Michikichi fursa inayoweza kuwatoa kimaisha wakulima wengi

Michikichi fursa inayoweza kuwatoa kimaisha wakulima wengi

Joined
Aug 15, 2022
Posts
21
Reaction score
51
Licha ya Tanzania kuwa na hali ya hewa inayoruhusu uzalishaji wa zao la michikichi, uzalishaji wake uko chini ukilinganishwa na nchi zianzozalisha kwa wingi kama vile Malaysia na Indonesia.

Ni kwa sababu hii Tanzania hujikuta ikiagiza karibu tani 400,000 za mafuta ya mawese ili kukidhi mahitaji ya mafuta yanayokaribia tani 600,000 kwa mwaka, huku pia ikizalisha tani 210,000 kutoka kwenye mazao mengine kama vile alizeti, karanga, ufuta, pamba na mawese.

Kuepuka matumizi makubwa ya fedha zinazotumika kuagiza mafuta haya, wakulima wanaweza kuchangamkia kilimo cha michikichi, ambacho ni aina ya kilimo kinachokubali katika maeneo mbalimbali nchini.

Hata ulimaji wake hauna ugumu sana ikiwa mkulima atafuata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa kilimo. Kwa sasa zao la michikichi linaelezwa kufanya vizuri zaidi katika mkoa wa Kigoma ambapo asilimia 80 ya mafuta ya mawese yanazalishwa mkoani humo.

Hata hivyo, uzalishaji huu unakwazwa na matunzo na mauzo ya mafuta hayo kwa kuwa wakulima wengi hawafuati misingi ya biashara. Mbali ya Kigoma, mikoa mingine inayoweza kustawisha zao hilo ni Pwani, Mbeya (hasa wilaya ya Kyela), Tanga, Tabora, mabonde ya mto Rufiji na Kilombero.

Fursa kwa wakulima
Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2017, imeonekana kuwa uuzwaji wa mafuta hayo umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka na hivyo kutoa fursa mpya ya wakulima wa zao hilo kimasoko.
Ni kutokana na fursa hiyo, Serikali sasa imeamua kuwekeza kwenye zao hilo ili kuongeza uzalishaji na kuziba pengo la uagizwajii wa mafuta hayo kwa matumizi ya ndani.

Mapema mwama huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea Mkoa wa Kigoma na kuitaka Wizara ya Kilimo kusimamia mkakati wa kuendeleza kilimo cha michikichi mkoani Kigoma, ili zao hilo lilete mapinduzi ya kiuchumi nchini.

Alisema kuwa mkakati uliowekwa katika kusimamia zao hilo ukitekelezwa, una mchango mkubwa kwa zao hilo kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya nchi.

Akikagua uzalishajii wa mbegu bora za michikichi, alipotembelea kituo cha utafiti wa michikichi Kihinga wilaya ya Kigoma, alisema kuwa ni lazima zao la michikichi lilete tija kwenye uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wakulima wa zao hilo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Dk Geofrey Mkamilo anasema baada ya Serikali kutoa kipaumbele kwa zao hilo, sasa wameanza kufanya utafiti wa mbegu bora. Alikitaja kituo cha utafiti wa michikichi cha Kihinga kilichoanzishwa kwa ajili hiyo kuwa kitazalisha mbegu zitakazozalisha chikichi tani tano hadi nane kutoka tani 1.5 za sasa kwa hekta moja.

Baadhi ya kampuni zimejitokeza kuwekeza kwenye zao hilo ikiwa pamoja na African Green Oil iliyoripotiwa kuwa na mpango wa kuendeleza hekta 20,000 ifikapo mwaka 2025. Hadi mwaka 2009, kampuni hiyo ilikuwa imepewa hekta 5,000 na ilipanda hekta 435 kwa ajili ya majaribio.

