Waswahili walinena kutueleza kwamba kawaida nikama sheria yaani kwa kawaida mwanadamu akikizoea sana kitu hufikia hatua akafikiria kwamba ni sheria. Wakati mwingine kuna mambo ambayo tunayafanya na tukimuona mtu hayafanyi tunamshangaa.
Kama ulivyo msemo huo kwa muda mrefu sasa kumekua na Shahada ya muda mrefu kwenye vyuo vyetu vikuu hapa nchini, shahada ambayo sio rasmi na wala sio sheria, lakini imekuwepo na inaendelea kuwepo kwa vile wahusika wameshindwa kusoma alama za nyakati.
Hata mimi sikuwahi kuifanyia shahada hiyo tafakuri jadidi lakini Makala ya Dk. Shoo kwenye gazeti la Rai tarahe 17 Mei mwaka huu ilinifungua macho na kunifanya niifikirie shahada hii kwa kina.
Shahada hii sio nyingine bali ni ile ya mgomo ambayo msomi wa nchi hii ambaye hakuwahi kugoma akiwa chuo kikuu anaonekana kama mtu wa ajabu, ni mtu wa ajabu kwa sababu kama ilivyo kwamba kawaida nikama sheria na ndivyo ilivyo kwenye vyuo vyetu..
Dk. Shoo aliitaja kama shahada ambayo mkufunzi wake hafahamiki na pengine hata muanzilishi pia huenda hafahamiki na hata faida yake au kazi anayotarajiwa kuipata mwanafunzi baada ya kuhitimu pia haifahamiki.
Lakini pamoja na makala ile ya Dk. Shoo, kilichonisukuma zaidi mimi kuandika makala hii ni mgomo wa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wa tarehe 4 Juni.
Mgomo huo ulikua unakusudia kuushinikiza uongozi wa chuo hicho uwarudishe chuoni wenziwao wanne waliofukuzwa kutokana na mgomo wa awali wa kushinikiza bodi ya mikopo iongeze fedha za mafunzo kwa vitendo na ada ambayo inatolewa kwa asilimia 40 tu.
Wanafunzi wa IFM wanaushangaa uongozi wa chuo kuwasimamisha viongozi wao akiwemo Rais kwa madai eti aliongoza mgomo. Wao wanasema kwamba kimsingi Rais hakuhusika na maandalizi ya moja kwa moja ya mgomo. Wala hakushinikiza wanafunzi wagome.
Pia wanasema kwamba ni uvivu wa kufikiria wa viongozi wa chuo hicho na kuto kuona mbali pia kushindwa kusoma alama za nyakati ambako kumewapelekea kutoa maamuzi kama hayo.
Kimsingi wanasema kwamba kwa Professa aliyekwenda shule, mtanzania na mwenye uzoefu wa kufanya kazi ya kufundisha au kusimamia uendeshaji wa chuo kikuu chochote nchini, lazima awe na uwezo wa kutambua kwamba sio kweli kwamba migomo inayotokea vyuo vikuu inachochewa na viongozi wa wanafunzi.
kwa mfano tukiangalia kama pale UDSM wanafunzi waligoma, sio kwa sababu Rais aliwashinikiza, ila ni kwa sababu tangu mwanzo wakati Rais anaomba kura aliambiwa kabisa kwamba suala la kugoma ili kudai haki za wanafunzi lazima liwe kwenye ajenda zake, na ndio maana alipopata nafasi hiyo wanafunzi wakamkumbushia ahadi ile na alikua hana budi afanye hivyo haya yalikua ni maneno ya mwanafunzi mmoja wa mwaka wa tatu IFM.
migomo mingine wala Rais hakuhusika. Kwa mfano mgomo wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza haukumhusisha Rais moja kwa moja, lakini lawama zote anatupiwa Rais na sisi wengine tunaonekana kama tumeburuzwa aliongeza mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Ali.
Lakini kimsingi elimu ya juu kama inavyoitwa ni ya watu wa juu, yaani watu wenye akili ya kutambua kipi kibaya na kipi kizuri, wazee wenye mvi na wajukuu kwa kifupi watu wazima.
Hii ndio maana baadhi ya wadau wanashindwa kuelewa kwamba ni kwa misingi ipi inayowapelekea wakuu wa vyuo kama wale wa IFM kufikiria kwamba kuna watu wanne tu waliowashinikiza wenzao kugoma? Na je hao walioshinikizwa hawana akili? Au nani miongoni mwa wanafunzi aliwahi kusema mimi sikugoma kwa hiyari yangu?
Hata kama kuna aliyegoma kwa shinikizo, pia lazima aulizwe aeleze kwa nini alikubali kushurutiswa na mtu ambaye hana mamlaka kwenye taasisi na wala hawezi hata kumfukuza chuo au kumchukulia hatua za kisheria? Huyu anaye goma kwa kushurutishwa ndiye anayepaswa kufukuzwa mwanzo. Nasema hivi kwa sababu huyu hajui anachotaka na mtu wa namna hiyo hata kwenye ujenzi wa taifa hatufai kwa sababu atakua mtu wa kuyumbishwa.
