Mfumo huu unatupeleka kuzimu
Kenny Mwaisabula
HATA uniamshe usingizini, kwangu mimi nahitaji mataji (vikombe), kwa maana moja tu ya ubingwa, gombana na serikali, gombana na FIFA, gombaneni wenyewe kwa wenyewe, gombaneni na waandishi wa habari hadi mpewe majina ya mabondia, lakini mimi furaha yangu ni ushindi tena si ushindi tu ni kunyakua mataji. Nje ya hapo mimi sielewi na akili yangu inakataa kuelewa. Inawezekana ikasemwa sasa, uongozi uko imara sana tofauti na zamani, mipango ya fedha leo inaonekana vizuri na kwa uwazi zaidi tofauti na zamani,
Viongozi hawalumbani tofauti na zamani, wana utaratibu mzuri wa kuzungumza tofauti na zamani, kwangu mimi yote hayo yanapitia sikio moja na kwenda sikio la pili, sielewi kama siyaoni mataji, akili inakataa kukubali.
Katika moja ya makala zangu za nyuma, nadhani katika gazeti hili hili niliwahi kuandika tatizo la soka letu kuwa si kocha wa kigeni na nilisisitiza hata aje Sir Alex Furgerson wa Manchester United ya pale England, kwa mfumo huu tutaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu.
Wengi waliniunga mkono, ingawa wachache walisema ninawachukia wale jamaa wa pale mjengoni Karume yaani TFF, lakini ukweli sina chuki yoyote na watu wale, kwanza Sunday Kayuni ni kaka yangu, penye matatizo na mimi anaweza kuniita wakati wowote kama mdogo wake, lakini katika suala linalohusu soka sishindwi kuweka bayana hisia zangu kupitia kalamu.
Tenga, ni lazima nikiri kuwa hanijui vizuri, hivyo sina sababu ya kumchukia mtu ambaye hanijui, mi' naandika kwa kueleza mustakabali wa soka letu na si vinginevyo.
Ni ukweli usopingika kuwa pamoja na mazuri yote ya uongozi wa Leodegar Tenga, lakini hatujawahi kucheka, yaani kuchukua kombe lolote na mbaya zaidi hata pale tulipotegemea tungefika angalau fainali kwenye fainali za CHAN, bado tulitolewa asubuhi tu.
Maana katika CHAN kwa taarifa yako sisi ndio tuliopeleka kikosi cha kwanza, wengine wote walipeleka vikosi vya pili, ndio maana mi' nasema katika hilo kila siku nitakuwa upande wa kushoto na kuwaacha rafiki zangu wapenzi kina Samson Mfalila na Eddo Kuwembe upande wa kulia na tukishirikiana katika ‘Monde' tu, mi' nataka mataji tu na si vinginevyo.
Pamoja na matatizo yote, mfumo mzima wa soka wameuua kina Tenga na Kayuni, leo hatuoni cha maana walichokifanya baada ya kuondoa zile ligi za madaraja ya nne, tatu, ngazi ya kanda daraja la pili na kuendelea mikoani; leo soka mahali ambako tulikuwa tunapata timu ya taifa haliko.
Utapataje watu kama kina Leopard Tasso Mukebezi ambaye alicheza mpira wake wote Kagera, Mohammed Chuma timu ya taifa miaka 11 bila kuachwa akitokea Mtwara, Kasimu Manga na Hussein Ngulungu, wakitokea Morogoro yaani Mji Kasoro bahari, Omary Zimbwe, Abdallah Luo, Omari Mahadhi wote hao Tanga.
John Lyimo, Mbwana Bushiri wa Moshi, Yunge Mwanansali Tabora na wengine wengi tu, unategemea nini?
Wakati leo Tanzania ina miundombinu rahisi kufika popote kwa siku moja tu, iwe unaenda Mtwara, Mwanza, Songea, Rukwa, Musoma, Kagera na kwingineko, TFF bado mmeng'ang'ania timu 12 tu katika Ligi Kuu, kwa nini zisiwe 20 ili angalau mchezaji wa ligi akapata mechi 35. Mimi napata taabu! Labda mnaweza mkasema mimi tu nashangaa, hata Babu Poulsen alishangaa nchi yenye watu karibu milioni 40 ina timu 12 tu za ligi kubwa kabisa ndani ya nchi na mchezaji anacheza mechi zisizozidi 22 tu kwa mwaka, ambazo kamwe hazitomfanya kuwa fiti tofauti na malengo ya FIFA ya mechi 40.
Hali hii imempa mashaka makubwa Babu Poulsen na kubaini kuwa kuna matatizo katika mfumo wa soka la nchi yetu.