Katika Wilaya ya Bagamoyo iliyopo mkoani Pwani, kampuni ya Tanzania Biodiesel Plant ilikuwa na hekta 16,000 kwa ajili ya kilimo hicho wakati kampuni ya Infenergy ilikuwa imepewa zaidi ya hekta 5,000 katika wilaya ya Kilombero kwa ajili ya lengo hilohilo.
Maeneo mengine yanayotajwa kufaa kwa kilimo hicho na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha mawese kwa wingi ni pamoja na mabonde ya Mto Rufiji na Kilombero.

Hali ilivyo kwa sasa
Wakulima wa Tanzania wamekuwa wakilima zao hilo kwa mazoea na siyo kibiashara. Kwanza mbegu wanazotumia hazina uwezo wa kuzaa matunda mengi na pia matunda hayo hayana kiasi kikubwa cha mafuta.

Mbegu za asili zinazotumika huzalisha tani moja hadi tatu kwa hekta moja na mafuta chini ya asilimia 8, wakati mti wa kisasa wa mchikichi huweza kuzalisha tani 12 hadi 40 za matunda kwa hekta moja ikwa pia na kiasi cha asilimia 25 hadi 30 za mafuta.
Kama wakulima watalima aina hiyo watapata masoko haraka kwani mazao hayo ndiyo yanayotakiwa na wawekezaji.

Nchi zinazozalisha mafuta mawese kwa wingi huzalisha kwenye mashamba makubwa yanayomilikiwa na vikundi vya wakulima. Lakini kwa Tanzania na hasa Kigoma, hakuna mashamba makubwa wala hakuna vyama vya wakulima wa michikichi. Wakulima wenyewe hawana taarifa za kutosha kuhusu masoko na hivyo kulifanya zao hilo kukosa mwelekeo wa kimasoko.

Kwa mfano nchi ya Malaysia ilizalisha tani milioni 20 za mafuta ya mawese katika mwaka 2015, ambazo zilikuwa asilimia 32 ya jumla ya uzalishaji wa kimataifa ambao ni tani milioni 62.8 kwa mujibu wa Bodi ya Mafuta ya Mawese ya Malaysia (MPOB).

Kwa mujibu wa Ripoti ya mwaka ya utafiti wa sekta ya kilimo (AASS 2016/17) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa eneo lililopandwa miti ya michikichi mwaka 2016/2017 lilikuwa hekta 9,742 lakini ni asilimia 79.2 tu ya miti hiyo ilivunwa.

Hii inadhihirisha kuwa licha ya jitihada za wakulima kulima zao hilo bado hawafaidiki inavyotakiwa na zao hilo kutokana na kukosa mbinu bora za kulima na masoko ya uhakika hapa nchini.

Hata hivyo, mabonde ya Rufiji mkoani Pwani na Kilombero (Morogoro) yanatajwa kuwa maeneo mapya ya kuendelezwa kwa ajili ya kwa kilimo cha michikichi, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini.

Mafuta ya mawese pia yanafungua fursa ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza sabuni na kutoa ushindani kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa hiyo nchini.
Wilayani Kyela, tayari wajasiriamali kama Nuru Njumbo ameanza kutengeneza sabuni hizo lakini ameileza Nukta kuwa changamoto inayowakabili ni upatikanaji wa mawese kwa wakati kutokana na uzalishaji mdogo wa zao hilo.
Nyongeza kwa hisani ya mtandao wa www.nukta.co.tz
 
Vijana wa JamiiForums kuna fursa ya kutajirikia huku. Kuna wakati inabidi mpumzike zile nyuzi za kina rikiboy na kina To yeye za kula tunda kimasihara.
Usipobadili mtazamo wako hapa JF na kuiga maisha ya mkumbo utapitwa na vingi.

Majukwaa yenye wachangiaji wachache ndio yenye fursa
 
KANUNI ZA KILIMO BORA CHA MCHIKICHI

Code:
Miongoni mwa kanuni ya awali kabla ya zote ni Kuchagua eneo.

