Ilikuwaje hiyo? Hebu tupe stori.
Ninachojua ni kwamba JKT walikuwa wanajiunga baada ya kumaliza kidato cha sita.
Pia jeshini kitu kinachoitwa mgomo hakipo kwani kule ni amri na utii.
Pia Mambo ya jeshi humalizwa kijeda
MGOGORO KATI YA MWL NYERERE NA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM ULIOLETA AZIMIO LA ARUSHA.
Chanzo: 430/
MWALIMU aliwahi kuelezea aina ya Vijana aliotaka kuwaona ,alisema alitaka "Vijana jeuri na wenye kujiamini sio Vijana akina " ndiyo bwana"...... Vijana wenye ujasiri wa kuhoji mfumo wa jamii usioshahabiana na matakwa na matarajio ya jamii : Vijana waasi wa mifumo kandamizi.
Alisema " Ni kazi bure na kwa kweli ni ubatili mtupu ,kuwa na Taifa lenye "Silaha" nyenzo za maendeleo za kisasa lakini Vijana wake ni waoga.( Joseph Mihangwa).
Mawaidha haya yalijenga jeuri ya kujiamini kwa Vijana wa kitanzania miaka hiyo ya 1960 hadi kung'atuka kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1985, Ni jeuri hiyo aliyowajengea ,ambayo Siku moja ilimtoa jasho Mwalimu mwenyewe pale wanafunzi wa Vyuo Vikuu walipogomea mpango wake wa Jeshi la kujenga Taifa(JKT) mwaka 1966 na kulazimika kuwatimua Chuo hapo Oktoba ,1966.
Mapema Februari 1966, Serikali ilichapisha muswada wa Sheria kwa madhumuni ya kuanzisha program na jeshi la kujenga Taifa (JKT) kwa lazima, kwa Vijana wote waliomaliza elimu ya kidato cha sita na Vyuo vya elimu ya juu ,kikiwemo Chuo Kikuu pekee cha Dar es salaam wakati huo.
Mpango huo uliendeshwa na kusimamiwa na wanafunzi wa kijeshi kutoka Israel ,uliwataka Vijana kutumikia jeshi la kujenga Taifa kwa miaka miwili, ambapo miezi sita ya kwanza ilikuwa kwa mafunzo ya kijeshi kambini na miezi 18 mingine ya kutumikia jeshi nje ya kambi kama watumishi wa umma. Walitakiwa pia kukatwa asilimia 60 ya mishahara yao kama mchango katika kulitumikia Taifa.
Chuo Kikuu cha Dar es salaam kilichoanzishwa mwaka 1961 baada tu ya Uhuru ,kilitoa wasomi wake wa kwanza mwaka 1964 ambao walionekana tishio kwa nafasi za vigogo madarakani kwa sababu ya elimu yao. Ni vigogo hao walioasisi wazo la jeshi la kujenga Taifa JKT ,kwa Vijana ,lakini kwa nia njema ya kuimarisha uzalendo.
Kabla ya program hii ,JKT iliyoanzishwa mwaka 1964 ,ilikuwa kwa Vijana wa kujitolea. Hadi oktoba 1966 ,ni Vijana 25 tu wa kujitolea waliokuwa wamejiunga. Na pale mpango huo ulipochukua mkondo wa kuwaingiza wasomi kwa lazima, Muswada wake haukupokelewa vyema na wasomi nchini na baadhi ya wabunge.
Wabunge wasomi kama kina Nicholaus Kuhanga na wengine , wakati wakijadili muswada huo, walisema, ;"Kuwakata Vijana asilimia 60 ya mishahara yao kuwa ni ujamaa ni uongo, Wabunge na viongozi wa Serikali wanasahau kwamba , ni wao haohao wanaomiliki majumba yenye thamani kubwa na magari ya kifahari kinyume na itikadi ya ujamaa, wanapaswa kuonyesha kwanza kwamba wao ni wajamaa kabla ya kuwataka Vijana hawa masikini kuwa wajamaa "(Hansard,Septemba 22----Oktoba 11,1966,UK,249).
