Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,468
- 911,184
- Thread starter
- #741
Yanga yasajili wawili kwa Sh mil. 24
Imeandikwa na Betram Lengama; Tarehe: 16th December 2010 @ 23:00
KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam imesema imetumia Sh milioni 24 kusajili wachezaji wawili Mzambia Davies Mwape na Juma Seif wa JKT Ruvu katika dirisha dogo la usajili mwezi uliopita.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako alisema jana kuwa wachezaji hao wote jumla ya gharama zao za usajili ni Sh milioni 24 na wala si zaidi ya hapo kama ambavyo inadaiwa na baadhi ya watu.
Pamoja na kueleza kiasi hicho cha fedha, lakini Mwalusako hakuwa tayari kusema mchanganuo wa kila mchezaji. Mwape amesajiliwa Yanga akitokea Konkola Blades ya Zambia, wakati Seif anatokea JKT Ruvu ya Tanzania.
Katika hatua nyingine Mwalusako alisema uongozi wa Yanga haujafuja Sh milioni 100 za usajili walizopewa na mfadhili wao Yusuph Manji na kuwa mambo hayo yatawekwa wazi kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji.
Akizungumza jana Mwalusako alisema tuhuma hizo kwamba wametumia vibaya fedha za usajili hazina ukweli wowote.
"Hakuna ukweli wowote juu ya tuhuma hizo dhidi ya uongozi wetu fedha tulizopatiwa zilitumika kwa utaratibu mzuri na matumizi yake tutayaweka wazi kwenye kikao kijacho cha Kamati ya Utendaji ambacho ndicho kikao chenye mamlaka ya kuhoji uongozi juu ya matumizi hayo na mengineyo katika klabu," alisema Mwalusako.
Mwishoni mwa Oktoba, Manji aliandika barua kwa uongozi wa Yanga kutaka ufafanuzi wa namna zilivyotumika Sh bilioni moja walizozipata kwa kipindi cha miezi mitatu tangu uongozi huo uingie madarakani.
Hata hivyo Mwalusako hakubainisha ni lini kikao hicho cha Kamati ya Utendaji kitafanyika wala hakufafanua zaidi kuhusiana na namna fedha hizo zilivyotumika.
Aidha Katibu Mkuu huyo wa Yanga alithibitisha kushindwa kwa klabu hiyo kupata kibali cha uhamisho wa kimataifa (ITC) cha mchezaji Kenneth Asamoah raia wa Ghana hivyo hatoweza kuitumikia klabu hiyo kwa kipindi hiki.
"Tumeshindwa kupata kibali cha Asamoah, lakini endapo tutafuzu kuingia kwenye raundi ya pili ya michuano ya kimataifa tutafanya jitihada za kukipata kibali hicho ili aweze kutusaidia kwenye michuano hiyo,"alisema Mwalusako.
Pia Mwalusako alisema kiungo wa klabu hiyo Abdi Kassim ‘Babi' amewataarifu amefuzu majaribio aliyokwenda kufanya katika klabu ya Vietnam Dong Long Tam An FC, ingawa bado hajapata taarifa rasmi kutoka katika klabu hiyo.
"Babi ametueleza amefuzu majaribio yake katika klabu hiyo ya Vietnam, lakini sisi kama klabu bado hatujapata taarifa rasmi kutoka katika klabu hiyo kututaarifu juu ya hilo ili tuweze kuanza majadiliano ya gharama zetu za kuwaachia mchezaji wetu huyo,"alisema.
Yanga walishabainisha kabla ya mchezaji huyo kwenda kwenye majaribio hayo kuwa watamwachia kwa gharama ya Sh milioni 100, hata hivyo jana Mwalusako alibainisha kuwa endapo klabu hiyo inamhitaji wako tayari kuzungumza nao, ili kujua uwezo wao endapo watamudu dau hilo ama la ili walipunguze.