Kanuni hii ni muhimu sana nayo inavigezo vyake ambavyo ni pamoja na:-

1. Liwe mabondeni lisilotuamisha maji muda wote. Lakini kama yanapita au kama yale ya maji ya mito kufurika ni mahala pake. Au yasichukue muda mrefu.

2. Iwe pembenzoni mwa vyanzo vya maji kama mito, bahari, Ziwa lakini usipande kwenye maji.

3. Isiwe kwenye vilele vya milima au kwenye miinuko mikubwa. 

4. Udongo tifutifu ndo unafaa sana. Mfinyanzi sana haufai ispokuwa ikiwa ni pembenzoni mwa mito, maziwa na bahari au mabondeni hata kama ni mfinyanzi itafanya vizuri sana.

5. Shamba lako liwe sehemu inayofikika kirahisi hasa kwa vyombo vya usafiri kama pikipiki na gari, rahisi kupeleka vitendea kazi wakati wa shughuli za mashambani ikiwemo na ikiwezekana unaweza kuweka barabara katika shamba lako.

6. Shamba lisiwe mbali na chanzo cha maji cha uhakika kwaajili ya uchakataji. Mashine za kukamua mawese huhitaji maji katika uchakataji wake.
Vyanzo hivi vya maji vyaweza kuwa Mtandao wa bomba za maji za uhakika, mito, ziwa, bahari na bwawa.



Jinsi ya kuandaa shamba la mchikichi .

Safisha shamba kwa kiwango cha kutokuwa na kichaka wala miti mingine shambani wala nyasi.

Chimba mashino kutegemea na upatikanaji wa samadi. Mfano unaweza kuchima mche mraba wa upana sm 75 urefu sm 75 na kina sm 75. Na yachimbwe kwa umbali wa mita 9 kwa mita 9 yaani kutoka shimo hadi shimo na mstari hadi mstari kutengeneza Mraba.

Changanya samadi yako na udongo uliouchimba wa juu weka kwenye chimo.
Au kama upatikanaji wa samadi ni changamoto waweza kupanda bila mbolea baada ya mwezi mmoja ukaweka NPK.

Hali ya hewa
Mchikichi unastawi ukanda wa jotojoto, na wenye mvua za kutosha. Kwani ilinuweze kuzaa sana unahitaji maji ya kutosha. Ndio maana kipindi cha masika michikichi inazaa sana kuliko kipindi cha kiangazi.

Mikoa inayostawi mchikichi

Mchikichi unahitaji maeneo ya mabondeni naam miinuko midogo kutoka usawa wa bahari.
Hivyo basi mwinuko wa mita chini ya 1500 kutoka usawa wa bahari ndo mchikichi hufanya vizuri.

Maeneo sahihi kwa mchikichi ni Mabonde na yanayopitisha maji kama kando kando na pembezoni mwa mito, bahari na maziwa. Hivyo basi maeneo yote ya kuzunguka ziwa Victoria kama Mara, Mwanza, Geita na Bukoba itafanya vizuri sana.

Maeneo yote ya kuzunguka au mwambao wa ziwa Tanganyika kama Kigoma, Rukwa na Katavi itafanya vizuri sana.

Ziwa Rukwa mkoa wa Rukwa itafanya vizuri.

Ziwa nyasa kama wilaya ya Nyasa itafanya vizuri. Manyara itafanya vizuri mwambao wa ziwa manyara.

Mwambao na bonde la Bahari ya hindi kama Pwani, Mtwara, Lindi, DSM itafanya vizuri sana ispokuwa karibu na mikondo ya chumvi

Mabonde ya mito kama Mto Wami, Rufiji, Malagarasi, Kilombero, Kagera, n.k haya yote yanastawi mchikichi.
Mabonde yanayopitisha maji kwa muda mrefu naam yale yote yanayolimwa mpunga ni maeneo sahihi kwa mchikichi.
Angalizo: Eneo linalopitisha maji hakikisha unapanda mchikichi ambao tayari ni mkubwa kwa kimo na wenye afya nzuri.