Muswada huu ulizua ukinzani mpana katika jamii hadi maofisini ,ambapo kuliripotiwa kisa kimoja na wakati wa mjadala bungeni. Juu ya mabishano makali ya maofisa wawili ; mmoja Msomi na mwingine asiye msomi , wakiapizana; yule asiyesoma akisema, " Kusoma si hoja hata muwe na digrii ,mtatufanya nini wakati tuna kila kitu, majumba ,magari ,vipusa (wasichana warembo) na madaraka tunayo?(Hansard, kama hiyo hapo juu) .
Mara tu muswada huo ulipopita ,wanafunzi waliwasilisha Serikalini madai yao ya kutaka muda wa JKT upunguzwe Kutoka miaka miwili hadi miezi sita na makato ya asilimia 60 ya mishahara yaondolewe .
Kukataliwa kwa madai hayo kulitafsiriwa kama nia mbaya ya Serikali dhidi yao, Ziara za mara kwa mara za viongozi wa Serikali Chuoni hapo kuzungumza na wanafunzi hazikubadili hisia za wanafunzi hao
Mambo yalitibuka zaidi pale aliyekuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na JKT wa wakati ule, Richard Wambura ,alipowahutubia wanafunzi ,Oktoba 18,1966, kwa hotuba ambayo ilitafsiriwa kuwa mpango wa JKT ulikuwa wa hila kwa lengo la kuwaonea na kuwanyanyasa Vijana kwa kuwa tu wao ni wasomi ,Baada ya hotuba hiyo, wanafunzi waliitisha mkutano wa dharura ambapo ziliundwa Kamati mbili ,moja ya kwenda kuonana na Rais Ikulu kuelezea malalamiko yao, na ya pili, kwenda Polisi kuomba kibali cha kufanya maandamano.
Kamati iliyokwenda kuonana na Rais ilitoa taarifa kuwa Mwalimu Nyerere hakuwa na uhakika juu ya kile kilichokuwa kikiendelea ; akayatupilia mbali malalamiko yao. Na ile iliyokwenda Polisi, ilitaarifu juu ya kukataliwa kibali, Hivyo ,Oktoba 21, 1966 ,uongozi wa wanafunzi ukaitisha kikao kingine cha dharura ,safari hii wakaazimia kuandamana bila kibali cha Polisi, kwenda Ikulu kukabiliana uso kwa uso na Mwalimu Nyerere.
Waliandaa mabango yenye ujumbe mbalimbali, Kwa kutaja baadhi tu, yalisomeka :"TUMECHOKA KUTUMIKIA WABENZI(mafisadi) "
"AFADHALI WAKATI WA UKOLONI", " KUMBUKA YA INDONESIA", "ATOKOMEZWE KAWAWA NA MPANGO WAKE WA JKT" na mengine mengi.
Hili la "KUMBUKA YA INDONESIA", liliikumbusha Serikali jinsi Serikali ya Rais Suharto wa nchi hiyo ilivyoangushwa kwa maandamano ya wanafunzi mwaka 1965.
Lakini hili la " AFADHALI WAKATI WA UKOLONI", inadhaniwa hadi leo kuwa bango hili halikuwa na ridhaa ya wanafunzi hao, bali lilipandikizwa na watu wa Usalama wa Taifa ili kuchokoza hasira ya Mwalimu Nyerere aweze "kuwaadabisha " waandamanaji hao. Na hili ndilo kweli lililomchoma zaidi Nyerere.
Huko Ikulu Oktoba 22, bila ya wanafunzi hao kujua ,Mwalimu aliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kuamua jinsi ya kukabiliana na waandamanaji watarajiwa, Iliazimiwa kuwa ,maandamano hayo yaongozwe na Polisi kuingia Ikulu siku hiyo, Oktoba 22, 1966.
