Nawapongeza sana Simba kwa uamuzi mgumu na wenye changamoto nyingi ya kujenga uwanja kwa kuwaomba watu wenye nia njema wawachangie. Watu wenye mioyo mepesi tayari wameshakata tamaa hata kabla zoezi zima halijaanza. Simba wasikate tamaa kwani uwanja wao watajenga na wengine watakuja kuiga huko baadae. Kwa watu waliojenga nyumba kwa kuunga unga wanajua kabisa jinsi ujenzi ulivyo mgumu lakini baada ya miaka kadha wanajikuta wapo ndani ya nyumba zao. Wale wenye mioyo mepesi ndio wale utawasikia nyumba inauzwa ipo kwenye linta, wengine hajapauliwa, wengine ipo kwenye msingi na hadithi kama hizo.
Hata wakati pori la Bunju linanunuliwa kulikuwa na maneno ya kukatisha tamaa. Ikaja ujenzi wa viwanja vya mazoezi napo kulikuwa na maneno kibao. Sasa Simba wanataka waanze ujenzi wa uwanja wao yameanza tena maneno. Kwa kifupi waswahili ni watu wa maneno na hupenda kuwakatisha tamaa wenzao ambao wana uthubutu wa kufanya mambo makubwa ambayo wao kwa mtizamo wao hasi wanaona hayawezekani.
Uzoefu unaonyesha kuwa unapoanza jambo fulani ukikutana na changamoto ndipo akili inapoanza kufanya kazi ya ziada ya kutafuta namna ya kutatua changamoto hiyo. Kwa hiyo basi nina hakika kabisa kwa kuwa Simba wameamua kuanza kujenga huo uwanja basi ni lazima huko mbele ya safari changamoto kubwa inayoonekana kwa sasa pesa itapatiwa ufumbuzi kwa kupatikana vyanzo vingi vya mapato na ujenzi utaisha salama.
Hakuna kitu kibaya maishani kama kukataa tamaa na hakuna kitu kizuri duniani kama kupambana na changamoto unazokutana nazo. Hivyo basi tusiwakatishe tamaa Simba bali tuwape moyo waendelee na jambo lao la ujenzi wa kiwanja chao. Mafanikio ya Simba ndio chachu ya mafanikio ya timu nyingie mwisho timu zote zikifanikiwa ndio mpira wetu Tanzania utakuwa wa kiwango cha juu.