Upandaji
Mche unapandwa ukiwa na umri usiopungua mwaka mmoja kwenye kitalu. Na namna ya upandaji nimeeleza hapo juu.

Matunzo

Mchikichi ni zao lenye gharama nafuu katika utunzaji wake, kwani halishambuliwi na wadudu kama umepanda iliyofikia umri wa kupandwa.
Matunzo muhimu ni palizi na kutifuliatifulia ili kuiwezesha mizizi yake kupenyeza zaidi kwenye udongo.

AINA YA MBEGU ZA MICHIKICHI

Aina za michikichi ni tatu, yaani Dura, Bubu na Tenera .

```Mbegu nzuri sana ni Tenera kwani hutoa mafuta mengi sana na huwa na kiini cha ndani yaani Mse ambao nao hutoa mafuta yaitwayo mafuta ya mise mafuta haya ya yana thamani mara mbili ya mafuta ya mawese
Code:
 .

 *UPATIKANAJI WA MBEGU BORA* 

Taasisi ya utafiti tanzania *TARI, ASA, Magereza na Halmashauri* hasa halmashauri za mkoa wa *Kigoma* wanakuwanazo mbegu bora na hawauzi miche.

Miche hutokewa BURE kwa wakulima. Japo kutokana na uhitaji kuwa mkubwa unaweza kuomba usipate kwa kiasi ulichoomba au wakati mwingine ukakuta  imeisha. 

Hivyo basi, taasisi na watu binafsi wanakuwa nayo hiyohiyo miche bora aina ya TENERA na huiuza kwa bei tofauti kutegemea na gharama binafsi za uzalishaji.

Hivyo wanakuwepo wazalishaji binafsi wa miche.
Ukihitaji miche unaweza kuniona nikuunganishe na wazalishaji waliopo karibu na unakotaka kuwekeza.

 *KIPINDI KIZURI KWA KUPANDA MICHE YAKO* 
Muda mzuri wa kupanda hutegemea na maeneo ulipo au unapotaka kuipanda.

1. Kwa maeneo ambayo wana mvua za Vuli pamoja na za Masika muda mzuri sana ni kuipanda mwanzoni mwa mvua za vuli. Kufika mwisho wa mvua za masika mche unakuwa umeshika au kustawi vizuri.

2. Kwa maeneo ambayo wana mvua za masika tu, muda mzuri wa kupanda ni mwezi Januari mwisho Februari katikati kama tarehe 15 hadi 20.

3. Kwa maeneo ambayo huwa yanafurika maji hasa pembezoni mwa mito unaweza kuipanda hata Kiangazi kipindi maji yakiwa yametoka (kupungua sana/ kipindi cha ukame).
Maeneo ya namna hii unatakiwa upande mche wenye umri zaidi ya miezi 10

 *Angalizo* : ```Kuipanda nje ya msimu au mwishoni msimu wa mvua kama hauna miundombinu ya umwagiliaji inaweza kupata stress ya ukame hasa pale juwa litakapowaka kabla haijajishikiza vya kutosha kwenye udongo. Lakini hata hivyo haiwezi kukauka
.

KILIMO MSETO KWA MCHIKICHI


**************************
Na Bishirangonga A. N
Bwana shamba .

Mchikichi ni zao ambalo ikiwa bado midogo inakuruhusu au inafaa uchanganye na mazao mengine.

Miongoni mwa mazao yanayoruhusiwa kuchanganya na michikichi ni pamoja na mazao ya muda mfupi kama vile Mahindi, Alizeti, maharage, mtama, karanga, Tumbaku, Pamba na mazao ya mbogamboga na bustani.
Mazao ya muda mrefu na wa kati kama Migomba yanaruhusiwa.

Mazao ambayo haishauriwi kuyalima kwenye michikichi ni pamoja na Muhogo kwakuwa muhogo ni miongoni mwa mazao yanayonyonya rutuba ya udongo sana hasa Kirutubishi cha Potasiamu

Faida za kulima kilimo mseto kwenye Michikichi:-

