Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,468
- 911,184
- Thread starter
- #1,981
16 kushiriki Ligi ya Mkoa Mbeya
Imeandikwa na Joachim Nyambo, Mbeya; Tarehe: 28th December 2010 @ 23:50
TIMU 16 zimethibitisha kushiriki Ligi ya Taifa ngazi ya Mkoa wa Mbeya inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali vilivyopo mkoani hapa mapema mwakani.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chama cha Soka mkoani hapa (MREFA) Laurence Mwakitalu timu hizo ni pamoja waliowahi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara mwaka 1988, Tukuyu Stars, Eagle FC, Vijana FC, Chipukizi FC, Bondeni FC na Kijiweni FC.
Timu nyingine ni Super Marine FC, Buffalo FC, Ilongo Shooting Stars, Mbalizi Super Stars, Wenda FC, Ibara FC, National FC, Airpot Rangers, Zaragoza FC na Eleven Boys.
"Timu hizo zote zimeshachukua na kurejesha fomu kwa gharama zilizokuwa zimewekwa hivyo kwa sasa tunaangalia taratibu nyingine ili kuanza kwa ligi hiyo," alisema.
Hata hivyo Mwakitalu alishindwa kutoa tarehe kamili ya kuanza kwa ligi hiyo kutokana na kile alichoeleza kutofanyika kwa kikao cha uchambuzi wa fomu zilizochukuliwa na timu hizo kilichoshindwa kufanyika Desemba 20 kutokana na mahudhurio ya wajumbe kuwa hafifu.
Alisema kuahirishwa kwa kikao hicho kulisababisha kutoanza kwa ligi hiyo Desemba 27 kama ilivyokuwa ikitarajiwa hivyo kuwataka wajumbe husika wakiwamo makatibu wa timu zitakazoshiriki pamoja na viongozi wa vyama vya soka katika wilaya husika kuhudhuria katika kikao kitakachofanyika Januari 3 mwakani.
Kuchelewa kuanza kwa ligi hiyo kunamaanisha kuchelewa kumalizika kwake kinyume na kalenda ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kutokana na Mkoa wa Mbeya kuwa na timu nyingi zinazoshiriki kutoka wilaya mbalimbali ambazo pia ni nyingi tofauti na ilivyo katika mikoa mingine.
Kalenda ya TFF inaelekeza ligi hiyo kuanza kabla ya Januari 5 na imalizike kabla ya Februari 28.





















