Chaneta, Chaneza wanaangamiza mipira wa pete
Send to a friend Sunday, 28 November 2010 19:51 0diggsdigg
Jessca Nangawe
MOJA ya tatizo kubwa linalorudisha nyuma maendeleo ya michezo hapa nchini ni suala zima la migogoro inayoota mizizi ndani vyama husika hadi kupelekea kupoteza mwelekeo na mwisho wa siku mchezo husika kufa au kukosa mwelekeo.
Licha ya kuwa ni jambo la kawaida kuwepo kwa migogoro ndani ya chama ama klabu hapa Tanzania jambo geni, lakini endapo inazidi na kuota mizizi ina athari kubwa sana kwa mchezo husika.
Tumeshudia migogoro mikubwa ikizuka katika klabu za Yanga na Simba, vyama vya michezo kama riadha, ngumi, soka na netibali kutokana na matatizo hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya michezo hapa nchini.
Nimesukumwa kusema ivyo kutokana na kuwepo kwa mgogoro ambao kwa sasa unaelekea kuota mizizi baina ya Chama cha mchezo wa Netiboli Tanzania (Chaneta) na wenzao wa visiwani (Chaneza) ambapo kila kukicha tatizo hilo halipatiwi ufumbuzi.
Ni muda mrefu sasa tangu mabaraza ya michezo BMT na BMTZ kuvitaka vyama hivi kuondoa tofauti zao na kujumuika pamoja katika shughuli mbalimbali za kimichezo ikiwemo kushirikiana katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Vyama hivi vimeonekana kuziba masikio kwani licha ya Wizara ya michezo kuinglia kati lakini mpasa sasa hakuna dalili wala kuwepo kwa upatano miongoni mwa vyama hivi.
Kikubwa ambacho vyama hivi vimeonekana kutofautiana ni kuhusiana na utendaji kazi miongoni mwa viongozi ambao mpaka nazungumza hakuna maelewano mazuri hali iliyopelekea hata wenzetu wa visiwani kususia kuleta timu kushiriki mashindano ya kimataifa yaliyomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini.
Hali hii kwa kiasi kikubwa imepelekea kuwepo kwa mgawanyiko ambao haufahamiki hatma yake nini kutokana na kila siku viongozi hawa kupiga kalenda ya kukutana na kuonekana kuwepo kwa kiini macho katika jambo hili.
Viongozi wa vyama hivi wanapaswa kufahamu umuhimu na heshima ambayo wamepewa na Rais Jakaya Kikwete kwa kuwaleta kocha kutoka nje kwa ajili ya kuinua mchezo huo hapa nchini.
Baada ya kuletwa kwa kocha huyo ambae alikuja kwa maslahi ya wote (bara na visiwani) Wizara ya michezo ilisisitizwa atumiwe kwa wote kwani agizo la Rais ni kutaka kuona maendeleo ya mchezo huo yakipatikana kwa wote na kumtumia kocha huyo kufundisha timu ya Taifa kwa ujumla kama ilivyo kwa timu ya Taifa ya wanaume 'Taifa Stars'.
Kikubwa ambacho vyama hivi wanapaswa kuliangalia kwa kina ni jinsi ambayo wamepewa heshima na kutekelezewa ahadi yao lakini sasa kushindwa kuwa na shukrani na matokeo yake kuzidi kupandikiza mizizi ya migogoro badala ya kuiondoa.
Pili viongozi hawa wanapaswa kufahamu mchezo huu umefikia wapi na unahitaji kupewa msukumo zaidi ili uweze kukua na kupanuka zaidi kama ilivyo kwa michezo mingine.
Sitapenda kuingilia majukumu ya viongozi hawa, lakini inawapasa kuheshimu kauli ya viongozi wao wa juu na kufanya kama walivyoagizwa kwa maslahi ya mchezo huu na Taifa kwa ujumla.
Nilijaribu kuzungumza na viongozi wa Zanzibar ambao wao walikua tayari kufikia muafaka endepo Chaneta watahitaji kukaa nao, lakini wakadai mpaka sasa hakuna taarifa yoyote waliyoipata kuhusu kukutana huko hivyo wameomba wasilaumiwe kwa kitu chochote kwani wao wanaheshimu katiba na taratibu za nchi.
Kitu kikubwa ambacho kinaonekana kuwepo kati ya vyama hivi ni ushindani usiokua na maana yoyote na hivyo kupelekea mgogoro huzidi kushika kasi bila kuwepo hitimisho lake.
Kama nilivyotangulia kusema migogro kama hii hujitokeza katika michezo yote lakini imekua ikitafutiwa ufumbuzi na kumalizika,hivyo ni muda na changamoto sasa kwa vyama hivyo kuchukua tahadhari mapema na kuhakikisha wanapata suluhu la mgogoro wao mapema na kulimaliza.
Mfano mzuri ni mgogoro ambao ulitokea kati ya Shirikisho la soka Tanzania TFF na wenzao ZFA ambao mwisho wa siku walifikia muafaka na kumaliza tofauti zao na mpaka sasa wamekua wakishirikiana katika maswala mbalimbali ya soka.
Nasema hivyo ili kutoa changamoto na msukumo wa vyama hivi kuweza kuiga wenzao kwa kubadilika na kuachana na dhana potofu za kulumbana katika zama hizi za ukweli na uwazi.
Chaneta na Chaneza wakae na kumaliza tofauti zao kabla tatizo hili halijawa kubwa zaidi na kuleta mpasuko ambao mwisho wake ni kuua kabisa maendeleo ya mpira wa pete hapa nchini.
Najua kwamba migogoro hii ya vyama vya michezo ni moja ya matatizo ya muungano hakuna shaka kwamba rais Kikwete na Dk Ally Sheini wataishiwishi wizara inayoshughulikia mambo ya muungano kulijumuisha na hili la michezo ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Naamini migogoro hii ikitatuliwa kwa haraka na vyama hivi vikiweka nguvu zao nyingi kwenye kutafuta mbinu za kuendeleza michezo basi hakuna shaka na sisi siku moja tutafika mbali zaidi kwenye nyanja hii.
Mungu ibariki Tanzania, Ibariki Afrika.