Aidha, Babu Poulsen amegundua kati ya timu 12, zaidi ya nusu ya hizo, yaani saba zinatoka mikoa ya jirani, yaani Dar es Salaam na Morogoro na zingine kila moja inatoka Songea, Dodoma, Mwanza, Kagera na Arusha, mikoa yote iliyobaki haina hata ligi daraja la nne, wana ligi moja tu wameipa jina Ligi ya TFF, naduwaa!!
Mikoa ya Manyara, Mtwara, Singida, Rukwa, Mara, Lindi, Tabora, Kigoma, Kilimanjaro, Tanga, Shinyanga, Mbeya na mingineyo, ndio giza totoro, soka limekufa!
Wajumbe wao wa TFF, wanasuburi uchaguzi tu wapande ndege waje Dar es Salaam na wavute ‘mpunga' wao, kwao wenyewe hiyo tosha kabisa, wanasema soka sasa ndio limekua tofauti na zamani, mi' ndio hapo nashangaa, jamani mie mtu wa bara huenda Kiswahili sijui vizuri.
Leo Kombe la Chalenji linachezwa mara tatu ndani ya ardhi yetu, tayari giza limetanda sijui itakuwaje, tulitakiwa twende fainali za mataifa ya Afrika Ghana, tumeshindwa!
Twende Angola tumeshindwa! Twende Afrika Kusini Kombe la Dunia ndio kabisa tumeshindwa! Tumebaki tunasema uongozi ahaa bwana safi, tofauti na zile enzi za Chalenji 1994 au Kakakuona 1992 au Mataifa huru 1980, sasa huu usafi gani?
Mimi urafiki wa mshumaa siuwezi unawaka huku unateketea, sitaki kabisa nitasimama kwenye ukweli, napenda nione mataji basi na sio kauli nyingine.
Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi, waziri mwenye dhamana ya michezo nchini, binafsi nakupongeza sana kwa kuchukua nafasi hii inayogusa hisia za watu moja kwa moja bila kujali elimu zao. Mheshimiwa utapata maneno mengi kutoka kwa watu wa aina mbalimbali, yaani wenye elimu ya juu kabisa hadi wale wa Ngumbalu na wote hao watakwambia wanalijua soka.
Mkuu wa nchi amekuamini, na moja ya maneno hayo utakayoyapata, mojawapo ni kutoka kwangu: TFF wameuharibu mfumo mzuri tuliokuwa nao awali wa ligi, onyesha makucha yako kama alivyofanya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli kwa kumbana mbavu Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara nchini, (TANROADS) na wewe shusha rungu lako kwa wale waheshimiwa wa pale mjengoni TFF, yaani Karume.
Shirikiana na wizara husika ili kurudisha thamani ya mwalimu shuleni, ili wapate fedha za kutosha na kwa wakati, ili wasishughulike na masomo ya ziada wala kuuza visheti, ili wajikite kufundisha kwa bidii wakati wa masomo, ili jioni vijana wetu tuwaruhusu wawepo michezoni.
Shirikiana na wizara husika, kuhakikisha wananchi wanarudishiwa viwanja vya wazi ili watoto wao wapate mahali pa kuchezea, shule nyingi leo zinaanzishwa hazina hata viwanja vya michezo, ni hatari kweli kweli.
Shule leo hii, eneo la kiwanja inajengwa shule nyingine, sijui watoto wetu watacheza wapi! Ukienda pale shule ya Msingi Kigogo, leo pembeni pana Mkwawa, Jamii haina habari na uwanja, pale Magomeni Shule ya Msingi Karume, pembeni yake kuna shule inaitwa Dk. Omary Juma ni balaa.
Ukiyafanya hayo, sasa rudisha michezo shuleni kivitendo, nje ya hapo utakuwa unatwanga maji kwenye kinu, usitegemee lolote.
Hayo ni machache tu kutoka kwangu, lakini mengi utaambiwa na wadau, kazi kwako kuchambua pumba na chuya.
Kombe la Chalenji leo liko ndani ya ardhi yetu, napata taabu kwa mfumo wetu kama kweli tutaweza kulibakisha nyumbani.
Michezo leo imekimbia, imeenda kwao, tumebaki kusifiana upuuzi.
Wako wapi wataalamu wale waliotuletea sifa na heshima mwaka 1994 kina Stephen Nemes, Dhikiri Mchumila, Deo Mkuki, Mustafa Hoza, Edibily Lunyamila, Nteze John, Mwanamtwa Kiwelu; siwaoni nabaki nashangaa, lakini kwa mfumo huu jamani hatuwezi kufika popote.