Ikulu: JK hangoki
na Happiness Katabazi na Sauli Giliard
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
OFISI ya Rais (Ikulu) imesema hakuna kundi lolote linalopanga njama za kutaka kumzuia Rais Jakaya Kikwete ili ashindwe kugombea urais katika muhula mwingine wa pili mwaka 2010.
Tamko hilo la Ikulu lilitolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salvatory Rweyemamu, aliyekuwa akizungumza na wanahabari ofisini kwake kuhusu habari zilizoandikwa katika gazeti la kila wiki lililochapishwa juzi Jumatano.
Katika mazungumzo yake hayo, Rweyemamu aliielezea habari hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho: Njama za kumngoa Kikwete zafichuka kuwa ni za uzushi na zenye lengo la kumfitinisha rais na mawaziri wake.
Mbali ya hilo, Rweyemamu alisema habari hiyo ya MwanaHalisi ilikuwa ni porojo za kuganga njaa na akawataka wanaoliendesha gazeti hilo kuachana na kazi ya habari iwapo wameshindwa kuifanya.
Huu ni uongo uliotungwa na kutiwa chumvi nyingi tu kwa lengo la kutaka kuuza gazeti. Ni porojo tu za kutaka kuuza gazeti, alisema mkurugenzi huyo.
Rweyemamu alichukua fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kutokuwapo kwa tishio wala njama za kumngoa Kikwete katika uongozi wake.
Unamngoa vipi rais ambaye utendaji wake wa kazi umeleta mafanikio makubwa kwa wananchi na umekuwa mfano wa kuigwa mbele ya mataifa mengine?
Hakuna tishio lolote, hakuna njama zozote za kumngoa rais madarakani, iwe ni leo au mwaka 2010, kama gazeti hilo lilivyodai... kama kungekuwa na njama hizo mtu wa kwanza kujua angekuwa ni rais mwenyewe, kwani rais ana vyombo vya ulinzi na usalama, alisema Rweyemamu.
Alisema kuwa Kikwete ameendelea kupendwa, kuungwa mkono na kuaminiwa na wananchi waliomchagua kwa kishindo, na zaidi ya yote, vyombo vya ulinzi viko macho wakati wote kuhakikisha kuwa yuko salama.
Katika hatua nyingine, mkurugenzi huyo alisema gazeti hilo linatumiwa na vyama vya upinzani na kazi yake imekuwa ni kueneza propaganda za vyama hivyo.
Wakati Ikulu ikitoa tamko hilo, Mbunge wa Igunga Rostam Aziz (CCM), amefungua kesi ya madai Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Ltd, inayochapisha gazeti la MwanaHALISI na Mseto, Saed Kubenea, akitaka amlipe fidia ya sh bilioni tatu kwa kumkashfu.
Mbali na Kubenea, wengine walioshitakiwa katika kesi hiyo ni mhariri wa MwanaHALISI, Hali Halisi Puplishers na Kampuni ya Uchapaji ya Printech Ltd.
Kesi hiyo ambayo tayari imeshapewa namba 143 ya mwaka huu, muda wowote kuanzia sasa inatarajiwa kupangiwa jaji wa kuiendesha.
Katika kesi hiyo, Rostam anadai kuwa, wadaiwa wote kwa nafasi zao wamekiuka miiko na maadili kwa kuchapisha habari ya uzushi dhidi yake.
Rostam anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Kennedy Fungamtama, alidai gazeti la MwanaHALISI la Septemba 24-30 toleo namba 116, katika ukurasa wa 1 na 2, wadaiwa waliandika na kuchapisha habari iliyokuwa na picha ya mlalamikaji na kichwa cha habari: Rostam atajwa tena. Ni katika ukwapuaji wa sh bilioni 13, ofisi, wafanyakazi wake watuhumiwa.
Anadai yeye (Rostam) akiwa mbunge, mfanyabiashara na mtu mwenye heshima ndani ya jamii, amefedheheshwa na habari hiyo, kwani inajenga chuki kwa wananchi. Kutokana na sababu hiyo, anaiomba mahakama hiyo iamuru (Kubenea) amlipe kiasi hicho cha fedha na pia aombwe radhi ukurasa wa mbele kwenye gazeti hilo.
Habari hiyo imejaa uzushi na haina ukweli wowote, haijafanyiwa utafiti kabla haijaandikwa, hivyo mwandishi wa habari hiyo amekiuka maadili ya kazi yake. Na kwa sababu hiyo, nataka nilipwe fidia ya kiasi hicho na (mahakama) iwaamuru wadaiwa waniombe radhi katika gazeti lao, alidai mbunge huyo katika hati hiyo ya mashitaka.
Juzi serikali ililitaka gazeti hilo kujitetea kwa nini lisichukuliwe hatua kutokana na habari iliyochapishwa kuwa kuna njama za kumngoa Rais Jakaya Kikwete ili asigombee urais mwaka 2010.
Kutokana na habari hiyo, serikali ilimpa siku tatu Kubenea, ambazo zinamalizika leo kuwasilisha maelezo yake ya kina Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kuhusu tuhuma mbalimbali alizoziibua katika habari hiyo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa juzi na wizara hiyo na kusainiwa na msemaji wake, Jacob Tesha, ilieleza gazeti hilo limedai kundi la watuhumiwa wa ufisadi limejipanga kumngoa Rais Kikwete mwaka 2010 na kuwataja baadhi ya viongozi wa CCM na mwanawe Rais, Ridhiwani, kuwa wanahusika katika njama hizo.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa habari hiyo ni ya uchochezi, inayolenga kumgombanisha rais na viongozi waandamizi wa CCM na kuleta mtafaruku katika familia yake.
Mbali na hilo, kupitia taarifa hiyo, serikali imewaonya baadhi ya waandishi wa habari ambao kwa makusudi, wamekuwa wakiandika habari zisizo sahihi na zenye kuchochea chuki miongoni mwa jamii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika miezi ya hivi karibuni, gazeti hilo limekuwa likiandika habari zisizo sahihi na za uchochezi, jambo lililosababisha wahariri wa gazeti hilo kuonywa na serikali mara kadhaa.