Lakini hebu tujiulize kumfukuza mtu chuo kuna faida gani? Nani anaweza kusimama mbele ya umma akasema kwamba ukimfukuza mwanafunzi mmoja wa kitanzania chuo kuna faida? Nchi ambayo msomi mmoja anategemewa na maelifu ya watu. Tunategemea nini tunpowafukuza wanafunzi?
Uongozi wa IMF uliwafukuza wanafunzi wanne ambao walisemekana kua ni wachochezi wa migomo. Lakini baada ya wao kua wamekushafukuzwa kukatokea mgomo mwingine wakuwataka wenzao warudishwe chuo.
Sasa kama wao ndio chanzo, wakati hawapo nani tena alikua chanzo? Je vyanzo vipya navyo vitafukuzwa chuo? Na mwisho wa mchezo huu mbaya ni nini ambacho watanzania, waliofukuzwa na familia zao zitafaidika nacho?
Nchi masikini kama Tanzania, nchi ambayo karibia asilimia tisini na tisa ya wananchi wake hawawezi kumudu gharama za kuwasomesha watoto wao elimu ya juu, tunawafukuza wanafunzi ambao kimsingi wanasomeshwa kwa mkopo. Mkopo ambao wanatakiwa waulipe na kibaya zaidi ni kwamba wakifukuzwa wanatakiwa walipe maramoja kwa mujibu wa kanuni za bodi ya mikopo.
Sasa naanza kupata picha juu ya ni nani waanzilishi wa shahada hii ambayo kimsingi viongozi wake na wasimamizi wake na waanzilishi wake ni viongozi wa vyuo husika na wizara husika kwa kushindwa kutekeleza madai ya wanafunzi na pia kushindwa kusuluhisha matatizo yanapotokea kwa njia ya busara na amani.
Kwa sababu kama yalivyo madai ya wanafunzi viongozi wa vyuo vikuu ambao ni maprofesa walitakiwa kua na uwezo wa kufikiria na kuona mbali zaidi kuliko mtu mwingine yeyote, sasa kwa nini wanajitia upofu? Hili ni suala ambalo kila anayeitakia mema nchi hii anapaswa alifikirie.
Kimsingi kumfukuza mtu chuo tukilinganisha na adhabu za kimahakama ni kama kumfunga mtu maisha. Nasema hivi kwa sababu mtu ambaye anasoma kwa mkopo anapofukuzwa chuo wala hatakua na jeuri ya kusema kwamba atakwenda kusoma sehemu nyingine kwa vile uwezo huo hana.
Nchi inayodai kufuata misingi ya kidemokrasia kama Tanzania lazima ijizatiti kuvumilia maudhi, maudhi ya wananchi wanaodai haki zao za msingi kwa mujibu wa demokrasia ambayo imewapa uhuru wa kujieleza, kupata habari na uhuru wa kusikilizwa. Kwa sababu tangu hapo serikali hii ni ya watu kwa ajili ya watu kama ilivyo maana ya demokrasia.
Sasa kwanini tunawafunga watu midomo? Tunawafunza wataalamu ambao watakua waoga, waoga wa kudai haki zao za msingi? Tunataka wakienda kazini wakipewa kazi bila vifaa wasihoji? Kwa vile tumewajaza ujinga wa kuto kuhoji, na pindi wanapo hoji tunawafukuza chuoni.
Ipo haja ya kubadilika na kufanya mambo kisomi zaidi la sivyo kutakua hakuna maana ya mtu kuitwa Profesa kama atakua hawezi kufanya uchambuzi wa mambo. Akajua faida na hasara na akazipima halafu ndio akatoa hukumu ambayo haitalenga kumkomoa mwanafunzi.
Ukweli ni kwamba suala la kumfukuza mtu chuo linawaogofya wale wanaobaki, pia huenda likasaidia kupunguza vurugu na migomo. Lakini bado suala liko palepale kwamba faida ni ndogo kuliko hasara.
kama kweli viongozi wa vyuo vyetu wana nia ya kutusaidia, kwanini wasiwasimamishe wanafunzi kwa muda? Kwanini wanawafukuza kabisa? hili lilikua swali la mdau mmoja ambaye ni mwanafunzi.
Baadhi ya wanafunzi wanadai kwamba kuna watu amboa wanachuki binafsi na wanafunzi na huwa wanasubiria kukiwa na kosa lolote wawafukuze vyuoni kuwakomoa.
mara kwa mara vyuo vimekua vikiripotiwa vibaya kwenye magazeti na wakati mwingine miongoni mwa Maprofesa huwa wanaandikwa vibaya pia. Sasa hutoke Profesa akawashuku watu baadhi labda kwa umaarufu wao na baada ya hapo huwasubiria wafanye kosa ili awakomeshe alinena Bw. Juma ambaye ni mdau wa elimu ya juu.
Migomo Vyuo Vikuu Ni Lazima? by saiboko on Blogster