Kikwete aelekea RT
Tuesday, 14 December 2010 21:09
Imani Makongoro
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kukutana na viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) mapema Januari kuzungumza nao juu ya rekodi mbaya ya wanaridha wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Akizungumza Ikulu, Rais Kikwete alisema kuwa rekodi ya mchezo huo hapa nchini iko chini na haionyeshi kiwango kizuri kama ilivyokuwa miaka ya 1970 hadi1980 enzi za Filbert Bayi, Juma Ikangaa na Suleiman Nyambui walifanya vema katika mashindano ya kimataifa.
Wengine walioiwakilisha vema Tanzania na kuiweka katika ramani ya Dunia kupitia michezo miaka hiyo ni Girdamis Shahanga, Mosi Ali, Nzael Kyomo, Cleva Kamanya na Simon Robert Naali
"Kwa nini tunashindwa kung'ara katika mashindano ya kimataifa na kuishia kuwa wasindikizaji kila siku, nitakutana nao na kujadiliana kwa undani juu ya jambo hili", alisema Rais.
Kikwete alisema kuwa Serikali inahakikisha rekodi ya michezo hapa nchini inakwenda kama ilivyopangwa na kuiweka Tanzania katika kiwango kinachotakiwa ambapo tayari imeleta makocha kutoka Cuba kwa ajili ya kuwafundisha wanamichezo hao, lakini wanashindwa kufanya vema katika mashindano ya kimataifa.
Michezo mingine ambayo serikali imeiunga mkono kwa kulipia makocha ni Mpira wa Miguu, Netiboli, Ngumi za Ridhaa na Judo.
Tanzania haikupata medali hata moja katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyomalizika Oktoba mjini New Delhi, India, kama ilivyokuwa kwa nchi za Kenya na Uganda