Halisi
JF-Expert Member
- Jan 16, 2007
- 2,802
- 614
Nimekutana na taarifa iliyotolewa leo na wakili wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Reginald Mengi, siku moja baada ya gazeti la Tazama kuandika habari na makala zenye muelekeo wazi wa chuki na jazba za wazi.
TAARIFA YA WAKILI MICHAEL NGALO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KICHWA CHA HABARI KATIKA GAZETI LA TAZAMA TANZANIA MENGI AKUMBWA NA KASHFA YA UFISADI Wananchi wataka Tume ichunguze bilioni 40 za Ukimwi
Ukurasa wa mbele wa gazeti la Tazama Tanzania toleo Na. 321 la Jumanne 6-113-19,2009 lilichapisha kichwa cha habari Mengi akumbwa na kashfa ya ufisadi Wananchi wataka Tume ichunguze bilioni 40 za Ukimwi.
Gazeti hilo lilichapisha katika ukurasa wa pili habari yenye kichwa cha habari Mengi na kashfa ya ufisadi. Habari hiyo inaeleza pamoja na mambo mengine kwamba mwanaharakati mmoja wa ukimwi amedai kwamba:-
Mengi alikuwa na sakata la akaunti ya zaidi ya bilioni 40 za wafadhili iliyofunguliwa kwa jina lake na ambayo mpaka sasa hakuna maelezo fedha hizo zilitumikaje au zilikwenda wapi, kwa sababu fedha hizo zilizowekwa katika akaunti yake zilichukuliwa na hazikuwafikia walengwa.
Mengi alifanya njama za udanganyifu kutumia fedha zote peke yake huku akiwaacha waathirika wakifa.
Uchunguzi wa kina ufanyike ili waliochukua fedha hizo warudishe kama walivyofanya wa EPA na Serikali ikabidhi upelelezi wa fedha hizo za waathirika wa ukimwi kwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili wahusika waweze kuhojiwa na kuchukuliwa hatua.
Yote yaliyoandikwa katika habari hiyo hayana ukweli wowote, na yanalenga kumkashifu Bw. Mengi. Inasema kwamba Bw. Mengi alifanya njama na udanganyifu kwa kutumia kwa manufaa yake binafsi Shilingi Bilioni 40 alizoomba na kuwekwa katika akaunti yake kwa manufaa ya waathirika wa ukimwi.
Gazeti la Tazama Tanzania linasema Bw. Mengi amekumbwa na ufisadi; linataka achunguzwe na atakiwe kurudisha fedha hizo kama walivyofanya watu waliohusishwa na EPA. Kwa maana ingine, linamwita fisadi na mwizi kama wale wa fedha za EPA.
Inaelekea Mhariri na Mwandishi wa gazeti hilo hawakufuata maadili ya
uandishi wa habari na hawakutaka kuandika ukweli, kwani wangefanya
uchunguzi angalao kwa kumhoji Bw. Mengi wangepata ukweli wa jambo hilo.
Wangefanya hivyo, wangebaini kwamba tarehe 17 Mei,2006 Mwanasheria
Mkuu wa IPP alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwamba IPP imegundua hati za kugushi za mradi uliopewa jina Home Based Care Services Centre na maombi yaliyopelekwa UNAIDS ya Sh. Bilioni 60 kutoka kwa mtu au watu waliojiita Reginald Mengi Community Services kama wamiliki wa mradi huo. IPP iligundua pia Bank Statement iliyogushiwa yenye jina Reginald Mengi Community Care ya NBC Corporate Branch iliyoonyesha kwamba mradi huo wa Reginald Mengi Community Services ulikwisha toa kwenye akaunti hiyo jumla ya Sh. 39,939,866,333.00 kutokana na maingizo ya jumla ya Sh. 41,552,733,874.00 ndani ya muda mfupi wa miezi minne tu.
Kwa kuwa IPP au Bw. Mengi hawakuwa na mradi unaoitwa Reginald Mengi Community Services au maombi ya msaada wa Sh. Bilioni 60.0 UNAIDS, ilihisiwa kwamba hati hizo ziligushiwa ama kwa makusudi ya kuzitumia kwa njia moja au ingine kuchafua jina la Bw. Mengi au kuzitumia katika vitendo vya jinai au vya udanganyifu mkubwa.
Mwanasheria Mkuu wa IPP aliwaandikia barua UNAIDS na kuwapa nakala za mradi uliogushiwa akitaka kujua kama walipata kupokea maombi ya msaada wa fedha kutoka kwa mradi huo na kuwaomba wawaripoti polisi wahusika kama wakifika ofisini kwao. UNAIDS walijibu kwa maandishi kwamba hawajapata maombi kama hayo na walitoa taarifa kwa vyombo vya habari tarehe 19 Mei,2006 kukanusha upokeaji wa maombi ya msaada kwa mradi huo.
Mwanasheria Mkuu wa IPP aliiandikia pia NBC Corporate Branch kutaka kujua kama wana akaunti ya Reginald Mengi Community Care na kama wanayo waeleze ilifunguliwa na nani. NBC ilipatiwa nakala ya picha ya Bank Statement. NBC walijibu kwa maandishi kwamba Bank Statement hiyo haikuwa ya NBC Limited.
Barua kwa UNAIDS na NBC zilinakiliwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Dar es Salaam.
Majibu ya UNAIDS na NBC yalithibitisha kwamba hati za mradi, maombi ya msaada wa fedha UNAIDS na Bank Statement ya NBC zilikuwa za kugushi kama ilivyokuwa imehisiwa.
Kutokana na kashfa za gazeti hili kwa Bw. Mengi, kuna nia ya kupeleka shauri mbele ya Baraza la Habari Tanzania kuliomba waitwe Bw. Mengi au Wakili wake, na Mhariri na Mmiliki wa gazeti la Tazama Tanzania na kusikiliza na kuamua kama Mhariri wa Tazama Tanzania na Mmiliki wake wamemkashifu Bw. Mengi au la, na hatimaye kuchukua hatua au kutoa maagizo inavyopasa na yenye nia ya kumaliza tatizo hili.
¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬
_____________________________
Michael Ngalo, Wakili
Ngalo & Company Advocates
14 Januari,2009
Last edited by a moderator: