Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye amezungumza na waandishi wa habari leo Mei 21, 2022 na kudai kuwa kilichofanywa na kundi lililojipa sura ya Halmashauri Kuu ndani ya chama hicho mapema leo ni uhaini.
Awali ilitolewa taarifa kuwa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi imemsimamisha Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia na Makamu Mwenyekiti Bara, Angelina Mtahiwa kutojihusisha na shughuli zozote za chama hadi Mkutano Mkuu utakapoitishwa ili wajieleze kuhusiana na tuhuma inazowakubali.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Mwenyekiti wa azimio hilo, Joseph Selasini alisema pamoja na kusimamishwa kwa viongozi hao pia wamelivunja Baraza la Wadhamini la NCCR na kuteua wajumbe wapya ambao watasajiliwa kwa mujibu wa taratibu zitakazowekwa.
Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Sisty Nyahoza naye alikiri kupokea barua kutoka NCCR-Mageuzi kuwa kuna mabadiliko ya wajumbe wa bodi ya wadhami.
Baada ya tamko hilo ndipo muda mfupi baadaye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Martha Chiomba, alifunga ofisi za chama hicho zilizopo Ilala, Dar es Salaam, ili kumzuia James Mbatia.
Baada ya tukio hilo, wanachama wanaomuunga mkono Mbatia ndani ya chama hicho walifika ofisini hapo na kufanikiwa kuingia ndani kisha kuzungumza na Wanahabari wakisema waliotangaza kumsimamisha Mbatia hawana mamlaka n ahata akidi haikutimia.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye amesema:
“Kilichofanyika ni uhaini na uhuni ndani ya chama na hatuwezi kukubali kilichofanyika, chama kitakaa na kufanya maamuzi, kinachotusikitisha zaidi Msajili wa Vyama vya Siasa ameshiriki katika uhuni huu.
“Huwezi kuvunja Bodi ya Wadhamini au kumsimamisha Mwenyekiti kihuni.
“Msajili haoni hata haya, alijulishwa aliyekuwa Katibu Mkuu amesimamishwa inakuaje anapokea maamuzi yanayofanywa na watu kama hao.
“Sisty Nyahoza ndiye anaendesha haya makundi, anafadhili haya makundi na tuna uhakika, ukifika wakati tutaweka ushahidi hadharani. Huyu ndiye mhuni wa kwanza katika huu mchezo mchezo mchafu.
“Huyo aliyeitwa Katibu Mkuu (Martha Chiomba) alisimamishwa katika Kikao cha Kamati Kuu, anayekaimu ni Anthony Kom hakushiriki kwenye hicho kikao na hajui kama kuna hicho kikao walichofanya.
“Hao Wahuni walikuja kujaribu kufunga ofisi lakini tumewadhibiti na ndio maana tupo ofisini hapa, ofisi ipo chini ya wanachama. Tutaudhibiti uhuni wao, tumejipanga na tupo imara, hakuna ambaye ataweza kuivuruga NCCR Mageuzi.”
Pia Soma >
NCCR Mageuzi yamsimamisha James Mbatia kufanya shughuli za Chama