiwa na kadi za kupokelea msaada. Kila kaya ilipokea mchele.
James Nkemasong, mwenye umri wa miaka 48, alikimbia kijiji chake katika eneo la Lebialem miaka miwili iliyopita akiwa na mkewe pamoja na watoto wake watano. Kwa sasa anaishi katika chumba kimoja cha kupanga mjini Buea.
"Mchele huu utatutosheleza kwa wiki kadhaa," alisema huku akiinua gunia la kilo 25 na kuliweka begani mwake. "Mambo yamekuwa magumu sana kwangu na kwa familia yangu. Tunapata shida kula milo mitatu kwa siku. Lakini mchele huu umetuletea afueni."
Hali kama hiyo inashuhudiwa pia huko Muyuka, mji mwingine katika Mkoa wa Kusini-Magharibi, ambapo Judith Mbah, mwenye umri wa miaka 38, anawapikia chakula watu 12 waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na migogoro.
"Mchele huu kutoka China ni laini na hauhitaji kuni nyingi kupikika," alisema. "Tunauchanganya na maharagwe pamoja na mafuta kidogo. Watoto wanauita 'wali mtamu' na wanauomba kila siku."
Mchele huo ulipowasili Limbe, haukuwa kwa ajili ya wale waliokimbia makazi yao kutokana na vita tu, bali ulikuwa pia kwa ajili ya watu waliokuwa wamepoteza kila kitu.
Mapema mwezi Agosti, mvua kubwa na ya kasi ilinyesha katika mji huo wa pwani ulio chini ya Mlima Cameroon. Maji ya mvua yalitiririka kwa kasi kutoka milimani bila njia ya kutokea, yakifurika katika makazi ya watu na kusababisha maporomoko ya udongo yaliyobomoa nyumba. Watu watatu walipoteza maisha.
Kwa jamii ambayo tayari ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya kuhama makazi kutokana na mgogoro wa kutaka kujitenga, mafuriko hayo yalisababisha janga jipya: si tu kupoteza makazi, bali pia kupoteza chakula. John Molua alipoteza sehemu kubwa ya mali yake kutokana na mafuriko hayo.
"Mvua inaendelea kunyesha. Lakini mchele huu unatupa utulivu na matumaini kwa wiki kadhaa. Wahanga wengi wamepata mchele huo, na tunahisi afueni kubwa. Umefika wakati muafaka, wakati ambao tunauhitaji zaidi," alisema.
Xiao Guofeng, mshauri wa masuala ya uchumi na biashara katika Ubalozi wa China nchini Cameroon, alisema msaada huo ni mojawapo ya hatua 10 madhubuti zilizotangazwa katika Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Beijing mwaka 2024.
"Msaada huu wa chakula ni mfano halisi wa urafiki kati ya China na Cameroon. Unaakisi sera ya China kuelekea Afrika, ambayo inaongozwa na kanuni za udhati, mshikamano, urafiki na uwazi, pamoja na maelewano mazuri ya urafiki na maslahi ya pamoja," alisema Xiao.
Meya Ngalle alibainisha kuwa hatua hiyo inaakisi ushirikiano wa zaidi ya miaka 55 kati ya Cameroon na China. "Hatua hiyo pekee inaimarisha si tu uhusiano kati ya mataifa, bali pia uhusiano kati ya raia, yaani uhusiano baina ya watu," alisema.
Katika maeneo kama Buea na Limbe, ambapo migogoro na mafuriko vimeweka familia katika hali ngumu sana, mifuko hiyo ya mchele inatimiza lengo la msaada: kuwasaidia watu kuendelea kuishi. Tukirudi Mbende, Njie alipika wali. Wajukuu zake walikula kwa haraka, kisha wakakimbia nje kucheza. Aliwatazama huku akitabasamu.
Katika eneo ambalo limeshuhudia mateso mengi mno, sahani ya wali wa moto inahuisha matumaini, sahani moja baada ya nyingine.