The Khoisan
JF-Expert Member
- Jun 5, 2007
- 16,434
- 14,547
Mtoto Sheikh Sharif Yusufu Mohammed
Maelfu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, jana walipigana vikumbo kugombea kupata huduma ya mtoto mwenye umri wa miaka 12 anayeaminika kuwa na karama ya uponyaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya magonjwa yote yanayomsumbua mwanadamu.
Nipashe ilifika jana asubuhi katika Mtaa wa Luponda, ulioko Magomeni Makuti, Wilaya ya Kinondoni na kushuhudia maelfu ya watu wa rika na jinsia tofauti wenye maradhi tofauti wakiwa wamefurika ndani na nje ya nyumba inayotumiwa na mtoto huyo kutolea huduma zake, wakisubiri kuhudumiwa.
Mtoto huyo, Sheikh Sharif Yusufu Mohammed, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Kiembesamaki, visiwani Zanzibar, amekuwa akitoa huduma yake kwa njia mbalimbali, ikiwamo kuwaombea dua (maombi) wagonjwa ili kupona maradhi yanayowasumbua.
Dua hiyo husomwa na Sheikh Sharif kwa awamu mbili tofauti; moja ikiwa ni kwa watu wote, ambayo huisoma kwa kushirikiana na wasaidizi wake na nyingine humsomea mgonjwa mmoja mmoja, huku akiwa amemuwekea mkono kichwani.
Wasaidizi wengine wa mtoto huyo ni Sheikh Salim Khamisi, maarufu kama "A'inan Mardhwiyyah", Sheikh Maulana Habshiy na Sheikh Sultan Khamisi (bwana dawa).
Njia nyingine inayotumiwa na mtoto huyo katika kuwahudumia wagonjwa, ni kuwapatia maji kwa matumizi ya kunywa kwa masharti, baada ya kuyaombea maji hayo.
Baadhi ya wagonjwa waliozungumza na Nipashe, walidai wanaamini huduma inayotolewa na mtoto huyo ni ya uhakika kwa vile kila aliyebahatika kuhudumiwa naye, alipona, wakiwamo watu waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi sugu na yasiyotibika.
Mmoja wa wasaidizi na kaka ya mtoto huyo, Sheikh Salim Khamisi, alisema miongoni mwa wagonjwa waliokwishahudumiwa na mdogo wake, ni pamoja na mama mjamzito, mkazi wa Mabibo, jijini Dar es Salaam aliyedumu na ujauzito kwa miaka minne.
Alisema baada ya kuhudumiwa na Sheikh Sharif, hivi sasa mama huyo yuko hospitali na kwamba, uchunguzi wa kidaktari umethibitisha kuwa ana ujauzito wa watoto mapacha na anatazamiwa kujifungua wakati wowote kuanzia hivi sasa.
Kwa upande wake, Sheikh Sharif alisema karama aliyonayo, amejaliwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, kwa karama hiyo kamwe hawezi kuthubutu kujiita yeye ni Nabii wala Mtume kwa vile anaamini kuwa Nabii Muhammad (S.A.W.) ndiye Mtume wa mwisho.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Huyu ndiye anafaa kumlinda JK siyo Mtabiri Yahya.