Maandamano hayo hayakuwahusisha Vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam pekee ,bali walijiunga wengine wengi kutoka Chuo cha Uganga cha Muhimbili ; Chuo Cha Ualimu Chang'ombe, Chuo cha Biashara (CBE) ,Shule ya Sekondari ,Aghakhan na Vijana " wapita njia" wengine.
Ikulu waandamanaji hao walilakiwa na Mwalimu mwenyewe ,Makamu wa pili wa Rais Rashidi Mfaume Kawawa na Mawaziri.
Mwalimu akamkaribisha msemaji mkuu wa waandamanaji kuelezea malalamiko yao ; naye bila kusita kwa Lugha ya kiingereza fasaha ,akatamka masharti yao kwa sauti ya ukali ,akisema;
"......Serikali inajaribu kutupa mzigo wa kugharamia mpango huu(JKT) mabegani mwa wanafunzi masikini, .......Ama tulipwe haki zetu zote za mishahara ; ama wale wote wanaopata mishahara ya juu nao watumbukizwe katika utaratibu huu uonekane kweli ni wa kujitolea na si mpango wa kunyonya wasomi Vijana pekee."
Akaendelea :" kwa hiyo Mheshimiwa ,kama utaratibu huu pamoja na mawazo ya viongozi wa juu hayakubadilika ,hatukubali mpango wa JKT kwa moyo.
Miili yetu inaweza kwenda ,Lakini mioyo yetu itabaki nje ya mpango huu" akatamka kwa kujiamini na kwa kushangiliwa na wenzake. Kisha akamaliza kwa kishindo ,akasema "Na vita hii baina ya wanasiasa na watu wenye elimu itaendelea daima, Aksante".
Akawa amemchokoza Mwalimu.
Mwalimu alianza kujibu risala hiyo, kwanza kwa upole na kwa sauti tulivu ,akasema
"Nilitarajia haya mapema ,nimeyaelewa malalamiko yenu , sisi Serikali tumeupata ujumbe wenu; natafuta njia ya kuelezea kidogo ; maneno yenu mliyotuambia viongozi wenu tumeyasikia," akasema akiangaza macho huku na kule kukazia hoja"
Sauti yake ikaanza kupanda kidogo; "Sasa mimi nimeyakubali masharti yenu, naweza kuwahakikishia kwamba sitamlazimisha mtu yoyote.
Mnayosema ni sawa ; kwamba hata miili yenu ikienda JKT ,mioyo yenu haitakuwa huko ............Sitampeleka hata mmoja wenu JKT ambaye moyo wake haupendi (makofi) maana huko si gerezani.
Lakini hata hivyo mpango wa JKT utaendelea kuwa ni wa lazima kwa kila mwanafunzi ambaye hatimaye atafanya kazi serikalini, kwa hiyo ni juu yenu kuamua,.......", akatahadharisha , kisha akaendelea.
" Mnayosema juu ya mishahara yetu ni ya kweli ,ni mikubwa mno (shangwe na makofi), mimi na ninyi tumo katika kundi la wanyonyaji . Je, hayo ndiyo mambo nchi iliyoyapigania ? Je, juhudi yote tuliyofanya ni kwa sababu ya kuneemesha kikundi cha wanyonyaji huku juu? Akahoji kwa ukali, kisha akawaeleza juu ya mapinduzi yanayotakiwa ,akasema:
"Siku nikayoweza kumlipa mfanyakazi wa Tanzania Mshahara wa shilingi mia tano kwa mwezi ,tutakuwa tumefanya mapinduzi makubwa sana ; hapo tutaweza kusimama juu ya mlima Kilimanjaro na kutangaza Mapinduzi ya Tanzania kwa faraja na fahari kubwa."