1. Utakuwa unaitumia ardhi vizuri yaani kiuchumi. Eneo hilo hilo unatunza mchikichi wakati huo unapata mavuno kutoka mazao mengine.

2. Itakuwea vyepesi kulihudumia shamba. Kwani ukifanya palizi na mchikichi utakuwa umeupalilia.

3. Zao la mchikichi litakuwa salama na majanga hasa ya moto. Kwani wengi wakilima bila kuchanganya na mazao mengine huwa inawawea vigumu kufanya la mara kwa mara na kwa wakati pamoja na kulitifulia zao.

4. Baada ya kutoa mazao yako unaufanya mchikichi ukue kwa kasi.

Zingatia: Unapofanya kilimo mseto hakikisha karibu na mchikichi haupandi kitu kingine yaani uuache mmea wa mchikichi huru kuanzia mita 1.5 pande zote bila kupapanda chochote .

Kufanya kilimo mseto husaidia mchikichi kukua haraka hivyo kupelekea kuanza kuzaa mapema.

Ushauri zaidi: Kwa maeneo yanayolimwa tumbaku, nashauri mlime, mseto na tumbaku. Tumbaku ni zao kwa kanuni zake linalotumia mbolea nyingi hasa NPK (10:18:24 au 17:17:17). Hizo mbolea nyingi hupenyeza hadi kwenye mchikichi hivyo kulifanya zao letu la Mchikichi kuwa na afya nzuri sana. Lakini pia wakulima wa tumbaku hujitahidi sana kufanya palizi mara kwa mara.

Japo kama hautatumia mbolea nyingi kwenye Tumbaku hasa NPK basi usichanganye na Mchikichi kwani Tumbaku huhitaji potasium nyingi sana ambapo hata mchikichi huhitaji kirutubishi hikihiki kwa kiwango kikubwa.

Hata ufugaji wa wanyama na samaki kwenye mashamba ya mchikichi ni mahala pake. Unaweza kufuga wambuzi, Kuku, ng'ombe, Ngurue, Sungura, Kondoo, n.k

Angalizo : Ufugaji wa Mbuzi, Kondoo na Ng'ombe uanze mchikichi ukiwa angalau na umri wa miaka 5 hapo hawawezi kula majani yake kwani unakuwa umeshakuwa mrefu.

KANUNI ZA UVUNAJI WA CHIKICHI/MIKUNGU

Mafuta na mazao yote ya michikichi ubora wake huanzia shambani naam wakati wa mavuno.


1. Mkungu wa chikichi baada ya kuvunwa unatakiwa ukamuliwe mapema kabla ya masaa 48 yaani siku mbili. Na inashauriwa vizuri zaidi ukamuliwe ndani ya masaa 24.

Pia sio muda wa kukamuliwa tu baada kakatwa, bali hata kukatwa au kuvunwa inatakiwa uvunwe kwa wakati/ mapema mara tu unapoiva.

Madhara ya kukamua michikichi ambayo imekaa muda mrefu ni kama yafuatayo
A. Mawese kuwa na tabia ya kukereketa kooni. Na hii ndo inasababisha baadhi ya watu kutoyapenda mafuta ya mawese kwani unakuta mtu kwa mara ya kwanza kuyatumia alitumia yale yaliyotengenezwa kwenye ngazi au chikichi zilizo haribika zinazokereketa kooni.
B. Husababisha mawese kutoa harufu. Unakuta chikichi limeshaanza kutoa uvundo.

2. Uhusiano kati ya kilimo cha michikichi na Ufugaji wa nyuki .

Uhusiano upo, mosi ua dume na ua jike la chikichi huwa yanapendwa na nyuki sana.

Pili michikichi hutengeneza msitu wake hivyo kuwafanya nyuki kuwa rahisi kupata chakula na maji.

Tahadhali: Mizinga ya nyuki isiwe ndani ya shamba la michikichi. Kwani shughuli za uvunaji wa michikichi hasa ikishakuwa mirefu huhusisha kudondosha makuti na mikungu ya chikichi kitu ambacho kwa nyuki itakuwa kama usumbufu kwao hivyo wanaweza kujihami wakihisi wamevamia.

