Yanga waifuata Dedebit usiku wa manane
Thursday, 10 February 2011 21:05
Jessca Nangawe
WACHEZAJI na viongozi wa Yanga, wameondoka usiku wa manane wa kuamkia jana kwenda Addis Ababa, Ethiopia tayari kwa mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya Dedebit ya huko.
Mchezo huo utakaokuwa wa marudiano, Yanga inatakiwa kushinda ama kutoka sare ya mabao zaidi ya manne, kwani chini ya hapo, Dedebit watakuwa na faida ya kuwa na mabao ya ugenini. Katika mchezo wa kwanza, timu hizo zilifungana mabao 4-4.
Wachezaji wa timu hiyo, wameondoka kwa matunaini makubwa ya kuhakikisha inashinda ugenini chini ya kocha wa mpya, Sam Timbe na msaidizi wake, Fred Felix Minziro.
Pamoja na kuwa na kibarua cha ziada kuivusha timu hiyo, nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa alisema kwa niaba ya wenzake kuwa wana matumaini makubwa licha ya kudai wanakwenda kukutana na timu ngumu ambayo wanaifahamu kwa kiasi kikubwa na wanahitaji kupambana kwa kila hali ili kurudi na ushindi.
"Tumekutana na Dedebit katika mchezo wa kwanza, tumeona uwezo wao na mbaya zaidi tulitoka sare hivyo tunahitaji kukaza buti zaidi katika mchezo huu ili tushinde, tunaamini kabisa matokeo haya ndiyo yatatupa sisi," alisema Nsajigwa.
Kwa upande wa beki wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema watahakikisha wanapigana vema na kuongeza juhudi pamoja na maarifa ili kushinda kwani hiyo ni nafasi ya mwisho kwao katika kusaka tiketi ya kuwania Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.
Naye kiungo wa timu hiyo, Godfrey Bony alisema kutakuwepo na ushindani mkubwa katika mchezo huo kutokana na wao kuwa ugenini na awali kukubali sare hivyo anategemea kuwepo na kazi kubwa ya kufanya ili waweze kushinda .
"Unajua bora tungeshinda ,nyumbani tungeweza kuwa na matumaini makubwa, lakini tunajipa moyo kutokana na kuwa mwamuzi wa mwisho wa mchezo ni filimbi ya mwisho...na tunaamini kwa kudra za Mungu tutashinda," alisema Bonny.
Yanga imeondoka ikiwa na jumla ya wachezaji 26 ambapo katika mchezo wa awali ilikubali sare ya magoli 4-4 nyumbani dhidi ya Dedebit ya Ethiopia na endepo itavuka hatua ya kwanza itakutana na Haras el-Hodood yenye maskani yake, Alexandria nchini Misri .