Kuthibitisha kwamba alikuwa hatanii juu ya mishahara mikubwa ,Mwalimu alisema ," Mshahara wangu mnajua ni kiasi gani! Shilingi elfu tano kwa mwezi ; ni kiasi kikubwa mno!!Mshahara mkubwa mno sawa na pato la Mkulima wa kawaida kwa miaka 25;
Naupunguza kwa asilimia ishirini kuanzia sasa hivi, .........Nchi hii ya hovyo ; mishahara minene mno" akasema kwa kucharuka na kufoka, katikati ya ukimya uliokosa shangwe wala makofi.
Akarejea kwenye hoja ya siku hiyo, akasema " Mimi nimeyakubali maneno yenu mnayosema .....Na ninyi ,mimi nawaomba mwende Nyumbani kwenu.... Rashidi (yaani Kawawa) ni jukumu lako kuhakikisha kwamba wanakwenda kwao."
Alikuwa amewafukuza wanafunzi wote 415 : mara wakazingirwa na Polisi ,wakaanza kushughulikiwa na FFU kwa ulinzi na kudhibitiwa.
Oktoba 28,1966 Chama cha wanafunzi (USUD) ,kupitia barua iliyotiwa sahihi na Kaimu Rais wa chama hicho ,kilimwomba Mwalimu awasamehe wanafunzi waliofukuzwa kwa sababu tu ya "Kuchambua jamii waliyomo"
Barua nyingine ya Oktoba 30,1966 iliweka bayana kuwa malalamiko ya wanafunzi hayakutendewa haki kwa kupotoshwa kwamba walitaka kupindua Serikali wakati haikuwa hivyo, bali kuitahadharisha Serikali juu ya matabaka yaliyokuwa yakijengeka nchini.
Mwalimu hakujibu barua zote ,Wala hoja za Washauri wake wa karibu akiwamo msaidizi wake ,Mama Joan Wickens.
Alikaa kimya akiwaza na kuwazua hoja za wanafunzi aliowatimua na hatima ya nchi. Kwa kipindi chote kati ya Novemba 1966.
Na januari 1967 ,Mwalimu alikuwa akiandika itikadi na Sera mpya ya kisiasa na kiuchumi kudhibiti matabaka yaliyokuwa yameanza kujitokeza Nchini.
Aliandika Sera ya ujamaa na kujitegemea iliyotafsiriwa vyema katika Hati(blue print) iliyopewa jina la " Azimio la Arusha" na kutangazwa Februari 5,1967 kuwa dira ya maendeleo ya nchi.
Aliyekuwa mlezi wa wanafunzi wa Chuo ,Profesa T.O. Ranger ,katika barua yake aliyomwandikia Msaidizi wa Rais Mama Joan Wickens ,Kumb: C3/SA.13 ya tarehe 2/3/1967.
Kumuomba amshawishi Mwalimu awarejeshe wanafunzi hao 23, alisema haikuwa halali kwa wanafunzi hao kutumika kama chambo kwa Serikali iliyokuwa imepoteza dira na yenye kujaa mafisadi wasiojali maslahi ya umma.
Wanafunzi hao walirejeshwa mwaka 1969 pamoja na adhabu ya kuchapwa viboko kwa mkono wa Mwalimu mwenyewe.
Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea vilipokelewa kwa nderemo na vifijo na jamii ya wasomi kama mkombozi wa wanyonge ,kuanzia hap.
Na nchi kuamua kufuata siasa za mrengo wa kisoshalisti ,wanafunzi Vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam walifunga fungate ya uswahiba na Serikali Fungate iliyokuja kukatwa na Sera za soko huria kwa kuzika Azimio la Arusha na kuanza Kwa Azimio la Zanzibar la mwaka 1992.
Hivyo kuibuka kwa matabaka kipindi kile kulipata dozi kupitia kuanzishwa kwa Azimio la Arusha , na mpango wa JKT tunaona bado unaendelea mpaka leo kama njia nzuri na mahsusi ya kuwajenga Vijana kimaadili zaidi na kizalendo wakati wa kulitumikia taifa letu.
Pichani chini Siku Mwalimu Nyerere alipokuwa akiongea na wanafunzi wa Chuo Kikuu.
Na. Fredy Nyaluchi