SoC04 Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Walemavu Tanzania - Mapendekezo ya Uboreshaji wake kwa Kutumia Mkoa wa Dar es Salaam kama Mfano

SoC04 Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Walemavu Tanzania - Mapendekezo ya Uboreshaji wake kwa Kutumia Mkoa wa Dar es Salaam kama Mfano

Tanzania Tuitakayo competition threads

miamiatz

JF-Expert Member
Joined
Dec 4, 2017
Posts
505
Reaction score
941
Tanzania ina utaratibu wa kutenga kiasi cha fedha kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri zote kwa ajili ya maendeleo ya vijana, wanawake na walemavu. Fedha hizo hutokana na asilimia 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri, ambapo asilimia 4% hutengwa kwa vijana, asilimia 4% kwa wanawake na asilimia 2% kwa walemavu. Utaratibu huo unalenga kuboresha hali za maisha za makundi hayo kwa kuwapatia fursa za kujiajiri na kujiongezea kipato. Andiko hili litatumia mkoa wa Dar es Salaam kama mfano katika kupendekeza njia ya kuboresha mfumo unaotumiwa kwenye utekelezaji wa malengo ya mfuko huo.

Vijana wengi katika mkoa wa Dar es Salaam wanajishughulisha na biashara wengi wao wakiwa kwenye biashara ndogo ndogo kama njia ya kujipatia kipato. Hata hivyo, mazingira ya biashara kwa vijana hayaonekani kuwa rafiki hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu kama Mbagala. Vijana wengi hulazimika kujenga vibanda vya muda ambavyo mara nyingi havina usalama wa kutosha wala mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Changamoto hizi zinahitaji suluhisho la kudumu ambalo litatoa mazingira bora ya biashara na kuongeza tija kwa vijana.

Pendekezo la Matumizi Mbadala ya Fedha za Mfuko

Ili kuboresha hali hii, inapendekezwa kwamba mkoa wa Dar es Salaam utumie sehemu ya fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Walemavu kutengeneza fremu za biashara kwa kutumia makontena ya mizigo (shipping containers). Kontena hizi zitagawanywa katika vyumba vinne kwa kila kontena, na kufanyiwa insulation ili kudhibiti joto. Pia, kila kontena litakuwa na feni na soketi za umeme kwa ajili ya kurahisisha shughuli za biashara. Makontena haya yatawekwa katika maeneo yenye makazi mengi ya watu na kuwekewa kivuli (shades) ili kutoa mazingira mazuri ya kufanya biashara. Pia, kontena hizi zitapangwa vizuri pembezoni mwa barabara katika maeneo yenye msongamano wa watu ili kuhakikisha upatikanaji wa wateja.

Kwa mwaka wa kwanza, inapendekezwa kutolewa kontena 5,000 ambapo kila kontena litakuwa na fremu nne za biashara, hivyo jumla ya fremu 20,000 zitatolewa. Kila kijana atakayepatiwa fremu atalipa kiasi cha Sh 2,500 kwa siku kama pango la fremu hiyo. Ili kuhakikisha ukusanyaji mzuri wa mapato, kampuni binafsi za mikopo midogo (microfinance companies) zitahusishwa kama inavyofanyika kwa ukusanyaji wa taka na ushuru wa maegesho. Kampuni hizi zitapata asilimia katika mapato hayo kama motisha ya kuendeleza huduma hii.

Makadirio ya Mapato

Kwa makadirio ya mapato kwa mwaka wa kwanza, kutakuwa na mapato yafuatayo:

1. Pango la Sh 2,500 kwa siku kwa kila fremu: Kwa fremu 20,000, mapato ya kila siku yatakuwa Sh 50 milioni na kwa mwaka (siku 360), mapato yatakuwa Sh 18 bilioni.

2. Kodi ya mapato ya Sh 250,000 kwa mwaka kwa kila fremu: Jumla ya fremu 20,000 zitalipa kodi hii, hivyo mapato yatakuwa Sh 5 bilioni kwa mwaka.

3. Leseni ya biashara ya Sh 70,000 kwa mwaka kwa kila fremu: Mapato ya leseni kwa mwaka yatakuwa Sh 1.4 bilioni kwa fremu zote 20,000.

