Walimu watwangana Dar
Maulid Ahmed
Daily News; Tuesday,October 14, 2008 @20:00
Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), jana walivamiwa na kupigwa na walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kutangaza kuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi imesitisha mgomo wao uliopangwa kufanyika leo nchi nzima.
Vurugu hizo za walimu kugeuka mbogo na kuwashambulia viongozi wao zilianza baada ya Rais wa CWT Taifa, Gratian Mukoba, kuwatangazia walimu waliokusanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee kwa ajili ya uzinduzi wa mgomo huo kuwa sasa haupo.
Ilibidi polisi wafyatue risasi hewani ili kutuliza vurugu hizo ambazo zilianza kuenea hadi barabarani. Mukoba ambaye wakati anaanza kuwahutubia walimu na kuwaeleza kuwa mwanasheria wao anakusudia kuwasilisha rufaa katika Mahakama ya Rufaa, alizomewa na walimu hao na alipowaeleza kuwa mgomo kwa sasa hautakuwapo hivyo wawe watulivu.
Mara alishtukia chupa za maji zikitoka kila pembe ya ukumbi huo na kuelekezwa katika meza kuu walikokaa viongozi wa chama hicho wa Taifa na Mkoa wa Dar es Salaam.
Walimu waliokuwa na jazba mbali ya kutupa chupa pia walianza kurusha viti kuelekea jukwaa la viongozi na kusababisha mkutano huo kuvunjika majira ya saa 6:17 mchana huku wengine wakizomea na kutoka nje.
Wakati hayo yakiendelea walimu wengine waliamua kuvamia meza kuu na kuvunja meza hali iliyosababisha viongozi waliokuwa wameketi hapo kukimbia na kujibanza pembeni huku wakilindwa na askari kanzu.
Miongoni mwao waliovamia meza kuu, walitoweka na simu ya Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Mwanza aliyefahamika kwa jina moja la Raphael ambaye alihudhuria mkutano huo kuwapa salamu za watu wa Mwanza na kuonyesha wanawaunga mkono katika mshikamano wao.
Walimu hao wakati wanafanya mashambulizi walisikika wakisema ‘chama kivunjwe'; ‘Mukoba umetusaliti jiuzulu'; ‘kesho (leo) tunagoma'.Wakati wanaendelea na vurugu hizo huku wengine wakijiangusha chini na kulia na kutoa kauli kali dhidi ya viongozi wao, ghafla mwalimu mmoja alichukua kipaza sauti na kuwaita wenzake ndani huku akiwaeleza mgomo upo pale pale hali iliyowarudisha baadhi ya walimu ukumbini ambapo baada ya kufika walianza tena kushambulia jukwaa kuu wakati huo meza na viti vikiwa vimeshaparaganyika.
Ilipotimia majira ya saa 6:45 mchana na kuona viongozi hao hawatoki ukumbini, walimu wengi wao waliokuwa nje ya ukumbi wakiimba walianza kurusha mawe juu ya bati la ukumbi huo ambapo baada ya dakika chache magari manne ya Polisi yaliwasili eneo hilo.
Gari moja liliegeshwa katika mlango wa nyuma wa ukumbi huo na polisi waliokuwamo ndani baada ya kuona walimu wanazidi kurusha mawe walifyatua risasi tano hewani kuwatawanya walimu na kutumia muda huo kuwaondoa Mukoba na Makamu Mwenyekiti wake, Honoratha Chotanda.
Baada ya viongozi hao kuondoshwa eneo hilo, walimu waliendelea na vurugu huku wakiimba na kucheza katikati ya barabara na kusimamisha magari mengine huku wakiwaimbia ‘kama sio juhudi zetu walimu, madereva mngesoma wapi'; ‘mnanunua magari ya ufisadi na kutumia fedha zetu'; na nyingine zenye mwelekeo wa kisiasa.
Kama hiyo haitoshi walimu walivamia gari la Polisi lenye namba T 210 AMV na kulizunguka huku wakiwaimbia ‘kama sio juhudi zetu walimu polisi mngesoma wapi ?' huku wakilisindikiza gari hilo lililoingia ndani ya ukumbi kwa kupitia mlango wa mbele na kuwachukua viongozi wengine waliobaki wa CWT.
Wakati gari hilo linatoka lilirushiwa chupa za maji lakini polisi hawakujibu mashambulizi. Baada ya viongozi hao kuondoka walimu hao waliendelea kuimba na walianza kuondoka kwa makundi.
Awali walimu hao wakati wanaanza mkutano wao majira ya saa 4:00 asubuhi walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumtukuza Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na kuonyesha picha yake kuwa alikuwa mtetezi wao.
Mbali na hizo waliimba nyimbo nyingine kuonyesha kuwa wao ni muhimu na kumshutumu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe kwamba; ‘Kama sio juhudi zetu walimu, Maghembe ungesoma wapi'; Hakuna kulala hadi kieleweke'; walimu ndio sisi tunaotegemewa kuleta maendeleo katika nchi'.
Hata hivyo hali katika ukumbi huo ilianza kubadilika aliposimama Mwenyekiti wa CWT wa Mkoa wa Mwanza na kueleza kuwa watalazimika kuacha mgomo kwa sababu ya amri ya Mahakama ila baadaye wataweza kulizungumza hilo, ndipo akaanza kuzomewa akitakiwa kukaa.
Aliposimama Naibu Katibu Mkuu, Ezekiah Oluoch na kutaka kuzungumzia juu ya tuhuma za ufisadi kuhusu jengo la Mwalimu House, ghafla alisimama mwalimu mmoja na kumtaka akatishe kwani hiyo haikuwa mada ya mkutano wao.
CWT ilitoa notisi ya kukusudia kugoma Oktoba 15 lakini Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi juzi iliamuru kusitishwa kwa mgomo huo baada ya serikali kuwasilisha mahakamani hapo hati ya zuio la mgomo.
Walimu hao walikusudia kugoma hadi hapo serikali itakapotekeleza madai yao ikiwamo kuwalipa malimbikizo ya mishahara, posho za uhamisho, kujikimu, usafiri na upandishaji wa madaraja.