Hivyo mizinga ya nyuki iwe nje ya shamba kidogo kama tufanyavyo kwenye alizeti.


MAZAO YA MCHIKICHI NI MENGI NA YANA KAZI NYINGI SANA .

Mchikichi soko lake linaanzia kwenye:-

1. Mafuta ya kupikia.
Kila uonapo moshi ukifuka kwenye majumba ya watu ujue wakati wa mapishi lazima mafuta yatumike.
Na haya mafuta ya kupikia kutoka kwenye mchikichi yapo ya aina nyingi kutegemea na mchakataji na mahitaji ya soko kama vile mawese, mafuta ya mise, korie, makoto, n.k

2. Mali ghafi katika utengenezaji wa mafuta ya kujipaka na vipodozi.
Vipodozi vingi na mafuta ya kujipaka yanatokana na zao la mchikichi na nazi. Ubunifu wa mtengenezaji ndo kiongozi katika uhitaji wa mali ghafi hii. Hapa tutahitaji vijana wengi wabunifu wawekeze vyakutosha kwenye viwanda vya vipodozi.

3. Mali ghafi muhimu na iliyo bora katika utengenezaji wa sabuni za miche za unga.

Kila uonaye kavaa nguo safi ujue imefuliwa na sabuni yenye nguvu ya kuondoa uchafu. Sabuni inayotengenezwa kwenye mafuta ya mise ni bora sana na huwa na nguvu kubwa ya kuondoa uchafu kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa povu jingi kuliko sabuni yoyote ile unayoifahamu.

Hizo ni baadhi ya faida kubwakubwa za kisoko kwa zao hili.

Zipo faida za kienyeji zisizo za kiushindani kwenye masoko kama:-
1. Yale makuti yake yanafaa na hutumika kuezekea nyumba, kutumika kama kuni na fagio.
2. Mchikichi ukizeeka waweza kuutumia kutengenezea Pombe maarufu kama Malovu. Pombe hii ni pombe kali sana.
Pia mti huu unaweza kuutumia kutengenezea mizinga ya nyuki 🐝.

3. Pia mti wa Mchikichi unaweza kutumika kutengenezea samani nyepesi. Kama meza n.k.

Fursa ya zao hili ukihusianisha na idadi ya watu.

Kwa kadri tuongezekavyo ndivyo mahitaji ya mafuta ya kupikia, sabuni na vipodozi huongezeka. Hivyo bado soko litaendelea kuwa kubwa sana.

Nchi zinazotuzunguka uzalishaji wake hauwezi kututisha kwani hata uzalishaji wao haujatosheleza mahitaji yao ya ndani.
Bado tunaweza kuwauzia .

Asanteni sana
 
Mm natafuta Mbegu za Tenera ndio najua ziko productive. Ukiweza kunielekeza niko tayari kwa kilimo hicho hata kesho. Tenera ni very productive na ndizo wanazotumia west Africa, Malaysia, Indonesia.. Nilipata kampuni moja inaitwa Palmelet wana branch nchini Benin lakin nikaogopa vibali vingi vya import ya germinated seeds
 
Mm natafuta Mbegu za Tenera ndio najua ziko productive. Ukiweza kunielekeza niko tayari kwa kilimo hicho hata kesho. Tenera ni very productive na ndizo wanazotumia west Africa, Malaysia, Indonesia.. Nilipata kampuni moja inaitwa Palmelet wana branch nchini Benin lakin nikaogopa vibali vingi vya import ya germinated seeds
Zipo TARI Kihinga, na kuna kambi ya JKT na gereza huko Kigoma wanazo pia kuna wakulima wapo Kigoma wanauza miche.
 
Back
Top Bottom