Jumla ya mapato yote kwa mwaka wa kwanza yatakuwa Sh 24.4 bilioni. Mapato haya yatasaidia kuongeza uwezo wa mkoa wa Dar es Salaam kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali kwa wananchi.

Manufaa ya Mradi

Mradi huu wa kutumia makontena kama fremu za biashara utaleta manufaa makubwa kwa mkoa wa Dar es Salaam. Kwanza, utaongeza nafasi za biashara kwa vijana na kuwasaidia kujiajiri kwa urahisi. Pili, utaboresha mazingira ya biashara kwa vijana na kuongeza usalama wa maeneo ya kazi. Tatu, mradi huu utaongeza mapato ya mkoa kupitia kodi na leseni za biashara, hivyo kusaidia kuboresha huduma za jamii. Aidha, mradi huu utapunguza tatizo la vijana kujenga vibanda vya muda ambavyo siyo salama na kuvuruga mandhari ya mkoa.

Pia, utekelezaji wa mradi huu utaboresha muonekano wa mkoa wa Dar es Salaam. Makontena yaliyowekwa vizuri pembezoni mwa barabara katika maeneo ya makazi ya watu wengi yatatoa mandhari nzuri na ya kuvutia. Mradi huu pia utasaidia kupunguza msongamano wa biashara holela barabarani na kuongeza usafi wa mazingira.

Matazamio ya Miaka 10 Ijayo

Sekeseke la ukosefu wa ajira linazidi kuwa kubwa kila siku. Sekta isiyo rasmi inaongoza kuajiri watanzania wengi. Utekelezaji wa mradi huu mkoa wa Dar es Salaam unakuwa ni mradi wa mfano na mikoa mingine kuiga kila mwaka. Hii itasaidia sana kujenga soko zuri la mazao ya kila aina na bidhaa mbali mbali za viwandani, kuongeza wigo wa mapato kwa kuwarasimisha wafanyabiashara wasio rasmi.

Hata wale wafanyabiashara ambao tunaona ni wadogo waliopo masokoni unakuta ana mauzo ya zaidi ya Sh 100,000 kwa siku sawa na zaidi ya milioni 35 kwa mwaka ambapo anatakiwa kulipia kodi ya 3.5% ya mauzo kwa mwaka ambayo ni zaidi ya milioni 1 kwa mwaka ila kwakuwa yupo nje ya mfumo rasmi wanakuwa nje ya wigo wa walipa kodi.

Ikiwa kila mkoa utafanya mradi huu kwa ukubwa tofauti tofauti unaoendana na hitaji la mkoa husika na ikiwa mfano wa mradi huu utatumika kwa mafundi randa, mafundi kuchomelea, na kadhalika basi baada ya miaka 10 tutakuwa tumekuza kwa kasi sana pato la taifa na kutoa ajira rasmi nyingi zaidi.

Angalizo la Utekelezaji wa Mradi

Wakati wa utekelezaji wa mradi huu, mkoa unapaswa kufanya utafiti wa kina ili kuboresha pendekezo hili na kuhakikisha linafanikiwa. Utafiti huu utasaidia kubaini mahitaji halisi ya vijana, maeneo bora ya kuweka makontena na jinsi ya kuboresha utendaji wa mradi huu. Pia, mkoa unapaswa kuangalia maboresho ya sheria na kanuni zinazohusiana na biashara ndogo ndogo ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu haukwamishwi na vikwazo vya kisheria. Maboresho haya ya sheria ni muhimu ili kuhakikisha vijana wanapata fursa nzuri ya kutumia fremu hizi za biashara bila matatizo.

Kwa kumalizia, pendekezo hili la kutumia makontena ya mizigo kama fremu za biashara ni suluhisho la kisasa na lenye tija kwa changamoto za vijana katika mkoa wa Dar es Salaam. Utekelezaji wa mradi huu utaboresha mazingira ya biashara, kuongeza ajira kwa vijana na kuongeza mapato ya mkoa. Hivyo, ni muhimu kwa mkoa wa Dar es Salaam kuzingatia pendekezo hili na kulitekeleza kwa umakini ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu kwa vijana, wanawake na walemavu.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom